Serikali yafikia muafaka katika mgogoro wake na wafanyabiashara juu ya matumizi ya mashine za kieletroniniki EFD’s. Hayo ameyasema jana Waziri wa Fedha Mhe. Saada Mkuya alipokuwa akitoa taarifa hiyo kwa vyombo vya habari juu ya Serikali kufikia muafaka wa makubaliano yaliyofanyika kwa ushirikiano wa Kamati kuu ya Taifa iliyoshirikisha wajumbe kutoka Wizara ya Viwanda na Biashara pamoja na Viongozi wa Jumuiya ya wafanyabiashara katika ngazi ya Taifa.
“Matumizi ya mashine za EFD yalipoanza yalileta changamoto kwa wafanyabiashara, hivyo niliunda kamati ya kitaifa pamoja na kamati katika ngazi za Mikoa na Wilaya pamoja na wenyeviti wakuu wa mikoa kutafuta suluhu la suala hili” alisema Mhe. Mkuya.
Waziri Mkuya aliendelea kusema Kamati imetoa mapendekezo mbalimbali kwa Serikali ikiwemo ya muda mfupi ambayo wameshaanza kuyafanyia kazi na mengine ni yakisera ambayo yatahitaji muda mrefu yatafuata utaratibu unaopaswa katika utekelezaji wake, kwa ufuatiliaji na ushirikiano wa karibu, kupitia kamati ya Kitaifa itakayodumu kwa kipindi cha miaka miwili.
Naye Mwenyekiti wa Jumuiya ya Wafanyabiashara nchini Bw. Johnson Minja aliipongeza serikali kwa kukubali kukaa meza moja na wafanyabiashara katika kutatua mgogoro huo uliyokuwepo katika matumizi ya mashine za EFD na kukukubali kupokea changamoto za wafanyabiashara na kuahidi kuzifanyia kazi. “Serikali imekubali kupitia mfumo wa utozwaji kodi kuanzia ngazi ya bandarini na kuongeza uwazi ili kuleta uelewa kwa wafanyabiashara na kuepuka kutozwa kodi kubwa kutoka na kukosa uelewa wa gharama za ulipaji kodi”, alisema Bw.Minja.
Aidha Mwenyekiti wa Jumuiya hiyo ya wafanyabiashara aliendelea kusema ni wajibu wa kila mmoja kulipa kodi na hii ni kwa maendeleo ya nchi na pia ni kosa kwa mfanyabiashara yoyote kuendesha biashara yake bila kuwa na namba ya utambulisho wa mlipakodi (Tin Number), tunataka namba ya walipakodi iendelee kuongezeka na kuondoa kabisa wafanyabiashara wasio lipa kodi.
Mbali na hayo nae Kamishana Mkuu wa Mamlaka ya Mapato (TRA), Rished Bade aliipongeza kamati kwa kuweza kufika mwafaka na kuweza kuzitambua changamoto mbalimbali zilizokuwa zikiwasumbua wafanyabiashara na ameahidi, kuwa ofisi yake itaendelea kuwawajibisha watu wote wanao kiuka taratibu za ulipaji kodi.
No comments:
Post a Comment