Foreign Exchange Rates

DStv Advert_020324

DStv Advert_020324

SBT Tanzania Advert_291123

Wednesday 10 August 2022

NHC KUTUMIA WATAALAMU WENYE UWEZO

Meneja Habari na Uhusiano NHC, Muungano Saguya akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dodoma kutoka vyombo mbalimbali nchini.

Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Nyumba la Taifa - NHC Nehemiah Mchechu ameandaa timu ya watalaamu yenye uwezo wa kufanya kazi kwa kuzingatia ubora licha ya vifaa vya ujenzi kupanda bei.

Hayo yamesemwa jana (tarehe 9/08/2022) na Meneja Habari na Uhusiano NHC Muungano Saguya alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari katika ukumbi wa Idara ya Habari MAELEZO uliopo jengo la PSSSF Makole jijini Dodoma.

Saguya amesema kuwa katika mwaka huu wa fedha 2022/2023 Shirika litaongeza nguvu katika uboreshaji wa makazi ya nyumba zake kwa kufanya matengenezo makubwa kwenye baadhi ya Mikoa ili kuziweka nyumba hizo katika hali iliyo bora zaidi.

“Mikoa ambayo itakwenda kunufaika na matengenezo hayo ni pamoja na Iringa, Tabora, Arusha, Kigoma, Morogoro, Lindi, Tanga , Mbeya, Mwanza, Singida, Kagera na Dar es Salaam, ambapo Shirika litatumia shilingi Bilioni 8 katika kurekebisha nyumba zake kwa kupitia Mameneja wa Mikoa husika” Alisema Saguya.

Amebainisha kuwa mpango wa matengenezo hayo ambao utaishia mwaka 2027 una lengo la kuboresha nyumba zake ili ziweze kuwa katika hali nadhifu na kutoa taswira halisi ya NHC na pia kuhakikisha wapangaji wake wanakaa katika nyumba zilizo bora zaidi.

Sanjari na hilo Meneja huyo wa Habari na Uhusiano NHC ameongeza kusema kuwa NHC itashirikiana na Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi na wadau wa sekta ya miliki nchini ili kubuni sera na sheria zitakazofanya sekta ya miliki na nyumba kuchangia uchumi wa nchi yetu.

“Kuanza utekelezaji wa sera ya ubia itakayoruhusu sekta binafsi kushiriki katika uendelezaji wa maeneo ya Shirika, Sera hii inalengo la kuharakisha uendelezaji wa maeneo yaliyo wazi kwa kujenga nyumba za vitega uchumi na hivyo kuliongezea Shirika na nchi mapato” Alisema Saguya.

Amesistiza kuwa Shirika linaendelea kununua ardhi ili kuongeza maeneo yake ya akiba ya ardhi kwa ajili ya ujenzi kwa siku za mbeleni, licha ya kwamba kwa sasa Shirika lina akiba ya ekari 2,362 za ardhi katika maeneo mbalimbali nchini, lakini pia Shirika linatarajia kuongeza ekari 400 za ardhi kwa ajili ya ujenzi wa nyumba nchini.

Amebainisha kuwa Shirika litaendelea na utaratibu wake wa kujenga viwanda ili kupunguza gharama za ujenzi kwani hata sasa katika miradi ya Shirika vipo viwanda vidogo vidogo vinavyolenga kupunguza gharama za ujenzi.

Katika hatua nyingine Saguya amesema kuwa Shirika lina lengo la kutekeleza mpango wa ujenzi wa nyumba 5,000 za ghara ya kati chini ujulikanao kama Samia Housing Scheme (SHS) wa nyumba za kuuza na kupangisha ambazo zitajengwa Jijini Dar es Salaam na kwamba 50% zitajengwa Dar es Salaam, 20% zitajengwa Dodoma na 30% zitajengwa katika Mikoa mingine nchini.

“Nyumba hizi zitaanza kujengwa kwa awamu ambapo kwa mwezi Septemba eneo la Kawe zitajengwa nyumba 500, Medeli nyumba 100 ambazo zitagharimu kiasi cha shilingi Bilioni 466 na kwamba mradi huu utachangia kutoa fursa ya ajira 26,400 kwa Watanzania” Alisema Saguya.

Sanjari na ujenzi huo Shirika litaendelea kukamilisha miradi ya Morocco Square, Kawe 711 na Golden Premium Residence (GPR) iliyopo Kawe. Pia kuanzisha miradi mingine ya ujenzi wa majengo ya biashara katika Mikoa ya Bukoba, Mwanza, Dodoma, Kahama, Morogoro, Masasi na Lindi.

Aidha, Shirika limedhamiria kuendelea na utekelezaji wa miradi ya ukandarasi ikiwemo ujenzi wa majengo ya ofisi ya Wizara 9 Jijini Dodoma, ujenzi wa shule ya Uchumi Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ujenzi wa majengo matano ya Wakala wa Ununuzi wa Serikali (GPSA), ujenzi wa jengo la TANZANITE Mererani, ujenzi wa Kitengo cha Moyo cha Jakaya Kikwete (JKCI) na miradi mingine itayojitokeza.

Shirika la Nyumba la Taifa mpaka sasa lina mtaji wa shilingi Trilioni 5.04 unaotokana na rasilimali ya majengo yake 2,650 yenye nyumba zipatazo 18,654 zilizopo katika Mikoa mbalimbali nchini.

No comments:

Post a Comment