Uzinduzi wa NMB Marathon 2022 zinazoandaliwa na Benki ya NMB, umefanyika katika Viwanja vya Leaders, Kinondoni Jijini Dar es Salaam, ukienda sambamba na mbio za majaribio za kilomita 5 na 10, na michezo mingineyo, huku mgeni rasmi akiwa ni Afisa Mtendaji Mkuu wa NMB, Ruth Zaipuna.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, ulioshirikisha waalikwa kutoka kampuni, taasisi na vikundi mbalimbali vya mbio za taratibu (jogging), Zaipuna alisema baada ya mafanikio katika mwaka wa kwanza wa mbio hizo (2021), NMB inaamini malengo ya miaka minne yatakamilishwa katika mbio za mwaka huu.
“Mwaka jana tulizindua mbio hizi za hisani tukishirikiana na CCBRT, tukaziita NMB Marathon chini ya kaulimbiu isemayo Mwendo wa Upendo. Lengo likawa kukusanya kiasi cha Sh. Bilioni 1 katika kipindi cha miaka minne, kwa maana ya Sh. Milioni 250 kwa kila mwaka.
“Lakini tukapata mafanikio makubwa yaliyotuwezesha kukusanya Sh. Milioni 400, ambazo tulizipeleka CCBRT na kusaidia kinamama mbalimbali waliokuwa na tatizo la Fistula. Mwaka huu, tumeona haja ya kuweka lengo la kukusanya Sh. Mil. 600 ili kutimiza Sh. Bil. 1 ndani ya miaka miwili,” alisema Zaipuna.
Zaipuna aliwashuruku wadhamini wakubwa wa NMB Marathon yaani Kampuni za Bima za Sanlam na UAP, pamoja na washiriki waliochangia kurejesha tabasamu kwa kinamama kwa kulipia gharama za matibabu yao, huku akiwataka Watanzania zaidi kujitokeza ili kupata Mil. 600 ili kuendelea kuwasaidia wamama wengi zaidi.
“Mbio hizi zitafanyika Septemba 24 mwaka huu, zitaanzia na kumalizikia hapa Leaders Club, ambako mgeni rasmi atakuwa Waziri Mkuu Kassim Majali, ambaye tulikuwa naye katika mwaka wa kwanza wa mbio hizi, tayari ametuthibitishia kuwa tutamaliza naye mchakato huu wa kukusanya Mil. 600,” alisema Zaipuna.
Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya CCBRT, Brenda Msangi, aliishukuru NMB kwa wazo zuri lililozaaa Mbio za NMB Marathon, ambazo zimesaidia kukusanya pesa kusaidia akina mama wanaohitaji msaada wa kitiba kumaliza tatizo la Fistula, ambalo linawakuta takribani kinamama 3000 kwa mwaka.
“Niwashukuru sana NMB kwa sababu sidhani kama kuna benki iliyowahi kutoa ahadi ya kusaidia Bilioni 1 ya matibabu ya Fistula. Tatizo hili ni kubwa nchini, kwani ukiondoa kinamama 3000 wanaopata tatizo hilo kila mwaka, wapo wagonjwa wa zamani wanaoendelea kusumbuliwa na tatizo hili.
“Kuna maeneo mawili yanayosababisha kinamama kuendelea kusumbuliwa na Fistula, la kwanza likiwa ni elimu. Jamii haina elimu ya kutosha juu ya tatizo hili, kwamba bado tatizo hili ahlielewki na jamii inawatenga wanawake wanaokumbwa na maradhi haya, yanayohusishwa na imani za kishirikina,” alisema Msangi.
Aliongeza ya kwamba, tatizo la pili ni gharama kubwa, kuanzia za usafirishaji wa wagonjwa kutoka waliko hadi hospitalini kwake, gharama za matibabu, pamoja na malazi na chakula wakati wakiendelea na matibabu, hivyo NMB imeona mbali kusaidia kada hiyo muhimu katika jamii.
Msangi alibainisha kuwa, kupitia Sh. Mil. 400 za NMB Marathon 2021, CCBRT iliweza kupambana na changamoto hizo mbili zinazokosesha tiba kwa akina mama wenye Fistula, ambazo ziligharamia tiba ya wanawake 60, pia zilitumika kuzunguka katika mikoa minne ya Rukwa, Kagera, Mtwara na Songwe kutoa elimu.
No comments:
Post a Comment