Foreign Exchange Rates

Selcom Pesa Advert_110225

Selcom Pesa Advert_110225

Standard Chartered Advert_300125

Standard Chartered Advert_300125

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

Tuesday, 4 March 2025

WAZIRI MKUU AZINDUA NBC KIGANJANI, AHIMIZA TAASISI ZA FEDHA KUOANISHA MIFUMO

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (katikati) akiongoza zoezi la uzinduzi rasmi wa huduma za kidijitali za Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) inayofahamika kama ‘NBC Kiganjani’ wakati wa hafla ya uzinduzi huo iliyofanyika jijini Dar es Salaam. Wengine ni pamoja na Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba (Mb) (wa tatu kushoto), Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Bi. Sauda Msemo (wa pili kushoto), Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi (wa tatu kulia), Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw Saad Mtambule (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji Bw Theobald Sabi (wa pili kulia) na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Bw Wallace Karia (kulia).
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa akizungumza kwenye hafla hiyo.

Dar es Salaam, March 3, 2025: Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amezindua rasmi huduma za kidijitali za Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) inayofahamika kama ‘NBC Kiganjani’ huku akitoa wito kwa mashirika na taasisi za fedha nchini kuhakikisha zinaboresha mifumo ya huduma za kielectronic kwa kuoanisha mifumo baina ya taasisi hizo.

Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba (Mb) akizungumza kwenye hafla hiyo.

Alisema hatua hiyo itarahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi zikiwemo utunzaji, utumaji na upokeaji wa fedha (Financial Inclusion).

Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa (katikati) akifurahia jambo sambamba na Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba (Mb) (kushoto), Mkurugenzi Mtendaji Bw Theobald Sabi (kulia) wakati wa hafla ya uzinduzi rasmi wa huduma ya kidijitali ya Benki ya Taifa ya Biashara (NBC).

Zaidi, Waziri Mkuu Majaliwa ameziagiza Wizara ya Fedha na Benki Kuu ya Tanzania (BOT) kusimamia uhamasishaji wa matumizi ya mfumo wa malipo kwa njia za kidigitali katika utoaji wa huduma mbalimbali za kifedha ikiwemo matumizi ya mashine ya POS na kadi hatua ambayo kwa kiasi kikubwa itasaidia kuchochea biashara ya ndani kwa kuwezesha miamala ya malipo kufanyika kwa uharaka, salama, na unafuu.

Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw Saad Mtambule akizungumza kwenye hafla hiyo.

Hafla uzinduzi huo imefanyika jijini Dar es Salaam ikihudhiriwa pia na Waziri wa Fedha Dkt Mwigulu Nchemba (Mb), Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi, Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Bw Saad Mtambule na Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Bi. Sauda Msemo.

Naibu Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Mhandisi Maryprisca Mahundi (pichani) akizungumza kwenye hafla hiyo.

Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya NBC Bw Theobald Sabi, aliwaongoza wafanyakazi wa benki hiyo sambamba na wadau mbalimbali wa sekta ya michezo walioongozwa na Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu nchini (TFF) Bw Wallace Karia.

Naibu Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT) Bi. Sauda Msemo akizungumza kwenye hafla hiyo.

Ni kutokana na kutambua umuhimu wa huduma za kidigitali katika utoaji wa huduma za kifedha katika kuchochea ukuaji wa uchumi ndio sababu Rais Samia Suluhu Hassan amenitumia nije kuwapongeza benki ya NBC kwa hatua hii muhimu ya mapinduzi ya kidigitali katika utoaji wa huduma za kifedha nchini…hongereni sana,’’ alipongeza.

Mkurugenzi wa Biashara, Bw Elvis Ndunguru (kushoto) akiongoza mjadala wakati wa hafla hiyo.

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu Majaliwa, hatua ya benki hiyo itasaidia serikali kuboresha ukusanyaji wa mapato kwa njia za kidijitali, kupunguza mianya ya ukwepaji wa kodi, na kuongeza uwazi katika mifumo ya fedha.



Aidha huduma hii itasaidia kuimarisha upatikanaji wa mikopo kwa wakulima, wafanyabiashara, na wajasiriamali wadogo kupitia mfumo rasmi wa kifedha, hatua inayochochea ukuaji wa uchumi. Kwa Biashara na Sekta Binafsi, NBC Kiganjani pia itachochea biashara ya ndani kwa kuwezesha miamala ya malipo kufanyika kwa uharaka, salama, na unafuu. Hili litahamasisha mzunguko wa fedha na kuchochea ukuaji wa sekta binafsi, ambayo ni mhimili mkubwa wa uchumi wetu.’’ Aliongeza.



Akizungumza kwenye hafla hiyo, Dkt Nchemba alisema hatua ya benki hiyo ni muhimu katika kuimarisha ujumuishi wa kifedha na kukuza uchumi wa kidijitali na kwamba Serikali itaendelea kushirikiana na sekta ya kifedha kuhakikisha kuwa huduma kama hizo zinawafikia wananchi wengi zaidi kwa ufanisi na usalama.

Zaidi niendelee kuwashukuru sana NBC kwa ufadhili wake kwenye masuala mbalimbali ya kijamii ikiwemo sekta ya michezo hususani kupitia mchango wake mkubwa katika kuboresha ligi kuu ya NBC…Hongereni sana’’ alipongeza.

Naye Bi Msemo pamoja na kupongeza hatua hiyo ya NBC, alitoa rai kwa taasisi za fedha nchini kuhakikisha zinawekeza zaidi kwenye mifumo ya kiulinzi kwa njia za kidigitali ili kuhakikisha usalama wa fedha za wateja wao kwa kuwa ukuaji unaoshuhidiwa sasa wa huduma za kidigitali unakwenda sambamba na ongezeko la wizi wa kupitia njia za kidigitali.

Awali akizingumza kwenye hafla hiyo Bw Sabi alisema huduma hiyo iliyoboreshwa ya Aplikesheni ya NBC Kiganjani na huduma ya NBC Lipa Kiganjani(Lipa namba ya NBC), zinalenga kuleta mapinduzi ya mfumo wa fedha nchini kwa manufaa ya Watanzania wote.

Na jambo la kufurahisha zaidi ni kwamba kupitia NBC Kiganjani App, mteja anaweza kufungua akaunti ya benki moja kwa moja kupitia simu yake ya mkononi na kuitumia papo hapo, bila kulazimika kutembelea tawi la benki. Huduma hii inarahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha na kuongeza ujumuishi wa kifedha kwa Watanzania wengi zaidi.’’

Zaidi ya hayo, kwa wateja wenye akaunti za mishahara, NBC Kiganjani inatoa mikopo ya papo hapo, kuhakikisha upatikanaji wa fedha kwa mahitaji ya dharura bila ucheleweshaji. Hili litasaidia kuharakisha miamala ya kifedha, hivyo kuchochea biashara na uzalishaji.’’ Alisema Sabi huku akibainisha kuwa kupitia huduma hiyo, mteja anaweza kuwekeza kwenye mifuko mbalimbali kama vile UTT na hati fungani za serikali na sekta binafsi.

Kwetu tunajivunia zaidi kuwafahamisha kwamba huduma hii ya Aplikesheni hii ya NBC Kiganjani na huduma nyingine tunazozindua leo, zimetengenezwa na wataalamu wa ndani wa NBC, ambao ni vijana wa Kitanzania.’’ Alisema.

No comments:

Post a Comment