Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Biashara kutoka Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Bw. Abdulla Makame Akiwaeleza waandishi wa Habari (hawapo pichani) Kuhusu Mkutano wa 29 wa Baraza la Mawaziri wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utakaofanyika Septemba 20 mwaka huu Jijini Arusha. Kulia ni Kaimu Mkuu wa Kitengo cha Mawasiliano wa Wizara hiyo Anthony Ishengoma.
Akieleza zaidi Makame amesema mkutano huo utapokea na kuidhinisha aina mpya ya hati ya kusafiria ya kielektroniki, zikiwemo sampuli za hati za kusafiria za kibalozi, za Maofisa na za kawaida za kusafiria.
Mkutano wa 29 wa Baraza la Mawaziri wa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki utapokea na kuidhinisha aina mpya ya hati za kusafiria za kielektroniki, zikiwemo sampuli za hati za kusafiria za kibalozi, za Maofisa na za kawaida.
Hayo yamesemwa leo Jijini Dar es salaam na Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Biashara, Uwekezaji na shughuli za uzalishaji wa Wizara ya Ushirikiano wa Afrika Mashariki Dk. Abdulla Makame wakati wa mkutano na waandishi wa habari.
Mkutano huo utakaofanyika Septemba 20 mwaka huu Jijini Arusha pia unatarajia kupokea na kuidhinisha taarifa mbalimbali sambamba na kutolea maamuzi masuala yanayohusu mtangamano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Aidha Mkutano huo utajadili mapendekezo na hadidu za rejea za uanzishwaji wa Dira ya maendeleo ya Afrika Mashariki ya mwaka 2050.
Pia mkutano huo utajadili mapendekezo ya mpango mwelekeo na shughuli mbalimbali zinazolenga kuandaa katiba ya shirikisho la Afrika Mashariki na kujadili mapendekezo ya baraza la ulinzi na usalama linalopendekezwa.
Baraza la Mawaziri katika Jumuiya ya Afrika mashariki ni chombo cha pili katika ngazi za kufanya maamuzi ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki baada ya Mkutano wa Kilele.
Frank Mvungi - Maelezo
No comments:
Post a Comment