Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Tuesday, 21 August 2018

TANZANIA NA UGANDA ZINATARAJIWA KUSAINI MKATABA WA MAKUBALIANO (MOU) KUHUSU UENDELEZAJI WA BOMBA LA KUSAFIRISHA GESI

Tanzania na Uganda zinatarajiwa kusaini Mkataba wa Makubaliano (MoU) kuhusu uendelezaji wa Bomba la kusafirisha gesi asilia litakaloanzia hapa nchini na kuishia Uganda na makubaliano ya kushirikiana katika masuala ya elimu na mafunzo (Education and Training).

Uwekaji saini wa MoU hizo utafanyika katika Mkutano wa Pili wa Tume ya Kudumu ya Pamoja ya Ushirikiano (JPC) Kati ya Tanzania na Uganda utakaofanyika Kampala kuanzia tarehe 21 hadi 23 Agosti 2018.

Ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo utaongozwa na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb).
Mkutano huo wa JPC unafanyika pamoja na mambo mengine ni utekelezaji wa azma ya Viongozi wa nchi hizo, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli na Mhe. Yoweri Kaguta Museveni ya kuimarisha ushirikiano wa kibiashara hususan, katika ujenzi wa miundombinu itakayoboresha biashara kati ya Tanzania na Uganda.

Maeneo mbalimbali ya ushirikiano yatajadiliwa katika mkutano huo yakiwemo ujenzi wa miundombinu ya barabara, usafiri wa majini, reli, anga, nishati ya Umeme na vituo vya kutoa huduma kwa pamoja mipakani ambayo yana mchango mkubwa katika ukuaji wa uchumi na biashara ya nchi hizo.
Maeneo mengine yatakayojadiliwa ni pamoja na ushirikiano katika Kilimo, utalii, biashara za mipakani na afya. Aidha, Mkutano huo utatoa fursa ya kuimarisha ushirikiano katika sekta za mazingira, maji na michezo.

Mkutano wa kwanza wa JPC ulifanyika Arusha mwezi Aprili 2017 ambapo pande mbili zilikubaliana kushirikiana katika maeneo mbalimbali ambayo mkutano wa Kampala utapata fursa ya kutathmini utekelezaji wake na kuibua maeneo mapya ya ushirikiano.

Imetolewa na:
Kitengo cha Mawasiliano ya Serikali,
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki,
Dar es Salaam.
20 Agosti 2018

No comments:

Post a Comment