Kitomari Banking & Finance Blog is a premier site for banking, finance, business, economic, investment and stock market news as well as selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the World. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.
Thursday, 21 July 2022
WAZIRI WA KILIMO AKUTANA NA WAKULIMA WA NJE WA MIWA KILOMBERO
Morogoro - Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe alifanya mkutano wa hadhara na wakulima wa nje wa miwa Kilombero ili kusikiliza changamoto zao katika azma ya kuhakikisha wakulima wananufaika na kilimo cha miwa. Mkutano huo wa hadhara ulifanyika Julai 17 katika kijiji cha Ruaha, Kilombero na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wadau wa maendeleo na maofisa wa Kampuni ya Sukari ya Kilombero (KSCL) ambao ni wabia wakuu wa wakulima wa miwa Kilombero.
Baada ya kusikiliza changamoto mbalimbali, waziri huyo alikuja na maazimio na maelekezo kama ifuatavyo;
Miundombinu ya Umwagiliaji:
Waziri baada ya kusikiliza kero za wananchi juu ya changamoto zinazowakabili wakulima hao, aliwaeleza kuwa serikali itatengeneza miundombinu ya umwagiliaji na kuunda tume maalum ya kusimamia kilimo cha umwagiliaji nchini ambapo ofisi za umwagiliaji za halmashauri zitasimamia uendelevu wa miundombinu hiyo. Tume ya Umwagiliaji itafanya kazi na KSCL katika kuandaa mpango mkuu wa umwagiliaji kwa ajili ya KSCL na Wakulima kabla ya kuwakilisha mpango huo katika Wizara ya Kilimo.
Mbolea:
Kufuatia changamoto za upatikanaji wa mbolea uliopelekea kupanda kwa bei ya bidhaa hiyo, Waziri aliwaeleza wakulima kuwa serikali inaendelea na mpango wa kuanzisha ruzuku ya mbolea kwa wakulima wote nchini ambayo itawanufaisha wakulima hao na kupunguza changamoto iliyopo ya ongezeko la bei.
Mbegu Bora:
Wakulima waliwasilisha changamoto zao za upatikanaji wa mbegu bora, tatizo linalochangiwa na ukosefu wa mitaji na utaalamu wa kuzalisha mbegu bora, hivyo kuathiri ubora wa mavuno yao. Baada ya mazungumzo mafupi na uongozi wa Kampuni ya Sukari ya Kilombero, Waziri aliahidi kwa serikali itaendesha kitalu cha kuzalishia mbegu ambapo wakulima watapata mbegu bora kutoka serikalini. Kampuni ya Sukari ya Kilombero ilikubali kutoa ardhi ya hekari 400 kuiwezesha serikali kuendesha mradi huo wa uzalishaji mbegu.
"Ubora wa muwa ni mchakato kuanzia mbegu iliyopandwa, namna ulivyolima, namna ulivyovuna na namna unavyopeleka kiwandani. Nimesikia kilio cha upatikanaji wa mbegu, tunaanzisha kitalu cha hekta 400 cha serikali cha uzalishaji wa mbegu hapa kwenu." - Mhe. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe
Kuboresha Mkataba wa Ugavi:
Licha ya wakulima wa Kilombero kuwa ndio wakulima wanaolipwa fedha nyingi zaidi (kwa tani) nchini Tanzania, Waziri alisema upo uwezekano wa kuboresha kiwango chao cha malipo na kuitaka Kampuni ya Kilombero na wakulima kukaa na kupitia upya mkataba wa ugavi ili kuona maeneo yanayoweza kuwaongezea wakulima mapato na pia kuimarisha uwazi katika mfumo wao wa mgawanyo wa mapato.
"Nitaunda timu itakayoongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo ili kuangalia mchakato wa maboresho ya mkataba wa ugavi na kuwahusisha wakulima ili kujianda na upanuzi wa kiwanda." - Mhe. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe
Elimu na Msaada kwa Wakulima:
Wakulima waliomba kupatiwa fursa za elimu kuhusu maeneo mbalimbali ili kuboresha kiwango chao cha mavuno kwa hekta. Kwa sasa, wakulima huzalisha wastani wa tani 20 kwa hekta na kuna uwezekano wa kukuza mavuno yao hadi tani 70 kwa hekta. Katika kukabiliana na hilo, Kampuni ya Sukari ya Kilombero ilimweleza Waziri kuwa wameanza kuwaunganisha wakulima na taasisi mbalimbali ili kuwapatia elimu na msaada katika kuboresha mbinu zao za kilimo na kukuza stadi za biashara. Mbali na hayo, kampuni imefanya maboresho katika Idara yake ya Huduma kwa Wakulima na kuongeza idadi ya wafanyakazi wa huduma kwa wakulima kutoka wafanyakazi nane (8) hadi arobaini na nane (48). Mfuko wa Maendeleo wa Tasnia ya Sukari (Sugar Industry Development Trust Fund - SIDTF) na KSCL watashirikiana na Taasisi ya Sukari ya Taifa (National Sugar Institute – NSI) na wadau wengine kuandaa programu za maendeleo ya Wakulima.
