Ndege ya abiria HM 777 ya Air Seychelles baada ya safari yake ya kwanza ya uzinduzi kwa kutua Kiwanja cha Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
Katika hotuba yake, Naibu
Waziri wa Uchukuzi, Mhandisi Dk. Tizeba alisema ujio wa Air Seychelles
umefungua ukurasa mpya wa safari kwa wananchi wa nchi za zisizopakana na bahari
ya Hindi (landlocked) na fursa zaidi za utalii kwani sasa watakuwa na uhakika
wa kuunganisha safari zao kwenda kokote duniani kwa ndege hiyo.
Shirika la Ndege la Taifa la
Shelisheli, Air Seychelles limeanza kufanya safari zake kati ya mji mkuu wa
nchi hiyo, Mahe na Dar es Salaam ambapo jana, Desemba 2, 2014, ndege yake ya
abiria HM 777 ilifanya safari yake ya kwanza ya uzinduzi kwa kutua Kiwanja cha
Ndege cha Kimataifa cha Julius Nyerere (JNIA), Dar es Salaam.
Ujio wa shirika hilo la ndege
unafanya mashirika ya ndege yaliyoanzisha safari zake kuja Dar es Salaam kwa
siku za hivi karibuni kufikia matatu, Air Seychelles, Flydubai ya Umoja wa
Falme za Kiarabu (UAE) na Rwandair ya Rwanda. Shirika lingine la ndege, Etihad
la Abudhabi (UAE) linatarajiwa kuanza safari zake mwaka 2015.
Uzinduzi wa safari za ndege
ya Air Seychelles ulifanywa na Naibu Waziri wa Uchukuzi, Mhandisi Dk. Charles
Tizeba na kuhudhuriwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Mahmoud Mgimwa,
wabunge na viongozi kadhaa wa Serikali na wadau wa masuala ya sekta ya usafiri
wa anga na maliasili na utalii nchini.
Naibu Waziri Tizeba alisema
ujio wa ndege hiyo utakuza sekta ya
utalii kati ya nchi hizo na kunufaisha wananchi wake na kwa kujua umuhimu wa
sekta ya usafiri wa anga kwa nchi hizo, alizitaka Tanzania na Shelisheli
kutekeleza mikakati ya kitaifa, kikanda na dunia ya usafiri wa anga kuleta
maendeleo ya sekta hiyo nchi mwao.
Alitoa rai kwa
wafanyabiashara ya sekta ya utalii kutumia fursa hii kukukuza biashara kati ya
nchi hizi kwani Tanzania ina hazina ya vivutio vya utalii ikiwemo maeneo ya
kihistoria Zanzibar na Bagamoyo, mlima mrefu kuliko yote Afrika, Kilimanjaro na
moja ya maajabu saba ya dunia, Kreta ya Ngorongoro mkoani Manyara.
Naibu Waziri Dk. Tizeba
alisema, Serikali itafanya kila iwezalo kuhakikisha safari za ndege kati ya Tanzania na
Shelisheli zinadumu na kwamba Serikali za nchi hizo zitahakikisha mkataba wa
ushirikiano wa sekta ya usafiri unasainiwa haraka iwezekanavyo na mamlaka husika
za usafiri wa anga nchini kwa mujibu wa masharti ya ICAO.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya
Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA), Mhandisi Suleiman S. Suleiman alisema ujio wa
ndege hiyo ni mafanikio makubwa kwani unaongeza idadi ya ndege zinazotua JNIA
ambapo juzi tu ilikuja Flydubai na wanatarajia mwakani, 2015 Emirates itaongeza
safari kutoka 12 hadi 14 kwa wiki.
“Sisi (TAA) hatulali. Tunafanya kazi kwa
ushirikiano na mshauri mwelekezi wa biashara ya ndege ambaye kazi yake ni kushawishi
mashirika zaidi ya ndege kuja Tanzania. Mpaka sasa kuna ndege 18 zinazokuja na
Januari mwakani, 2015, ndege ya Etihad
inatarajiwa kuanza safari zake pia”,
Mkurugenzi Mkuu huyo wa TAA alisema.
Akizungumza katika hafla
hiyo, Meneja Mkuu wa Mahusiano wa Air Seychelles, Alan Renaud alisema safari za
ndege hiyo kati ya Mahe – Dar es Salaam zitakuza utalii na biashara kati ya
Tanzania na Shelisheli na kuwa kiungo cha safari za mashirika mengine ya ndege
duniani ambako abiria wataunganisha safari zao.
“Dar es Salaam ni njia
nyingine muhimu ya safari za ndege yetu tulizoongeza na inaonesha hatua mpya ya
kukua kwa shirika letu. Ikiwa na watu zaidi ya milioni nne na ya pili kwa
ukubwa ukanda wa bahari ya Hindi, kiungo kikubwa kwenda mbuga na hifadhi maarufu
za wanyama na vivutio vingine vya utalii kama Mlima Kilimanjaro wenye theluji,
Dar es Salaam ni chachu kubwa ya utalii na biashara,” alisema Renaud katika hotuba yake.
Alisema, ujio wa ndege hiyo
ni matokeo ya ushirikiano mkubwa kati yao na Shirika kubwa la ndege la Etihad
Airways lenye hisa asimia 40 lililowawezesha kupata ndege ya kwanza aina ya
Airbus A320 na kuifanya Mahe kama kitovu
cha abiria kutoka Afrika Mashariki kwenda nchi za Mashariki ya Kati, Asia na za
Bara Hindi.
Air Seychelles ilianzishwa
mwaka 1978 na ilianza safari za masafa marefu mwaka 1983. Kwa sasa shirika hilo
la ndege linafanya safari kwenda Abudhabi, Antananarivo (Madagascar), Hong
Kong, Johannesburg (Afrika Kusini),
Mauritius, Mumbai (India) na Paris (Ufaransa) na safari 200 za ndani mwake kwa
wiki. Air Seychellles itafanya safari zake kati ya Mahe na Dar es Salaam (JNIA)
mara mbili kwa wiki, Jumanne na Jumapili.
Imetolewa na Kitengo cha Sheria na Uhusiano
Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania (TAA)
Dar es Salaam
Desemba
2, 2014
No comments:
Post a Comment