Kampeni ya DCB Lamba Kwanza iliyozinduliwa Mei 29 mwaka huu na kudumu kwa muda wa miezi mitatu huku ikiwa na lengo la kukusanya amana za kiasi cha shilingi Bilioni 15, iliwawezesha wateja wa benki hiyo kuwekeza na kupata riba ya hadi asilimia 14 ya amana wanayowekeza ambapo mteja alianza kupokea riba yake ya mwezi papo hapo.
Akizungumza jijini Dar es Salaam leo, Mkurugenzi wa Biashara, James Ngaluko alisema ‘tunatoa shukurani zetu za dhati kwa wateja wetu kwa kuweza kuipokea bidhaa hii na kuweza kunufaika nayo kwani wamenufaika sana,kila mwezi umekua mwezi wa faida. Mteja anafurahia riba yake inayolipwa mwanzo wa mwezi kila mwezi, malipo ya riba ni rafiki mteja anaweza kuwekeza kuanzia miezi mitatu (3) mpaka miaka miwili (2). Ni jambo la fahari kuona Benki ya kitanzania inatoa fursa kwa Watanzania na kuwawezesha kuboresha maisha na uchumi’.
Alisema DCB Lamba Kwanza imepokewa kwa mikono miwili na wateja wetu na kufanikiwa kuvuka malengo kwa kukusanya amana ya zaidi ya shs bilioni 18.5 ambapo awali Benki ilikusudia kuuza kiasi cha shs bilioni 15.
“Kwa namna ya kipekee ningependa kwanza kabisa kuwashukuru wateja wetu kwa kuendelea kutuunga mkono kwa kila bidhaa tunayoiingiza sokoni na kutuwezesha kuvuka malengo hii inaonyesha ni jinsi gani DCB inavyo aminika kwenye soko.
“Benki ya DCB tupo imara na tumejidhatiti katika kubuni na kuingiza bidhaa zitakazokidhi kiu ya mahitaji ya huduma za kifedha kwa wateja wetu,”
Kwa sasa benki imeendelea kufanya maboresho katika baadhi ya huduma zake ikiwa ni pamoja na kupunguza riba na kuongeza muda wa marejesho hadi miaka 15 kwa mikopo ya ujenzi na ununuaji wa nyumba za makazi kwa wateja wetu wote hususan wafanyabiashara na waajiriwa. Hii imefanya benki yetu kuongoza kutoa mikopo mingi zaidi ya ujenzi wa nyumba na ununuaji wa nyumba Tanzania. (kwa takwimu za Tanzania Mortage Refinance-taasisi iliyo chini ya benki kuu). Tunatoa wito kwa wajasiriamali wote na wafanyakazi wenye lengo la kununua au kujenga nyumba kuwahi fursa hii.
Vilevile benki inatoa huduma za kidigitali kupitia DCB DIGITAL inayomuwezesha mteja kufungua akaunti kupitia simu yake ya mkononi, DCB sokoni inayomsaidia mkulima,wenye viwanda vya kilimo pamoja na wafanya biashara wa kilimo kwenye mnyororo wa thamani. Vile vile tuna akaunti na huduma nyingi zinazotoa fursa kwa watanzania kuweka akiba lakini pia kupata faida ya fedha zao.
Kampeni hii ni muendelezo wa mafanikio yanayofanywa na Benki ya DCB kwani Benki hii imeendelea kupata faida, na kufikia kipindi cha nusu ya kwanza ya mwaka huu imeweza kupata faida ya sh. bilioni 1.2 ikiwakilisha ongezeko la asilimia 118% kutoka faida ya kipindi kama hicho kwa mwaka 2018. Utendaji wa benki umeimarika,huku ufanisi katika nyanja zote muhimu ukiongezeka kwa kiwango cha kuridhisha ukichagizwa na kukua kwa biashara na ukusanyaji wa mikopo chechefu. Vile vile benki imeendelea kuvunja rekodi katika malengo kama ilivyotokea hivi karibuni ilipotangaza kuvuka malengo katika zoezi la uuzwaji wa hisa zake kwa kuuza hisa milioni 36.6, ikiwa ni zaidi ya malengo ya awali ya kuuza hisa milioni 33.9 na kufanikiwa kukusanya sh. Bilioni 9.7 sawa na asilimia 108.99 ya matarajio ya awali ya kukusanya shilingi Bilioni 8.9.
“Tunafurahi kuwaambia kuwa lengo letu limetimia, kampeni imeisha lakini bidhaa ya DCB Lamba Kwanza itaendelea, hivyo wale wateja ambao bado hawajafungua akaunti hii bado ipo na wanaweza kuwahi katika matawi yetu kuanza kuwekeza na ‘KULAMBA’ riba.
Ikumbukwe Kuwa
- Benki ya Biashara ya DCB ilianzishwa mwaka 2002 ikiwa kama Benki ya Jumuiya ya Wananchi “community bank” na Manispaa za Jiji la Dar es Salaam kufuatia kilio cha wakazi wengi wa Jiji kutokuwa na njia rahisi ya kupata mitaji midogo midogo ya biashara.
- Benki ya DCB imekuwa ni benki ya kwanza kuorodheshwa kwenye Soko la Hisa mwaka 2008, na imeweza kukuza mtandao wake wa matawi kufikia matawi nane likiwepo tawi la Dodoma, na inatarajia kuongeza matawi mengine mikoani katika miaka ya mbeleni.
- Uboreshaji huduma na mahusiano ya wateja umekuwa ndio kigezo kikuu katika kuongeza amana nafuu na za muda mrefu hasa kutoka kwa wanahisa waanzilishi na mashirika mbalimbali yaliyoendelea kuwekeza na benki ya DCB.
- Idadi ya wateja imeongezeka kutoka 144,475 mwaka 2017 kufikia 195,611 Agasti 2019 na hivyo kuchangia ongezeko kubwa la miamala ya kibenki.
- Benki ya DCB imefungua mtandao wa mawakala na huduma za kijiditali hadi kufikia 1000 nchi nzima.
No comments:
Post a Comment