Arusha, Julai 21, 2025 — Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imekutana na wateja wake wakubwa kutoka mashirika binafsi, taasisi mbalimbali, na wateja wa kawaida (corporates) jijini Arusha ili kujadili fursa za biashara, kuwasilisha huduma mpya za benki hiyo, na kuwajengea wateja uelewa mpana juu ya faida na manufaa ya huduma hizo. Aidha, benki hiyo ilitumia fursa hiyo kupata mrejesho wa moja kwa moja kuhusu jinsi ya kuendelea kuboresha huduma zake ili ziendane na mahitaji halisi ya wateja wake.
Katika kufanikisha hilo, NBC kupitia kitengo chake cha Biashara na Uwekezaji (CIB) iliandaa hafla maalum ya chakula cha jioni iliyoongozwa na Mkurugenzi wa Wateja Wakubwa wa NBC, Bw. Elvis Ndunguru, akiwa ameambatana na maofisa waandamizi kutoka makao makuu na matawi ya benki hiyo jijini Arusha.
Akizungumza kwenye hafla hiyo, Bw. Ndunguru alisema tukio hilo ni sehemu ya jitihada endelevu za benki hiyo kuwa karibu zaidi na wateja wake, hasa kwa kutambulisha huduma mpya kama NBC Connect, ambayo imelenga kuleta suluhisho la kifedha kwa kundi hilo la wateja.
“Tukiwa kama muhimili muhimu wa utoaji wa huduma za kifedha nchini, NBC tunatambua umuhimu wa utoaji wa huduma bora na kukuza ushirikiano kati yetu na wateja wetu. Hii inasababishwa na mabadiliko yanayoletwa na ubunifu wa kiteknolojia tunaoendelea kuufanya kila siku,” alisema Bw. Ndunguru.
Aliongeza kuwa kupitia hafla hiyo, benki ilielezea maboresho makubwa yaliyofanyika kwenye huduma zake pamoja na kuzindua huduma mpya zilizo rahisi na za kidigitali, zinazokidhi mahitaji ya wateja wakubwa wa taasisi hiyo.
Huduma ya NBC Connect ilielezwa kuwa ni sehemu ya mpango mpana wa benki hiyo wa kuwasogezea huduma karibu zaidi wateja wa kada ya juu, wakiwemo mashirika binafsi, taasisi za serikali, na makampuni makubwa.
“Tunaamini kuwa msingi wa huduma za kipekee ni kuelewa mahitaji na matarajio ya wateja wetu. Matukio kama haya yanatupa nafasi ya kupata mitazamo mpya ambayo hutuwezesha kuboresha zaidi huduma zetu na uzoefu wa wateja,” alifafanua.
Mkakati wa Kukuza Ushirikiano wa Kibiashara
Bw. Ndunguru alibainisha kuwa NBC imekuwa ikijikita katika utoaji wa suluhisho bunifu za kifedha, teknolojia ya kisasa, ubia wa kimkakati, na kuchangia ukuaji wa uchumi huku ikizingatia masuala ya jamii kama vile elimu, afya, na uhifadhi wa mazingira.
“Tunazialika jumuiya za wafanyabiashara kuangalia kwa upana zaidi fursa zinazotokana na ushirikiano na taasisi hii ya kifedha yenye dira ya mafanikio ya wateja wake. NBC inalenga kuwa mshirika mwaminifu na anayeaminika kwa maendeleo ya biashara nchini,” alibainisha Ndunguru.
Maoni ya Wateja
Baadhi ya wateja wa NBC waliokuwepo kwenye hafla hiyo waliipongeza benki kwa hatua hiyo, wakieleza kuwa imekuja wakati muafaka hususan kipindi hiki ambacho Mkoa wa Arusha unashuhudia ukuaji mkubwa wa uchumi unaochagizwa na sekta ya utalii, biashara, kilimo, na viwanda.
“Kwa sasa Arusha iko kwenye kasi kubwa ya maendeleo ya kiuchumi, hasa kupitia sekta ya utalii. Ni jambo la faraja kuona NBC inatambua umuhimu wa kuwa bega kwa bega na wadau wake kwa kuwaletea huduma bora na za kisasa, ikiwemo huduma za kidigitali ambazo zimekuwa mkombozi katika masuala ya miamala na makusanyo ya serikali,” alisema Bw. Abdallah Kiwango kutoka TANAPA.
Endelea kutembelea blogu yetu kwa taarifa zaidi kuhusu huduma za kifedha, mafanikio ya taasisi za kifedha, na maendeleo ya sekta mbalimbali nchini.










No comments:
Post a Comment