Shughuli zinalenga kuimarisha usafi wa mazingira na kukuza Uchumi wa Buluu katika ukanda wa Ziwa Victoria
Mwanza, Tanzania – 24 Januari 2026
Benki ya Equity Tanzania, kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wa mazingira, imefanikisha utekelezaji wa shughuli za kijamii na kimazingira katika ukanda wa Ziwa Victoria jijini Mwanza, ikiwa ni sehemu ya jitihada zake za kuunga mkono usimamizi endelevu wa mazingira na kukuza Uchumi wa Buluu.
Shughuli hizo zilihusisha makabidhiano rasmi ya vifaa vipya vya kuhifadhi taka ngumu katika Soko la Samaki la Mwaloni, pamoja na zoezi la usafi wa ufukwe wa Ziwa Victoria. Makabidhiano ya vifaa hivyo yaliongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Ilemela, Mhe. Amir Mohammed Mkalipa, akishirikiana na viongozi wengine kutoka Wilaya za Ilemela na Nyamagana pamoja na uongozi wa Soko la Samaki Mwaloni.
Katika zoezi la usafi wa ufukwe wa ziwa, Benki ya Equity Tanzania ilishirikiana na taasisi ya HUDEFO, vijana takribani 70 wa kujitolea kutoka vyuo vya SAUT na TIA, wadau wengine wa mazingira, pamoja na wafanyakazi wa Benki ya Equity. Ushiriki huu wa pamoja unaakisi dhamira ya benki katika kuhamasisha ushirikiano wa jamii katika kulinda mazingira na rasilimali za maji.
Makabidhiano ya vifaa vya kuhifadhi taka ngumu yanalenga kuboresha hali ya usafi na usalama wa kiafya katika Soko la Samaki Mwaloni, kupunguza uchafuzi wa mazingira, na kuchangia ustawi wa kiuchumi na kiafya kwa wafanyabiashara na wadau wote wa soko hilo. Aidha, zoezi la usafi wa ufukwe wa Ziwa Victoria lililenga kuondoa taka ngumu na plastiki, kuzuia uchafuzi wa maji ya ziwa, pamoja na kutoa elimu na mafunzo kuhusu usimamizi endelevu wa taka na fursa zinazotokana na Uchumi wa Buluu.
Akizungumza wakati wa tukio hilo, Bi. Hellen Dalali, Mkuu wa Kitengo cha Uendelevu wa Benki ya Equity Tanzania, alisema benki inaamini kwa dhati katika uwezeshaji wa jamii na ulinzi wa mazingira. Alisisitiza kuwa shughuli hizo hazikulenga tu usafi wa mazingira na makabidhiano ya vifaa, bali pia zilikuwa jukwaa la kujenga uelewa kuhusu umuhimu wa kutunza vyanzo vya maji na kukuza Uchumi wa Buluu kwa kushirikisha wajasiriamali na vikundi vya kijamii.
Aliongeza kuwa juhudi hizo ni sehemu ya mkakati mpana wa Benki ya Equity Tanzania wa kuinua maisha ya Watanzania kupitia miradi endelevu yenye athari chanya kwa jamii, uchumi na mazingira.
Benki ya Equity Tanzania inaendelea kutoa mikopo nafuu na dhamana maalum kwa wajasiriamali, hususan katika sekta za Uchumi wa Buluu, nishati safi, na usimamizi endelevu wa taka. Vilevile, benki hutoa mafunzo ya ujasiriamali na elimu ya kifedha bila malipo, kwa lengo la kuwajengea wadau uwezo wa kuendesha biashara zao kwa ufanisi na weledi zaidi.
Kwa maelezo zaidi:
📧 infotz@equitybank.co.tz
📞 0768 985 500


.jpeg)


.jpeg)
No comments:
Post a Comment