Foreign Exchange Rates

CRDB Bank Advert_070325

Selcom Pesa Advert_110225

Selcom Pesa Advert_110225

Standard Chartered Advert_300125

Standard Chartered Advert_300125

Thursday, 9 October 2025

NMB YAPIGA JEKI MAADHIMISHO YA WIKI YA VIJANA NA MWENGE WA UHURU KWA SH. MILIONI 30

Mbeya. Benki ya NMB imeikabidhi Ofisi ya Mkoa wa Mbeya hundi ya Shilingi Milioni 30 kwa ajili ya kudhamini maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa na Sherehe za Kuzima Mwenge wa Uhuru zitakazofanyika tarehe 14 Oktoba 2025 jijini Mbeya.

Akikabidhi hundi hiyo kwa Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, Meneja wa NMB Kanda ya Nyanda za Juu, Wogofya Mfalamagoha, alisema udhamini huo ni mwendelezo wa jitihada za benki hiyo kuunga mkono shughuli mbalimbali za maendeleo zinazoratibiwa na serikali.

“Fedha hizi ni sehemu ya mchango wetu kusaidia maandalizi ya sherehe hizi muhimu kwa taifa. Katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, NMB imetoa udhamini wa zaidi ya Shilingi Milioni 439 kwa ajili ya mbio za Mwenge wa Uhuru,” alisema Mfalamagoha.

 

Uwajibikaji kwa Jamii

Mfalamagoha alieleza kuwa kupitia Mfuko wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR), NMB imekuwa ikitekeleza miradi inayolenga kutatua changamoto katika sekta za elimuafya, na misaada ya kijamii, hasa nyakati za majanga.

“Kwa zaidi ya miaka kumi mfululizo, tumekuwa tukitenga asilimia 1% ya faida yetu kila mwaka kusaidia jamii. Udhamini huu ni uthibitisho wa dhamira yetu ya kuhakikisha jamii inanufaika na mafanikio ya benki,” aliongeza.

Hivi karibuni, Jarida la Global Banking & Finance Magazine lenye makao yake New Jersey, Marekani, liliitambua NMB kama Kinara wa Uwajibikaji kwa Jamii Tanzania 2025 na Benki Salama Zaidi nchini Tanzania.

Mtandao na Ubunifu

Kwa sasa NMB inajivunia mtandao mpana wenye matawi 242 nchini, mashine za ATM 720, zaidi ya mawakala 60,000, na wateja zaidi ya milioni 8.7.

Katika kuongeza upatikanaji wa huduma, benki imeanzisha bidhaa bunifu kama MshikoFasta, huduma ya mikopo ya kidijitali isiyohitaji dhamana, ambapo wateja wanaweza kukopa kuanzia Sh. 1,000 hadi Sh. 1,000,000 kupitia simu zao za mkononi.

Serikali Yaipongeza NMB

Akizungumza baada ya kupokea hundi hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Beno Malisa, aliishukuru NMB kwa udhamini huo, akisema utasaidia maandalizi ya maadhimisho hayo muhimu ya kitaifa.

“Tunawashukuru sana NMB kwa mchango huu mkubwa. Naomba taasisi nyingine ziige mfano huu wa kurudisha sehemu ya faida kwa jamii,” alisema Malisa.

Aliongeza kuwa NMB imeendelea kushirikiana na serikali katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo na akatoa wito kwa wananchi wa mkoa huo kuendelea kuiamini benki hiyo kwa huduma bora na salama za kifedha.

Maadhimisho ya Wiki ya Vijana Kitaifa 2025 yatahitimishwa Oktoba 14 jijini Mbeya, siku ambayo pia itaambatana na kumbukumbu ya miaka 26 tangu kifo cha Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Kambarage Nyerere, pamoja na uzimaji wa Mwenge wa Uhuru.

No comments:

Post a Comment