DAR ES SALAAM, 27 JUNI 2025
Katika kuadhimisha miaka 25 tangu kuanzishwa kwake nchini Tanzania, Vodacom Tanzania PLC imezindua kampeni maalum ya kitaifa iitwayo "Tupo Nawe, Tena na Tena", kama sehemu ya kutambua mchango wake katika kuimarisha mawasiliano na huduma za kidijitali kwa Watanzania.
Kampeni hiyo ya miezi minne inalenga kuwakumbusha wananchi namna ambavyo Vodacom imekuwa mshirika wa karibu katika safari ya maisha yao – kuanzia enzi za simu za kawaida hadi zama za kisasa za huduma za mtandao wa kasi wa 5G, M-Pesa, afya mtandaoni na elimu kupitia simu janja.
Tangu kuingia sokoni miaka 25 iliyopita, Vodacom imeendelea kuleta mapinduzi ya mawasiliano nchini, ikiongoza katika kutoa huduma bunifu zinazogusa nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Kupitia kampeni hii, kampuni hiyo inatoa shukrani kwa wateja wake wote waliokuwa sehemu ya mafanikio hayo, huku ikiahidi kuendelea kuwa mstari wa mbele katika utoaji wa huduma bora, za kisasa na zinazokidhi mahitaji ya wakati.
“Tumekuwa pamoja na Watanzania kwa miaka 25 – katika mafanikio, changamoto na mabadiliko ya teknolojia. Tunaahidi kuendelea kuwa sehemu ya maisha yao kwa ubunifu zaidi katika miaka mingi ijayo,” imesema sehemu ya taarifa ya kampuni hiyo.
Kwa hatua hii, Vodacom inajidhihirisha tena kama mtandao unaoaminika zaidi nchini na mwezeshaji mkuu wa Tanzania kuelekea uchumi wa kidijitali.
No comments:
Post a Comment