Dar es Salaam, Juni 30 2022: Balozi wa Marekani nchini Tanzania Dkt. Donald J. Wright amethibitisha nia ya Serikali ya Marekani katika kuimarisha ukuaji wa uchumi wa Tanzania kupitia ushirikiano mpya uliosainiwa katika Makao Makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam kati ya Benki ya CRDB na Mashirika ya Kimarekani ya USAID na DFC.
Kupitia ushirikiano huo, Mashirika ya Kimarekani ya USAID na DFC yatashirikiana na Benki ya CRDB kuwezesha mikopo yenye thamani ya Shilingi Bilioni 100 za kItanzania. Ushirikiano huo utaiwezesha Benki ya CRDB kutanua wigo wa uwezeshaji wa mikopo wa wanawake na vijana sambamba na kutoa mikopo zaidi katika sekta za elimu, afya na sekta zisizo rasmi Tanzania nzima.
"Benki ya CRDB inayo furaha kubwa kufanya kazi na USAID na DFC katika kusaidia biashara ndogo nchini Tanzania.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela kwa pamoja na Balozi wa Marekani nchini Tanzania, Dkt. Donald Wright wakisaini hati ya makubaliano ya mikopo ya uwezeshaji yenye thamani ya Bilioni 100 kati ya Benki ya CRDB na Mashirika ya Kimarekani ya USAID na DFC kwa ajili ya kuiwezesha Benki hiyo kukopesha sekta mbalimbali nchini zikiwemo Sekta ya Ujasiriamali, kwa maana ya wajasiriamali wadogo na wakati (MSMEs), Sekta ya Elimu, Sekta ya Afya na biashara zisizo rasmi. Hafla hiyo imefanyika kwenye makao makuu ya Benki ya CRDB, jijini Dar es salaam.
"Serikali ya Marekani inatambua kuwa hakuna chombo peke kinachoweza kutatua changamoto za Tanzania hivyo tunafurahi na kusheherekea mikataba hii miwili na Benki ya CRDB ambayo itaongeza ushirikishwaji wa kifedha na uwezeshaji kwa makundi muhimu kama vile wanawake na vijana," alisema Dkt. Donald J. Wright, Balozi wa Marekani nchini Tanzania.
Ushirikiano huu unalenga kuboresha maeneo yafutayo;
- Mikopo katika Sekta ya Afya: Benki itatoa mikopo ya hadi Shilingi Bilioni 20.3 katika sekta ya afya. Mikopo hii itatumika kusaidia katika ujenzi wa mahospitali, vituo vya afya, kliniki, vituo cha uchunguzi wa afya, maduka ya madawa na huduma za uzazi pamoja na ununuzi wa vifaa ya matibabu na ujenzi au ukarabati wa maeneo ya kutolea huduma za afya.
- Mikopo katika Sekta ya Elimu: Benki itatoa mikopo ya hadi Shilingi Bilioni 37.5 katika sekta ya elimu kusaidia katika mnyororo wa thamani wa elimu ikiwemo uanzishwaji wa elimu isiyolenga kupata faida, shule za msingi na sekondari zinazolenga misingi ya imani ya dini ambazo zitahudumia sekta ya elimU sambamba na utoaji mikopo kwa biashara zinazolenga kutoa upatikanaji wa vifaa vya elimu.
- Mikopo kwa Biashara Ndogo na Kati: Benki itatoa hadi Shilingi Bilioni 17.9 katika sekta ya biashara ndogo na kati. Benki itajikita katika biashara za sekta zote za uchumi kusaidia katika mitaji ya uendeshaji, manunuzi ya vifaa, ujenzi na ubadilishwaji wa sehemu za biashara ili kukuza biashara.
- Mikopo kwa Sekta zisizo Rasmi: Benki itatoa hadi Shilingi Bilioni 23.1 kusaidia biashara zisizo rasmi kutoka katika sekta zote za uchumi ambapo kipaumbele kitakua kwenye biashara zinazoendeshwa na vijana na wanawake.
No comments:
Post a Comment