Foreign Exchange Rates

CRDB Bank Advert_070325

Thursday, 22 January 2026

FORLAND YASAINI MAKUBALIANO NA RUVUMA, LINDI KUIMARISHA UHIFADHI WA MISITU

Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa kushirikiana na Serikali ya Finland, imesaini hati ya makubaliano ya kikanda (MoU) chini ya Mradi wa Maendeleo ya Matumizi ya Ardhi na Minyororo ya Thamani ya Misitu Tanzania (FORLAND), yenye lengo la kuimarisha usimamizi, uratibu na uhifadhi endelevu wa mandhari ya misitu katika mikoa ya Ruvuma na Lindi.

Hatua hii inakuja muda mfupi baada ya makubaliano kama hayo kusainiwa na mikoa ya Njombe na Iringa, ambako mradi wa FORLAND tayari unaendesha shughuli za usimamizi wa misitu na uimarishaji wa minyororo ya thamani ya mazao ya misitu.

Kupitia makubaliano haya, mradi wa FORLAND unatarajiwa kutekelezwa katika maeneo mbalimbali muhimu, yakiwemo uzalishaji wa mbegu bora za miti, uimarishaji wa mikakati ya kudhibiti na kupambana na majanga ya moto wa misitu, pamoja na utoaji wa elimu na mafunzo kwa wakulima wa miti ili kuongeza tija na uendelevu wa shughuli zao.

Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Mratibu wa Mradi wa FORLAND kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii, Bi. Emma Nzunda, alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa karibu kati ya serikali kuu, serikali za mikoa, wadau wa misitu na jamii katika kuhakikisha utekelezaji wenye mafanikio wa mradi huo.

Kwa upande wake, Mshauri Mkuu wa Kiufundi wa Mradi wa FORLAND kutoka Finland, Bw. Michael Howkes, alisema mradi huo unalenga kuimarisha mnyororo mzima wa thamani wa sekta ya misitu kuanzia kwa wakulima wa miti, wasafirishaji, viwanda vya uchakataji, hadi kujenga uwezo wa wadau mbalimbali wanaohusika katika sekta hiyo.

Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bw. Joseph Martin, pamoja na Katibu Tawala Msaidizi (Huduma za Kiuchumi na Uzalishaji) wa Mkoa wa Lindi, Bw. Mwinjuma Mkungu, kwa pamoja walikiri kuwa majanga ya moto wa misitu yamekuwa changamoto kubwa inayorejesha nyuma jitihada za wakulima na ukuaji wa uchumi wa maeneo husika. Walieleza kuwa kusainiwa kwa makubaliano hayo kutasaidia kwa kiasi kikubwa kukabiliana na changamoto hizo kwa njia ya pamoja na iliyoratibiwa.

Kwa upande wao, wadau wa misitu nchini wameeleza kuwa mradi wa FORLAND utaondoa au kupunguza changamoto mbalimbali zinazowakabili wakulima wa miti, hususan matumizi ya mbegu feki, upungufu wa elimu ya kitaalamu, pamoja na athari za majanga ya moto wa misitu.

Kwa ujumla, kusainiwa kwa makubaliano haya kunaakisi dhamira ya pamoja ya Serikali, washirika wa maendeleo na wadau wa misitu katika kukuza usimamizi endelevu wa mandhari ya misitu, kuboresha maisha ya wananchi, na kuchangia kikamilifu katika utekelezaji wa malengo ya kitaifa na kimataifa ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi pamoja na uhifadhi wa bayoanuai.

Hafla ya utiaji saini wa makubaliano hayo ilihudhuriwa pia na wadau mbalimbali wa sekta ya misitu na mazingira kutoka mikoa ya Ruvuma na Lindi.

No comments:

Post a Comment