Dar es Salaam, Novemba 20, 2025 — Benki ya Stanbic Tanzania imekabidhi msaada wa vifaa tiba vyenye thamani ya zaidi ya Shilingi milioni 25 kwa Kituo cha Afya Goba, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuendelea kuboresha huduma za afya kwa jamii.
Vifaa vilivyotolewa ni pamoja na Unit Suction Machine (1), Patient Monitor (1), Oxygen Concentrator (1), Roll Cloth Cotton (3), Manual Vacuum Aspirators (2), pamoja na vifaa vya TEHAMA ambavyo ni Vishikwambi (3), Televisheni (1), Kompyuta za Mezani (2) na Armored Cable (1).
Makabidhiano hayo yalifanywa na Meneja wa Kanda wa Benki ya Stanbic, Bi. Edditrice Marco, kwa niaba ya benki, na kupokelewa na Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Goba, Dkt. Elias Ndahani. Hafla hiyo ilishuhudiwa pia na mgeni rasmi, Afisa Tarafa ya Kibamba, Bi. Beatrice Mbawala, kwa niaba ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Mhe. Albert Msando.
“Ni Sehemu ya Miaka 30 ya Kukua Pamoja” — Stanbic
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Bi. Edditrice Marco alisema msaada huo umetolewa kupitia mpango wa uwajibikaji kwa jamii (CSR) wa Stanbic, ukiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka 30 tangu benki ilipoanza kutoa huduma nchini.
“Tunatambua umuhimu wa sekta ya afya katika ustawi wa jamii. Kupitia msaada huu tunalenga kuboresha huduma kwa wagonjwa na kusaidia watoa huduma kuongeza ufanisi. Hii ni moja ya njia tunazosherehekea miaka 30 ya kukua pamoja na Watanzania,” alisema Bi. Marco.
Kituo Cha Afya Goba Chafunguka: “Msaada Umefika Wakati Muafaka”
Mganga Mfawidhi, Dkt. Elias Ndahani, aliishukuru benki kwa mchango huo muhimu, akibainisha kuwa kituo bado ni kipya na kinahitaji vifaa vya kuboresha huduma.
“Vifaa hivi vitasaidia sana hususan upande wa upasuaji na dharura. Mashine za kusaidia kupumua zitasaidia kuokoa maisha ya mama na mtoto wakati wa kujifungua. Msaada huu umefika wakati muafaka,”alisema Dkt. Ndahani.
Uongozi wa Serikali Wapongeza Stanbic Kwa Kujitolea
Katika hotuba yake, Afisa Tarafa ya Kibamba, Bi. Beatrice Mbawala, aliipongeza Stanbic kwa kuendelea kuwekeza kwenye huduma za kijamii badala ya kutafuta faida pekee.
“Stanbic wameamua kurudisha kwa jamii kupitia msaada wenye thamani kubwa. Wangeweza kutoa mikopo wakapata faida, lakini wamechagua kusaidia afya, elimu na mazingira. Tunawapongeza kwa moyo huu wa kujitolea,” alisema.
Bi. Mbawala alitoa wito kwa uongozi wa kituo kuhakikisha vifaa hivyo vinatunzwa ili viwanufaishe wakazi wa Goba na maeneo ya jirani.

.jpeg)
.jpeg)


No comments:
Post a Comment