Manunuzi ya Pamoja ya Pembejeo:
Kampuni ya Sukari ya Kilombero ilimweleza waziri kuwa taratibu na mazungumzo yanaendelea ili kuingia makubaliano ya manunuzi ya pamoja ya pembejeo kati ya kampuni hiyo na wakulima, hali itakayowasaidia wakulima kupata pembejeo za kilimo kwa wakati unaostahili. Mkataba huo utaainisha muundo wa upatikanaji wa gharama za mtaji na mabohari kulingana na miongozo kutoka mamlaka husika.
Usajili wa Wakulima:
Waziri aliipongeza Tume ya Maendeleo ya Ushirika kwa kushirikiana na wadau kwa kuwezesha usajili wa wakulima wapya 2,000 katika kanzi data ya kidijitali na kufanya jumla ya wakulima waliosajiliwa kufikia 9,700. Hatua hiyo itaiwezesha serikali na mamlaka husika kufuatilia maendeleo ya wakulima ili kuwapatia misaada mbalimbali.
"Kwenye mazao ya korosho, pamba na kwenye tumbaku mkulima hatakiwi kuwa na fedha taslimu ili kununua pembejeo kwa vile tayari ana soko. Tunahitaji kujua aina na mahitaji ya mbolea na viuatilifu. Kupitia usajili wa wakulima, mabenki yatatoa fedha na mkulima atakatwa atakapouza mazao yake." - Mhe. Waziri wa Kilimo, Hussein Bashe
Upatikanaji wa Mitaji:
Waziri aliziagiza mamlaka husika kuhakikisha kuwa wakulima wote wanasajiliwa katika kanzi data ya kidijitali ili kuongeza imani kwa taasisi za kifedha na kukuza upatikanaji wa mikopo kwa wakulima. Pia alizitaka taasisi za fedha kupitia upya masharti yao ya mikopo ili kuwawezesha wakulima wadogo kupata mikopo. KSCL iliahidi kufanya kazi na wakulima hao pamoja na Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania (TCDC) ili kuvutia fursa za mitaji kwa wakulima.
Uwazi katika Vipimo Ubora wa Miwa:
Waziri huyo alisema serikali itashirikiana kwa karibu na Kampuni ya Sukari ya Kilombero katika kutengeneza mfumo utakaohakikisha uwazi kwenye vipimo vya ubora wa miwa ili kuwahakikishia wakulima kuwa wanalipwa kiasi stahiki kulingana na kiwango cha sukari kwenye miwa yao. Serikali itaunda kikosi kitakachofanya kazi na KSCL na kuripoti matokeo ya vipimo vya ubora wa miwa kwa wakulima hao wa nje.
Usimamizi wa AMCOS:
Waziri alimuagiza mrajisi wa vyama vya ushirika kusimamia kwa ukaribu shughuli za vyama vya ushirika ikiwemo katiba zao, uteuzi wa viongozi, utoaji wa zabuni, malipo kwa viongozi wa vyama ili kuhakikisha haki za wanachama zinalindwa.
Mawasiliano:
Jina: Ephraim Mafuru
Simu: +255 699 100398
Barua-pepe: emafuru@illovo.co.tz
Kampuni ya Sukari ya Kilombero:
● Kampuni ya Sukari ya Kilombero imefanya uwekezaji mkubwa wa zaidi ya Dola za Marekani milioni 166 katika biashara katika kipindi cha miaka 20 iliyopita. Uwekezaji huo umehusisha uboreshaji wa uzalishaji wa miwa na sukari pamoja na uwekezaji katika kiwanda cha kisasa chenye uwezo wa kusambaza Kilolita milioni 12 za pombe yenye ubora wa juu.
● Illovo Sugar Africa, inamilikiwa na Kampuni ya British Foods ya Nchini Uingereza kwa asilimia 75 ya mtaji wa hisa uliotolewa kwa Kampuni ya Sukari ya Kilombero, na kiasi cha asilimia 25 cha hisa zinamilikiwa na Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania.
● Kampuni ya Sukari ya Kilombero inafanya shughuli za uzalishaji wa sukari katika Mkoa wa Morogoro na inajumuisha maeneo mawili ya kilimo na viwanda vya sukari ambayo ni Msolwa na Ruembe. Kampuni inazalisha sukari chini ya chapa maarufu ya ‘Bwana Sukari’.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment