Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), imeendelea kuongeza na kuimarisha huduma zake za kibenki kwa njia za kidigitali ili kuwawezesha wafanyabiashara na wateja wengine kufanya miamala mingi ya kibenki mahali walipo imeelezwa jijini Mwanza hivi karibuni.
Akizungumza na wateja wa benki hiyo jijini Mwanza ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya mwezi wa huduma kwa wateja wa NBC, Meneja Huduma katika Kitengo cha Wateja wa Makampuni wa benki hiyo, Mary Opiyo alisema benki hiyo imerahisisha huduma zake nyingi kwenda kidigitali ili kuwafanya wateja wao kupata muda zaidi wa kufanya biashara zao kuliko kupata huduma hizo katika matawi yao.
“Sasa mteja wetu anaweza kufanya malipo akiwa ofisini kwake kwa njia ya mtandao wa intaneti akatuma pesa kwa wateja wake ambao pengine ingebidi awapelekee au waje pale, NBC itaendelea kuboresha na pia imo mbioni kuongeza huduma nyingine bora zaidi hususan malipo kwa njia ya mtandao ili kutengeneza fursa mbalimbali za kibiashara kwa wateja wetu”, aliongeza meneja huyo.
Akizungumza katika hafla hiyo Mkuu wa Kitengo cha Fedha Taslimu na Miamala kwa wateja Wakubwa na wa Kati wa beni hiyo, Jimmy Myalize alisema mkutano huo una lengo la kuwashukuru wateja wao kwa biashara wanayowapa na kuweza kuwaamini wakawa benki waitumiayo kwa ajili ya mambo yao ya kifedha.
Alisema pia katika kukutana kwao wameweza kuwafahamisha bidhaa zao mpya, benki ipo wapi na maendeleo ya benki kwa ujumla na pia kupata mrejesho kutoka kwao juu ya huduma za NBC na kama kuna maeneo wangependa yaboreshwe ili kuweza kuwahudumia vizuri zaidi.
“Pia tunawakutanisha wateja wetu ili kuweza kuongea biashara na kutengeneza fursa za kibiashara kati yao jambo litakalosaidia wateja wetu kukua kibiashara kwani mteja anapokua na sisi kama benki tunakua”
Benki ya NBC huadhimisha Mwezi wa Huduma kwa Wateja mwezi wa Oktoba kila mwaka kwa kufanya shughuli mbalimbali za kijamii kama vile kutoa misaada mbalimbali na kutoa elimu ya kifedha na ujasiriamali kwa makundi tofauti, kutembelea wateja wao mahali walipo na kufanya mikutano na wateja hao.
No comments:
Post a Comment