Dar es Salaam, 10 Juni 2025 – Katika kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake, Vodacom Tanzania PLC imezindua kampeni kubwa ya kitaifa inayobeba kauli mbiu ya “Tupo Nawe, Tena na Tena”, ikilenga kusherehekea mafanikio makubwa iliyopata katika kuwaunganisha Watanzania tangu mwaka 2000.
Kampeni hii ya miezi minne, inayotarajiwa kudumu kutoka Juni hadi Oktoba 2025, inalenga kusisitiza nafasi ya Vodacom kama sehemu muhimu ya maisha ya kila siku ya Watanzania – kutoka enzi za mawasiliano ya sauti hadi zama hizi za kidijitali zenye huduma bunifu kama M-Pesa, mtandao wa 5G, elimu kwa njia ya simu, huduma za afya mtandaoni na biashara za kidijitali.
“Miaka 25 ya Mahusiano na Maendeleo ya Teknolojia”
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC, Bw. Philip Besiimire, alisema:
“Miaka 25 ya Vodacom siyo tu kuhusu teknolojia; ni kuhusu mahusiano tuliyojenga na maisha ya Watanzania tuliyoyagusa. Kupitia ‘Tupo Nawe, Tena na Tena,’ tunawashukuru Watanzania kwa kutuamini na kutufanya kuwa mtandao wa mawasiliano unaoaminiwa zaidi nchini. Na bado tupo – na tutaendelea kuwa nanyi kwa miaka mingi ijayo.”
Bw. Besiimire aliongeza kuwa mafanikio ya Vodacom yamejengwa juu ya ubunifu wa huduma kama M-Pesa, iliyozinduliwa mwaka 2008, ambayo imeleta mapinduzi makubwa katika sekta ya fedha na kusaidia kuimarisha ujumuishi wa kifedha nchini. Aidha, kupitia mtandao wa 5G wa kwanza nchini, Vodacom inaendelea kuwaunganisha Watanzania na ulimwengu wa kidijitali.

Huduma Mtaani Kupitia Msafara Maalum
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Biashara, Bi. Brigita Shirima, alieleza kuwa Vodacom itawaendea moja kwa moja wateja kupitia msafara maalum utakaotembelea mikoa yote ya Tanzania Bara na Visiwani.
“Tutakuwa mitaani tukitoa zawadi, kuuza simu janja kwa bei nafuu, kutoa huduma za bure kama WiFi, kutambua mawakala na wabia wetu, pamoja na kushiriki katika shughuli mbalimbali za kijamii kupitia programu ya ‘Siku 25 za Upendo’,” alisema Bi. Shirima.
Bi. Shirima alisisitiza kuwa kampeni hii ni ya kipekee kwa sababu inalenga kuwaenzi Watanzania kama mhimili wa mafanikio ya Vodacom. Aliwasihi wateja wote kushiriki kikamilifu katika shughuli mbalimbali za kampeni hiyo.
Zaidi ya Miaka 25 ya Kuaminika
Kwa mujibu wa takwimu za Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Vodacom kwa sasa inahudumia zaidi ya wateja milioni 28 nchini. Katika maadhimisho haya ya miaka 25, kampuni hiyo inaahidi kuendelea kuboresha huduma zake kwa viwango vya juu, sambamba na mahitaji ya kizazi cha sasa na kijacho.
No comments:
Post a Comment