Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Bw. Lawrence Mafuru akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), jijini Dodoma. |
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Bw. Jacob Kibona, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi hiyo jijini Dodoma. |
Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), Bw. Godfred Mbanyi, akizungumza wakati wa uzinduzi wa Bodi ya Wakurugenzi ya Taasisi hiyo, jijini Dodoma. |
Waziri wa Fedha na Mipango ameiagiza Bodi ya Wakurugenzi ya Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), kuchukua hatua za kinidhamu kwa wanaokiuka maadili ya taaluma ya ununuzi na ugavi.
Maagizo hayo yalitolewa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Lawrence Mafuru kwa niaba ya Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), wakati akizindua Bodi ya Wakurugenzi ya PSPTB, jijini Dodoma.
Alisema kuwa Bodi hiyo ina jukumu la kusimamia maadili na mienendo ya Wataalam ikiwa ni pamoja na uhuishwaji na utengenezwaji wa mitaala inayozingatia umahili wa kitaaluma na mahitaji ya soko, uandaaji na usimamiaji wa miongozo mbalimbali inayohusu taaluma hiyo.
“Wadau wa ununuzi na ugavi wana matumaini makubwa kutoka kwenu kwani nyie ndio mtatoa dira chanya katika kutekeleza majukumuyao, mkasimamie tafiti mbalimbali zinazohusu taaluma na kutoa majibu kwa changamoto zinazojitokeza kwenye taaluma ili kuongeza tija katika utendaji,” alisema Bw. Mafuru.
Alisisitiza kuwa Bodi hiyo ina wajibu wa kusimamia utoaji wa mafunzo endelevu kwa wataalam na wadau wengine kwenye mnyororo wa ununuzi na ugavi, kufanya kazi za ushauri zinazohusu taaluma ya ununuzi na ugavi na kusimamia vyema matumizi ya tehama na mifumo ya kielectroniki katika shughuli za kusajili wataalam.
Aidha, Bw. Mafuru aliihakikishia Bodi hiyo kuwa Wizara ya Fedha na Mipango itaendeleza ushirikiano na Bodi ili iweze kutekeleza majukumu yake kwa hatua zinazolenga kuondoa kabisa uzembe na ukiukwaji wa maadili katika fani ya ununuzi na ugavi kwani pesa nyingi za Serikali, zinatumika kupitia taaluma hiyo.
Alitoa rai kwa waajiri nchini kutoa ushirikiano kwa Bodi hiyo, hususani usimamizi wa maadili kwa wataalam waliosajiliwa na Bodi kwa kutoa taarifa kwenye Bodi zinazohusiana na ukiukwaji wa maadili kwa wataalam, ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwani hakuna ufanisi bila maadili na weledi.
“Hakikisheni waajiri wote wanaajiri watumishi wenye sifa stahiki zinazotambuliwa na sheria ya PSPTB na kuzingatia mahitaji yaliyopo kwenye Waraka wa Maendeleo ya Utumishi Na. 3 wa mwaka 2015 wa kada zilizopo chini ya Wizara ya Fedha na Mipango”, alisisitiza Bw.Mafuru.
Bw. Mafuru alimpongeza Mwenyekiti na wajumbe wa Bodi Bw. Jacob Kibona, kwa kuteuliwa na kuaminiwa kuisimamia Bodi ya Wataalam wa Ununuzi na Ugavi kwa kipindi cha miaka mitatu kuanzia Novemba 2021 hadi Novemba 2024.
Pia alimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa PSPTB, Ndugu Godfred Mbanyi kwa kuteuliwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwa Mtendaji Mkuu wa PSPTB.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa PSPTB Bw. Jacob Kibona, aliahidi kuwa Bodi itasimamia na kuimarisha taaluma ya ununuzi na ugavi sambamba na kuongeza nguvu ya kupambana na vitendo vyote vinavyokinzana na maadili ya kitaaluma ikiwemo ubadhilifu wa mali, rushwa na ukiukwaji wa taratibu za ununuzi na gavi.
Alisema kupitia Bodi hiyo itasimamia fedha zitakazotolewa na Serikali kwa ajili ya kukwamua shughuli zilizokwama kutokana na ukosefu wa fedha uliochangiwa na kutokuwa na bodi kwa muda mrefu na kuahidi kuisaidia Serikali kutekeleza malengo yake kwa weledi na kutoa huduma bora kwa Watanzania.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Godfred Mbanyi alisema kuwa Menejimenti ya taasisi hiyo itatoa ushirikiano kwa Bodi hiyo na kuahidi kuwa watafanya kazi kwa weledi na kuwa itapokea ushauri na maelekezo ili kuongeza ufanisi.
No comments:
Post a Comment