Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emanuel Tutuba amesema kuwa Noti Mpya za Tanzania zenye Saini ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) na yeye mwenyewe, za toleo la mwaka 2010, zitaingia kwenye mzunguko kuanzia tarehe mosi Februari mwaka huu.
Gavana Tutuba amesema hayo wakati akimkabidhi Mhe. Dkt. Nchemba, Noti kifani za shilingi elfu kumi, elfu Tano, Elfu Mbili na Shilingi Elfu moja, katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha, Jijini Dar es Salaam, kwa mujibu wa Sheria na Taratibu zinazosimamia masuala ya fedha nchini.
Gavana Tutuba alifafanua kuwa Noti hizo zitatumika sambamba na Noti zilizopo hivi sasa, zinamwonekano wa Noti zinazotumika hivi sasa zilizotolewa Mwaka 2010, ikiwemo alama za usalama, ukubwa, rangi na mambo mengine, isipokuwa ina marekebisho kwenye saini ya Waziri wa Fedha, na Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania.
Akizungumza baada ya kupokea sampuli za Noti hizo mpya, Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alimshukuru Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuruhusu jambo hilo kufanyika na kumpongeza Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania, Bw. Emmanuel Tutuba, kwa kusimamia mchakato wa uchapaji wa Noti hizo kwa weledi na uadilifu mkubwa.
“Mpaka kufikia hatua hii ni heshima kubwa kwa Taifa letu na inaendeleza heshima ya wataalam wetu mnavyoweza kusimamia kwa umakini mambo yenye maslahi mapana kwa nchi yetu” Alisema Dkt. Nchemba.
Mhe. Dkt. Nchemba aliridhia Noti hizo ziingizwe kwenye mzunguko na kuanza kutumika kama ilivyopangwa tarehe moja Februari mwaka huu.
No comments:
Post a Comment