DAR ES SALAAM, Juni 26, 2025 – Benki ya Taifa ya Biashara (NBC), mdhamini mkuu wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara (NBC Premier League), imekabidhi rasmi kombe la ubingwa kwa klabu ya Yanga SC baada ya kuibuka kidedea kwa msimu wa 2024/2025. Hafla hiyo muhimu ilifanyika kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, ikiambatana na mechi ya mwisho ya msimu dhidi ya wapinzani wao wa jadi, Simba SC.
Katika mtanange huo maarufu kama ‘Kariakoo Derby’, Yanga SC iliibuka na ushindi wa mabao 2-0, na hivyo kutawazwa mabingwa rasmi wa ligi hiyo. Tukio la kukabidhi kombe lilihudhuriwa na maelfu ya mashabiki pamoja na viongozi mbalimbali akiwemo Makamu wa Kwanza wa Rais wa TFF, Athuman Nyamlani, na Mkurugenzi Mtendaji wa NBC, Bw. Theobald Sabi.
NBC Yajizatiti Kuendeleza Maendeleo ya Soka
Akizungumza katika hafla hiyo, Bw. Sabi alieleza kuwa NBC inajivunia kuwa sehemu ya mafanikio ya Ligi Kuu ya Tanzania kupitia udhamini wake wa kudumu, akiongeza kuwa benki hiyo ina dhamira ya kuwekeza zaidi kwenye maendeleo ya wachezaji na ustawi wa mchezo huo.
“Tangu tuanze kudhamini Ligi Kuu ya NBC, tumeshuhudia ushindani mkubwa na wa kuvutia. Ushindani huu si tu umepandisha kiwango cha mchezo, bali pia umetuletea burudani ya hali ya juu,” alisema Sabi.
Alisisitiza kuwa msimu ujao benki hiyo itaongeza nguvu zaidi katika maeneo kama vile:
- Programu za maendeleo ya vijana
- Huduma za bima bora kwa wachezaji, hasa ya afya
- Huduma mahsusi za kifedha kwa wanamichezo ili kuwawezesha kiuchumi kupitia usimamizi bora wa fedha.
NBC Yakaribisha Mashabiki kwa Njia Mbali Mbali
Katika kuhakikisha mashabiki wake wanashiriki kikamilifu kwenye mchezo huo wa kihistoria, NBC iliandaa:
- Usafiri maalum kwa maofisa na wateja wake jijini Dar es Salaam
- Maonyesho ya moja kwa moja kupitia skrini kubwa kwenye maeneo mbalimbali ya jiji na mikoani
- Huduma za benki zilizotolewa na timu ya masoko ya NBC katika maeneo ya tukio na viunga vya uwanja
Haya ni miongoni mwa jitihada zinazodhihirisha dhamira ya NBC kuendelea kuibeba Ligi Kuu na kukuza mchezo wa soka nchini.
Endelea kutembelea blogu yetu kwa taarifa zaidi kuhusu maendeleo katika sekta ya michezo, benki, biashara, na uchumi. Kila wiki tunakuletea taarifa mpya, uchambuzi wa kina, na makala maalum kwa ajili ya kukuimarisha kielimu na kiuwekezaji.
No comments:
Post a Comment