Moshi - Wizara ya Kilimo imepongeza juhudi mbalimbali zinazofanywa na benki ya Biashara ya Taifa (NBC) katika uwezeshaji wa wakulima kupitia mikopo na bidhaa mbalimbali ikieleza kuwa hatua hizo zitawakomboa wakulima wengi dhidi ya umasikini hapa nchini.
Hayo yalisemwa wakati wa uhitimishaji wa maonesho ya kwanza ya Kahawa yaliyofanyika Mjini Moshi na kuhusisha wadau mbalimbali wa sekta ya kilimo na fedha ili kusherekea siku ya kahawa Duniani (International Coffee Day).
Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gelard Kusaya alisema taasisi za fedha zina mchango mkubwa katika kuendeleza sekta ya kilimo kupitia uwezeshaji kwa wakulima na wafanyabiashara kwa njia ya mikopo yenye riba nafuu.
Kusaya alisema Wizara imefurahishwa sana na huduma ya ‘NBC Shambani’ na kwamba itakuwa na msaada mkubwa kwa wakulima kufanya kilimo-biashara ili waweze kuona tija zaidi.
NBC Shambani ni huduma maalumu kwa wakulima inayowawezesha kufungua akaunti za vikundi (Amcos) au akaunti ya mkulima mmoja mmoja bila gharama za uendeshaji.
“Mkulima anayetaka kujikita katika kilimo biashara ni lazima awezeshwe katika suala la fedha, mikopo mnayoitoa tunaamini inakuwa na faida kubwa kwa mkulima na mkulima ataweza kuzalisha zaidi,” alisema Kusaya.
Meneja wa NBC Tawi la Moshi, Lazaro Mollel alisema maonesho hayo yamekuwa na faida kubwa katika kufahamu mahitaji ya wakulima hasa wakulima wa zao la kahawai li kuongeza ubunifu wa bidhaa.
Alisema benki hiyo imeleta huduma maalumu kwaajili ya wakulima iitwayo NBC Shambani ambayo inawawezesha wakulima kufungua akaunti za vikundi (Amcos) pamoja na akaunti ya mkulima mmoja mmoja bila gharama za uendeshaji.
“Huduma ya NBC Shambani inawalenga wadau wote wa kilimo wakiwamo wasambazaji, wakulima, wauzaji wa pembejeo na pia inatoa fursa kwa wakulima wanaofanya kazi kwenye vikundi vya ushirika (Amcos) kufungua akaunti ya kikundi kufungua akaunti ya pamoja na ya mtu mmoja mmoja ambazo uendeshaji wake ni bure,” alisema.
Katika maonesho hayo, NBC imeweza kukabidhiwa tuzo ya mdhamini mkuu wa maonesho hayo ambayo ni ya kwanza kufanyika nchini Tanzania.
No comments:
Post a Comment