Foreign Exchange Rates

CRDB Bank Advert_070325

Selcom Pesa Advert_110225

Selcom Pesa Advert_110225

Standard Chartered Advert_300125

Standard Chartered Advert_300125

Wednesday, 17 December 2025

NMB YAKABIDHI VIFAA TIBA VYENYE THAMANI YA SH. MILIONI 15 KITUO CHA AFYA MAKOLE, DODOMA

Dodoma, Tanzania — Benki ya NMB imeendelea kuonesha dhamira yake katika kusaidia maendeleo ya jamii kwa kukabidhi vifaa tiba na mahitaji mbalimbali vyenye thamani ya shilingi milioni 15 kwa Kituo cha Afya Makole kilichopo jijini Dodoma.

Msaada huo ni sehemu ya mkakati wa Benki ya NMB wa kuchangia uimarishaji wa sekta ya afya nchini, hususan katika kuboresha utoaji wa huduma za afya kwa wananchi katika ngazi ya jamii. Kupitia mchango huu, kituo hicho kinatarajiwa kuongeza ufanisi katika kuhudumia wakazi wa Makole pamoja na maeneo jirani yanayopata huduma katika kituo hicho.

Vifaa tiba hivyo vilipokelewa rasmi na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Makole, Dkt. Revocatus Kitena, ambaye aliishukuru Benki ya NMB kwa msaada huo unaokuja wakati muafaka, akieleza kuwa utasaidia kwa kiasi kikubwa kuboresha mazingira ya kazi na huduma kwa wagonjwa.

Hafla ya makabidhiano ilihudhuriwa na uongozi wa Benki ya NMB ukiongozwa na Meneja wa NMB Kanda ya Kati, Bi. Janeth Shango, akiambatana na baadhi ya Mameneja wa Matawi ya Benki hiyo kutoka Kanda ya Kati. Bi. Shango alisisitiza kuwa Benki ya NMB itaendelea kushiriki katika miradi yenye mchango chanya kwa jamii, hususan katika sekta nyeti kama afya, elimu na maendeleo ya kijamii.

Hatua hii inaonesha dhamira ya Benki ya NMB katika kutekeleza wajibu wake wa kijamii (CSR) na kuunga mkono jitihada za Serikali katika kuboresha huduma za afya kwa Watanzania.



No comments:

Post a Comment