Meneja wa Habari na Uhusiano Shirika la Nyumba la Taifa (NHC), Muungano Saguya akizungumza na Wanahabari. |
Baadhi ya Waandishi wa Habari kutoka vyombo mbalimbali wakifuatilia mkutano huo. |
Meneja wa Habari na Uhusiano NHC, Muungano Saguya akiwaelezea Waandishi wa Habari vipaumbele vya Shirika la Nyumba la Taifa. |
Taarifa hiyo imetolewa leo (tarehe 4/4/2022) na Meneja Habari na Uhusiano NHC Muungano Saguya alipokuwa anatoa taarifa ya vipaumbele vya Shirika katika mkutano uliofanyika katika jengo la Kambarage House.
Saguya amevitaja vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na kukamilisha miradi mikubwa iliyosimama ya Morocco Square na Kawe 711 jijini Dar es Salaam ambayo ilisimama tangu mwaka 2018 kutokana na upungufu wa fedha.
“Shirika limepewa kibali cha awali na Serikali ya Awamu ya Sita cha kukopa shilingi Bilioni 173.9 kumalizia miradi hiyo na tayari Hazina imeshaidhinisha mkopo wa Shilingi Bilioni 44.7 na tayari utekelezaji wa miradi hii unaendelea, ikiwamo mpango wa awali wa biashara (Business Plan) na kujenga nyumba za makazi ya watu wa kipato cha kati na maduka ya biashara (Shopping Malls) eneo la Kawe” amesema Saguya.
Amebianisha kuwa katika kusaidia suala la makazi hasa baada ya Serikali kuhamia Dodoma, Shirika litaendelea kujenga nyumba katika jiji la Dodoma, ujenzi utakaojumuisha nyumba za makazi za Medeli Awamu ya 3, Iyumbu Awamu ya 3 (Nyumba za ghorofa) na miradi mingine baada ya kupata ardhi ya uendelezaji eneo la Ndejengwa.
Kipaumbele kingine alichokitaja Saguya ni kukaribisha wawekezaji kutoka sekta binafsi ili kufanya uendelezaji wa majengo ya biashara na makazi katika maeneo na viwanja vya Shirika vilivyo wazi kwani vitasaidia kuongeza mapato ya Shirika, mapato ya Serikali, kukuza uchumi na ajira kwa Watanzania.
“Tutashirikiana na Taasisi na wadau mbalimbali ili kurahisisha utekelezaji wa miradi yetu hususan ushiriki wao wa kuweka miundombinu muhimu ya barabara, maji na umeme katika maeneo ya ujenzi” amesema Saguya
Ameongeza kusema kuwa Muundo mpya na Mpango Mkakati wa Shirika ili Muundo na Mpango huo uwe na wigo mpana wa kusaidia kuleta ufanisi na kubeba majukumu makubwa ya sekta ya nyumba, ilani ya Uchaguzi ya CCM na Mpango wa Taifa wa Maendeleo, Muundo na mpango Mkakati unapitiwa.
Kipaumbele kingine alichokitaja Meneja huyo wa Habari na Uhusiano NHC ni kuendelea kusimamia miliki ya nyumba za Shirika zipatazo 18,622 kwa kuzifanyia matengenezo ipasavyo kupitia Mpango wa Matengezo ya nyumba wa miaka mitano (2021/22-25/26). Katika kufanikisha hili Shirika limetenga shilingi Bilioni 50 kutekeleza mpango huo na kwamba huu ni ukarabati mkubwa utakaohusisha kubadilisha paa, vyoo na madirisha chakavu.
“Tunaangalia uwezekano wa kupunguza gharama za ujenzi kwa kuanzisha viwanda vitakavyosaidia kuzalisha vifaa vya ujenzi vinavyotumiwa na Shirika” amesisitiza Saguya
Kwa upande wa madeni ya kodi Saguya amebainisha kwamba madeni hayo yanayofikia shilingi bilioni 22 na madeni mbalimbali yatokanayo na uuzaji wa nyumba na viwanja yanayofikia shilingi bilioni 11.1 na msisitizo utakuwa kuhakikisha kila anayedaiwa analipa deni lake ili kuliwezesha Shirika kuendelea kuwahudumia Watanzania wote kwa kutumia rasilimali za umma.
Kati ya vipaumbele 11 kipaumbele kingine ni kuendelea kukamilisha ujenzi wa majengo 8 ya Wizara mbalimbali za Serikali katika mji wa Mtumba jijini Dodoma (awamu ya pili) na miradi hiyo itakapokamilika itagharimu jumla ya shilingi Bilioni 186.83. Msisitizo umewekwa katika kuikamilisha miradi hiyo kwa wakati kwa kuongeza usimamizi, udhibiti na ubora wa majengo hayo.
Akihitimisha mkutano huo Meneja huyo wa Habari na Uhusiano NHC amevihakikishia vyombo vya Habari vikiwa ni muhimili muhimu wa upashaji habari kwa wananchi na uelimishaji NHC itaendelea kushirikiana navyo katika kujenga taswira ya Shirika.
No comments:
Post a Comment