Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Tuesday, 9 August 2022

RAIS SAMIA SULUHU HASSAN AIPONGEZA BENKI YA CRDB, AHITIMISHA MAONESHO YA NANENANE JIJINI MBEYA


Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ameipongeza Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Serikali kubuni mfumo wa kidigitali utakaoiwezesha Wizaya ya Kilimo kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Mbolea Tanzania (TFRA) kuagiza mbolea na kuisambaza kwa mkulima, hivyo ruzuku itolewayo na Serikali kumfikia mnufaika kama ilivyokusudiwa.

Mhe. Rais ametoa pongezi hizo jana alipohitimisha rasmi Maonyesho ya wakulima Nanenane katika Viwanja vya John Mwakangale Jijini Mbeya. Mhe. Rais amezitaka taasisi za fedha na benki za biashara nchini kuendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha sekta ya kilimo inapewa kipaumbele.

“Aidha, nazipongeza benki nchini kwa kushiriki vyema katika kuhakikisha sekta ya kilimo inakua na kuleta tija nchini, niipongeze Benki ya CRDB kwa kushirikiana na Serikali kufanikisha mfumo huu kwani naamini utaleta mapinduzi makubwa ya kilimo nchini,” alisema Rais Samia.

Benki ya CRDB imekuwa kinara katika kuhakikisha inashirikiana na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar na wadau wa sekta za kilimo, uvuvi, mifugo, misitu, biashara na viwanda ikiongozwa na kaulimbiu yake isemayo “Kilimo chetu, Viwanda vyetu, Uchumi Wetu” hivyo kuongeza tija ya uwekezaji kwenye sekta hizo ikizingatiwa umuhimu wa kuunganisha wateja wote kwenye mnyororo wa thamani katika uzalishaji ili kuwapatia uhakika wa masoko ya bidhaa zao.


Mkurugenzi Mtendaji Abdulmajid wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alielezea namna benki hiyo ya kizalendo imekuwa mdau mkubwa wa sekta zote za kiuchumi nchini kwa kuwasaidia wakulima, wafugaji au wavuvi iwe mmojammoja, vikundi, vyama vya ushirika vya msingi (AMCOS), wakulima wakubwa, wafanyabiashara wa mazao ya kilimo na wawekezaji kwenye viwanda vinavyoongeza thamani ya malighafi zinazozalishwa nchini.

“Kiujumla zaidi ya 43% ya mikopo yote itolewayo kwa ajili ya kilimo nchini imetolewa na Benki ya CRDB. Kwa mwaka 2021/2022, tumetoa zaidi ya shilingi bilioni 769. Sehemu kubwa ya mikopo itolewayo na Benki ya CRDB imeelekezwa katika kilimo cha mazao ya biashara, kilimo cha mazao ya chakula, uvuvi, mifugo, uzalishaji wa malighafi za viwanda, ujenzi wa viwanda vya uchakataji wa mazao ya kilimo, utengenezaji wa pembejeo, uendelezaji wa mazao ya misitu, usindikaji na usambazaji,” alisema Nsekela.


Kwa kipindi cha miaka mitano ilyopita hadi Juni 2022, alisema Benki ya CRDB imetoa mikopo kwenye sekta ya kilimo kiasi cha TZS 2.6 Trilioni. Ikumbukwe CRDB ilikuwa benki ya kwanza nchini kutoa mikopo kwa riba ya tarakimu moja ikitoza asilimia 9 katika sekta ya kilimo.

Maeneo makubwa ambayo Benki ya CRDB imejikita katika kusaidia uwezeshaji kwenye sekta ya kilimo ni mikopo ya pembejeo na uendeshaji wa mashamba ambapo imesaidia upatikanaji wa mbolea na pembejeo nyinginezo muhimu kwa gharama nafuu. Sehemu kubwa ya mbolea inayoingizwa nchini inatokana na uwezeshaji wa CRDB.

Benki pia imebuni utaratibu mzuri wa kuagiza mbolea kupitia utaratibu mahususi wa dhamana (Letter of Credit) ambapo waagizaji wa mbolea huweza kuingiza bidhaa hii muhimu kwa kilimo kwa gharama nafuu ya asilimia 2 kwa mkopo wa fedha za kigeni na asilimia 4 kwa mwaka kwa mkopo wa shilingi za Kitanzania.

Awali, maonyesho hayo yaliyofunguliwa na Makamu wa Rais, Mhe. Dkt. Philip Mpango, alizitaka benki nchini kushirikiana na Serikali akisisitiza kuwa Benki ya CRDB inachukulia kwa umuhimu mkubwa kuziwezesha sekta muhimu zenye mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa Taifa.

“Tunafahamu kuwa Serikali yetu ya Awamu ya Sita chini ya uongozi wako Mheshimiwa Rais, imedhamiria kwa dhati kabisa, kujenga uchumi unaoshamirishwa na kilimo, uvuvi, mifugo, misitu, biashara na viwanda. Kiuhalisia sehemu kubwa ya viwanda vyetu vinategemea sana mazao ya kilimo, uvuvi na mifugo kama chanzo muhimu cha malighafi. Sisi Benki ya CRDB tupo mstari wa mbele kuunga mkono juhudi hizi kwa kutoa mazingira wezeshi ya upatikanaji wa fedha na elimu ya uwekezaji,” alisema Nsekela.


Kwa mara ya kwanza, Serikali imetenga TZS 150 bilioni kwa ajili ya ruzuku ya mbolea ili kupunguza gharama za pembejeo hii ni baada ya kutenga TZS. 1.0 Trilioni kuzipa benki nchini chanzo nafuu cha fedha kwa ajili ya mikopo nafuu kwenye kilimo.

Wateja wa Benki ya CRDB wanaweza kupata huduma za fedha kwa wakala wa CRDB, kwenye simu zao za mkononi au kwenye tawi la benki hata mashine za kutolea fedha zinazopatikana hadi vijijini.

Pamoja na jitihada hizo, Benki imeingiza sokoni akaunti maalum kwa ajili ya wakulima, wafugaji na wavuvi ijulikanayo kama “Fahari Kilimo” ikiwa ni sehemu ya mkakati mpana wa kuwahudumia wakulima kwa ukaribu kwa kuzingatia mahitaji yao. Nsekela amesema benki itaendelea kuwezesha zaidi ili kuinua uchumi wa Taifa kupitia fursa zilizopo kwenye sekta zote za uchumi.

No comments:

Post a Comment