Na Mwandishi Wetu – Ngorongoro, Arusha
Benki ya NMB, kupitia kampeni yake ya NMB Kijiji Day, imefanya shughuli mbalimbali za kijamii katika Tarafa ya Loliondo, Wilaya ya Ngorongoro mkoani Arusha, ikiwa ni sehemu ya juhudi zake za kuwa karibu zaidi na wananchi wa maeneo ya vijijini. Shughuli hizo zilijumuisha michezo, elimu ya fedha, pamoja na uhamasishaji wa vijana kuhusu fursa zilizopo kupitia michezo na ujasiriamali.
Tukio hilo lilifanyika katika Uwanja wa WASSO na liliwajumuisha wakazi wa eneo hilo waliopata fursa ya kushiriki katika michezo mbalimbali kama jogging na mpira wa miguu. Mechi ya kuvutia kati ya timu ya Loliondo na Serengeti ilipamba tamasha hilo, ambapo timu ya Serengeti iliibuka kidedea kwa ushindi wa mabao 3–1.
Elimu ya Fedha kwa Wananchi
Mbali na burudani ya michezo, Benki ya NMB ilitoa elimu ya fedha kwa vikundi vya ujasiriamali, ikilenga kuwawezesha wakazi wa Ngorongoro kuelewa mbinu za kuendesha biashara kwa tija. Zaidi ya watu 150 walifikiwa, wakifundishwa kuhusu umuhimu wa kuhifadhi fedha, namna ya kupata mikopo, na kutumia huduma za kifedha katika kukuza uchumi wao.
Bw. Innocent Mwanga, Afisa Masoko wa NMB Kanda ya Kaskazini, alieleza kuwa benki hiyo imejipanga kuendelea kushirikiana na jamii katika kuimarisha michezo na kuinua uchumi wa wananchi kupitia elimu ya fedha.
"Tutaendelea kuwa karibu na wananchi wa vijijini na kutumia kampeni kama NMB Kijiji Day kuwa jukwaa la kubadilisha maisha yao kupitia elimu, michezo na huduma za kifedha," alisema Bw. Mwanga.
Vijana Watoa Wito wa Kuanzishwa kwa Ligi Rasmi
Katika tukio hilo, vijana wa Ngorongoro walitoa wito kwa wadau na wapenzi wa soka kuanzisha ligi rasmi za wilaya, ili kusaidia kuinua vipaji vya michezo, kuwaepusha vijana na vishawishi, na kuwahamasisha kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo kupitia michezo.

Ushuhuda Kutoka kwa Wananchi
Wakazi wa Ngorongoro, akiwemo Philemon Molel, wameipongeza Benki ya NMB kwa ubunifu wa kufikisha huduma vijijini:
“Tunaishukuru NMB kwa kutuletea elimu ya fedha moja kwa moja vijijini. Hii imetufungua macho kuhusu namna ya kutumia huduma za benki kuinua biashara na maisha yetu,” alisema Molel.
NMB Kijiji Day: Jukwaa la Mabadiliko
Kampeni ya NMB Kijiji Day imejikita kuwa jukwaa la kipekee linalounganisha huduma za kifedha, michezo na elimu ya jamii kwa wananchi wa vijijini. Kupitia kampeni hii, benki hiyo inaendelea kujenga misingi ya maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii.
#NMBCares | #NMBKijijiDay | #ElimuYaFedha | #MichezoNaMaendeleo
No comments:
Post a Comment