Serikali imeipongeza Benki ya NMB kwa kuzindua Mfuko Maalum uliotengewa Sh. Bilioni 100 za kukopesha wasambazaji na wauzaji wa Nishati Safi ya Kupikia kwa Watanzania, na kwamba Serikali itaingia kifua mbele katika Mkutano Mkuu wa Nishati wa Wakuu wa Nchi za Afrika (Mission 300), unaofanyika Januari 27 na 28 jijini Dar es Salaam.Pongezi hizo zimetolewa na Naibu Waziri Mkuu, Dk. Doto Biteko, wakati wa uzinduzi wa mfuko huo, aliobeba dhamira chanya ya kuunga mkono juhudi za Serikali katika Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia (2024-2034) na kwamba tukio hilo ni uthibitisho tosha wa ushirikiano uliopo baina ya Serikali na Sekta Binafsi katika kustawisha jamii ya Watanzania.
Kwa niaba ya Serikali na Wizara ya Nishati, Dk. Biteko aliishukuru NMB kwa wazo hili na kwamba wako tayari kuwaunga mkono ili jambo hilo likatimizwe, huku akisema wazo la kuhakikisha mawakala na wasambazaji wa nishati safi za kupikia wanapata mitaji ili kufikisha huduma mijini na vijijini, litasaidia kuchochea upatikanaji na matumizi ya nishati hiyo.
“Hakika mpango huu wa NMB kutenga Shilingi Bilioni 100 kwa ajili ya jambo hili, unastahili pongezi kubwa sana, hasa ikizingatiwa kuwa kama benki ina njia nyingi sana za biashara, ambazo wangeweza kuwekeza fedha hizo sehemu nyingine ili kuweza kuendelea kujizalishia faida zaidi.
“Lakini, msukumo huu wa kuja kuweka kiasi hiki kwenye Nishati Safi ya Kupikia inaonesha dhamira ya dhati ya benki kuchangia maendeleo endelevu kwa taifa letu la Tanzania, lakini ni kielelezo tosha cha uzalendo wa kweli uliopo kati yenu Menejimenti pamoja na wafanyakazi wa benki hii.
“Mtendaji Mkuu wa NMB tayari ameeleza hapa faida mbalimbali za matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia na mimi nisisitize kuwa, faida hizo za Afya Bora, Mazingira Safi, Kuboresha Uchumi na Ufanisi wa Nishati hizi na ukweli kuwa nishati safi ni salama, ndio maana hata Rais Samia Suluhu Hassan amekuwa kinara wa hili nchini, Afrika na duniani kote.
“Wote tunafahamu kwamba, licha ya ukosefu wa mitaji, changamoto kubwa ya wananchi kuendelea kutumia nishati isiyo safi ya kupikia, ni ukosefu wa elimu juu ya nishati safi ya kupikia, hivyo suala la NMB kuanza pia kutoa elimu ya hili ni jambo zuri na la kipekee sana kwa ustawi wa matumizi ya nishati hii safi.” Alisema Dk. Biteko.
Alibainisha kuiwa shukrani na pongezi kwa NMB hazitaishia tu katika Nishati Safi ya Kupikia tu, bali zinaenda pia kwa mambo makubwa ambayo imekuwa ikifanya kwa manufaa kwa taifa letu la Tanzania, ikiwemo misaada mbalimbali mashuleni, zahanati, vituo vya afya na hospitali na kuchagiza maendeleo endelevu kwa jamii, sambamba na upandaji miti.
Januari 27 na 28, Tanzania inatarajia kuwa mwenyeji wa mkutano uliopewa jina la Mission 300 kuakisi dhamira ya kuwafikia watu milioni 300 barani Afrika kuhakikisha wanatumia Nishati Safi, ambapo zaidi ya marais 25, Mawaziri wa Fedha na Nishati 60 wa Afrika, watashiriki mkutano huo, mweji akiwa Rais Dk. Samia Suluhu Hassan.