Dar es Salaam, Agosti 19, 2022: Wanahisa wa TOL Gases Limited wameidhinisha gawio la shilingi 40.00 kwa kila hisa katika Mkutano Mkuu wa Mwaka uliofanyika 19 Agosti 2022 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam.
Kampuni imeweza kukuza kiasi cha gawio ukilinganisha na gawio la shilingi 34.78 kwa hisa kwa mwaka 2020. Taarifa za fedha za kampuni kwa mwaka unaoishia Desemba 2021 zinaonyesha kukua kwa mapato kwa asilimia 25, kutoka shilingi bilioni 19.8 kwa mwaka 2020 hadi shilingi bilioni 24.8, ambapo faida baada ya kodi ilikua kwa asilimia 41 kutoka bilioni 2.3 kwa mwaka 2020 hadi bilioni 3.3 kwa mwaka 2021.
Ukuaji wa mapato ya kampuni hiyo umechangiwa na maboresho ya kiutendaji yaliyofanyika hivi karibuni sambamba na mikakati ya upanuzi iliyochangia kuimarisha nafasi ya kampuni kama mzalishaji na muuzaji wa gesi za viwandani na hospitalini pamoja na kupanua wigo wake wa usambazaji bidhaa katika nchi nyingine za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kama vile Zambia, Zimbabwe, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na Malawi.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Bodi wa kampuni ya TOL Gases, Michael Shirima, alipongeza maboresho ya kiutendaji na jitihada zilizofanywa na kampuni katika kuhakikisha upatikanaji wa hewa ya Oksijeni inayotumika mahospitalini wakati wa mlipuko wa Uviko-19.
"Kutokana na ugonjwa wa Uviko-19, mwaka 2021 ulikuwa na changamoto nyingi katika nyanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii kwa ujumla. Nina furaha kuripoti kwamba tulifanikisha lengo letu la kuisaidia serikali kuhakikisha upatikanaji wa gesi ya Oksijeni katika kipindi kile kigumu, na ninaipongeza Kampuni kwa kuhakikisha upatikanaji wa gesi hiyo muhimu katika vituo mbalimbali vya huduma za afya."
Mbali na kuripoti ongezeko la faida kwa mwaka 2021, TOL Gases Limited imeelezea mikakati mbalimbali inayotarajiwa kukuza matokeo ya kifedha ya Kampuni. Hivi karibuni Kampuni imezindua mradi wa mpya ambao ni wa pili katika Wilaya ya Rungwe na utakuza uwezo wa Kampuni wa kuzalisha gesi ya ukaa.
Akizungumzia mradi mpya wa gesi ya ukaa, Mwenyekiti alisema, "Kiwanda hiki kipya kitaongeza uwezo wa Kampuni wa kuzalisha gesi ya ukaa na kinatarajiwa kukuza mapato ya kampuni kwa kiasi kikubwa. Aidha, kampuni imewekeza katika magari mapya ya usambazaji ili kuimarisha nafasi yake kama mzalishaji na msambazaji wa kuaminika wa gesi za viwandani na hospitalini."
Mradi mpya wa gesi ya ukaa upo katika kijiji cha Ikama, Wilayani Rungwe jijini Mbeya na unatarajiwa kukuza mapato ya kila mwezi kwa takribani shilingi bilioni 8.2, ikiwa ni ongezeko la asilimia 42 la mapato yatokanayo na uzalishaji wa gesi ya ukaa pekee.
Mawasiliano:
Jina: Daudi Mlwale - Director of Sales & Business Development
Simu: +255 685 750 218
Barua-pepe: dmlwale@tol-gases.co.tz
Kuhusu TOL Gases:
- TOL Gases Limited, kampuni inayoongoza kwa uzalishaji na usambazaji wa gesi za viwandani na gesi za hospitali nchini Tanzania, ilianzishwa mwaka 1950 kama East Africa Oxygen na baadaye kubadilishwa jina na kuwa Tanzania Oxygen Limited kabla ya umiliki wake kuchukuliwa na Serikali kupitia Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) mwaka 1978
- Mwaka 1998, TOL iliorodheshwa katika Soko la Hisa la Dar es Salaam, na hadi sasa, Watanzania 10,711 wanamiliki hisa za TOL.
- TOL Gases Limited inazalisha gesi za viwandani ikiwa ni pamoja na Industrial Oxygen, Acetylene, Carbon-dioxide, Nitrogen, na gesi nyingine kama Helium, Argon, Argoshield, Ammonia, na Freon. Kampuni pia inazalisha gesi za hospitalini ikiwa ni pamoja na Medical Oxygen, Nitrous Oxide na Compressed Air.
- Gesi zinazozalishwa na TOL Gases Limited zinatumika katika viwanda mbalimbali nchini Tanzania, Afrika Mashariki na katika nchi za SADC. Matumizi ya gesi zinazozalishwa na TOL ni katika huduma za afya na matibabu ya dharura, uzalishaji wa vinywaji kama vile soda na bia, uungaji vyuma viwandani, uchomeleaji na utengezaji wa bodi za magari, uchimbaji wa mafuta na gesi asilia katika kuongeza uzalishaji na ulinzi dhidi ya ajali za moto, sekta ya madini katika ufuaji wa vyuma na dhahabu, na katika viwanda vya kusindika bidhaa kama vile maji, juisi, matunda, nyama na mboga mboga.
No comments:
Post a Comment