Dar es Salaam, Septemba 25, 2025 – Mwanariadha wa kimataifa wa Tanzania na mshindi wa mbio ndefu za Mashindano ya Dunia ya Riadha ya Tokyo, Alphonce Simbu, amefichua kuwa siri kubwa ya ushindi wake ni maandalizi ya muda mrefu pamoja na motisha aliyopata kupitia NBC Dodoma Marathon iliyofanyika Julai mwaka huu.
Akizungumza jana jioni katika hafla fupi iliyoandaliwa na Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) kwa ajili ya kumpa pongezi maalum, Simbu alisema licha ya ushindani mkali kutoka kwa wanariadha wa kimataifa, maandalizi na morali kubwa kufuatia ushindi wa mbio za kilomita 21 za NBC Dodoma Marathon vilimpa nguvu ya kushinda Tokyo.
Hafla hiyo ilifanyika makao makuu ya NBC jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na maofisa waandamizi wa benki hiyo wakiongozwa na Mkurugenzi Mtendaji Theobald Sabi, pamoja na wadau wa riadha wakiongozwa na Rais wa Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), Rogath John Akhwari, ambaye alifuatana na baadhi ya wanariadha akiwemo Simbu.
“Ushiriki na ushindi wangu katika mbio za kilomita 21 za NBC Dodoma Marathon ulikuwa chanzo cha morali niliyokuwa nayo niliposhiriki mashindano ya Tokyo. Nilizitumia mbio za Dodoma kama kipimo cha utimamu wangu kimwili, na ushindi wangu pale ndio ulikuwa mwanzo wa ushindi wangu jijini Tokyo,” alisema Simbu.
Aidha, aliwashukuru waandaaji wa NBC Dodoma Marathon kwa kuweka mashindano yenye ushindani, akisisitiza kuwa sasa yanatumika kama kipimo sahihi kwa wanariadha wa Kitanzania kabla ya kushiriki mashindano makubwa zaidi duniani.
Simbu pia aliishukuru serikali, wadau wa michezo, na benki ya NBC kwa pongezi na mchango wao katika kukuza riadha nchini.
“Nimepokea salamu nyingi za pongezi, ikiwemo kutoka kwa Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan. Leo nimepokea pongezi rasmi kutoka NBC, wadau muhimu sana wa michezo nchini. Hii ni ishara ya kuthamini mchango wangu na mchezo wa riadha kwa ujumla,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Theobald Sabi, alimpongeza Simbu kwa kuandika historia mpya kupitia muda wa 2:09:48 katika mashindano ya Tokyo.
“Kwa niaba ya Bodi na Menejimenti ya NBC, tunashukuru RT na Simbu kwa kuipeperusha bendera ya Tanzania. Kama mwanafamilia wa NBC Dodoma Marathon, ushindi wake ni fahari kubwa kwa taifa letu,” alisema Sabi.
Naye Rais wa RT, Rogath John Akhwari, alisisitiza mchango wa NBC Dodoma Marathon katika kuinua viwango vya riadha nchini.
“Medali hii ya dhahabu haijawahi kuletwa nchini hapa kabla. Imekuja wakati ambao NBC Dodoma Marathon imekua mbio yenye hadhi ya kimataifa. Hii ni uthibitisho kwamba sasa tuna mashindano ya ndani yanayoweza kutumika kupima uwezo wetu kimataifa,” alisema Akhwari.
Akhwari aliongeza kuwa RT ipo kwenye mchakato wa kuanzisha programu ya kisasa ya kuandaa vijana na watoto ili kuendeleza mafanikio yanayoendelea kuonekana katika mchezo wa riadha nchini.








No comments:
Post a Comment