Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Tuesday 20 August 2024

DKT. BITEKO APONGEZA JITIHADA ZA CRDB BANK MARATHON KUSAIDIA WATOTO, WAKINAMAMA NA VIJANA

 
Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Dkt. Doto Biteko (katikati), akiwa ameongozana na Waziri wa Michezo, Dkt. Damas Ndumbaro (watatu kulia), Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila (wapili kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (watatu kushoto), Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Bank Foundation, Martin Warioba (kulia), Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela (wanne kushoto) pamoja na viongozi wengine wakianza mbio za kilometa tano katika kilele cha msimu wa tano wa CRDB Bank Marathon zilizofanyika viwanja vya farasi 'The Green Grounds' jijini Dar es salaam Agosti 18, 2024 na kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 8,000.


Dar es Salaam, 18 Agosti 2024 – Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati, Mhe. Dkt. Dotto Biteko ameipongeza taasisi ya CRDB Bank Foundation kwa kuendelea kuandaa mbio za CRDB Bank Marathon ambazo zimejielekeza katika kusaidia jitihada za serikali kuboresha sekta ya afya, kusaidia wenye uhitaji, pamoja na kukuza ustawi wa jamii.

Dkt. Biteko ametoa pongezi hizo wakati wa kilele cha msimu wa tano wa CRDB Bank Marathon ambapo Shilingi Milioni 350 zimekusanywa kwa ajili ya kusaidia watoto wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI), huduma za afya kwa wakinamama wenye ujauzito hatarishi hospitali ya CCBRT, na uwezeshaji wa vijana.


“Niwapongeze kwa kuendelea kusaidia matibabu ya wakinamama na watoto wetu. Wakinamama ndio wamebeba uchumi wa Taifa letu. Lakini pia wakinama ndio waangalizi wa familia zetu hususani watoto. Hivyo ukiimarisha afya ya mama na watoto umeimarisha afya ya Taifa,” amesema Dkt. Biteko huku akisema Serikali na Watanzania wanaona jitihada hizo zinazofanywa na Benki ya CRDB kupitia CRDB Bank Foundation.


Akizungumza Waziri wa Sanaa, Utamaduni, na Michezo, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema CRDB Bank Marathon imesaidia kwa kiasi kikubwa kuchochea ari ya michezo nchini. Dkt. Ndumbaro amesema mbio hizo zimekuwa jukwaa muhimu kwa wanariadha nchini kuonyesha vipaji vyao katika jukwaa la kimataifa kwani mbio hizo zimesajiliwa kimataifa na Shirikisho la Upimaji Mbio Kimataifa (AIMS) na Shirikisho la Riadha Duniani (World Athletic).

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema katika kiasi cha fedha kilichokusanywa; shilingi milioni 100 zitakwenda kusaidia watoto wenye uhitaji wa upasuaji wa moyo Taasisi ya Jakaya Kikwete (JKCI), Shilingi Milioni 100 kusaidia huduma za afya kwa wakinamama wenye ujauzito hatarishi hospitali ya CCBRT, na Shilingi Milioni 150 uwezeshaji wa vijana.


Katika mbio hizo zawadi za jumla ya Shilingi Milioni 98.7 zimetolewa kwa washindi 60 wa mbio za kilometa 42, 21, 10, 5, pamoja na mbio za baiskeli za kilometa 65. Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Bank Foundation, Martin Warioba amesema jumla ya washiriki waliojiandikisha mwaka huu ni 8,000 huku akisema lengo la mwaka kesho ni kupata washiriki 10,000 Tanzania, huku malengo ya washiriki Burundi na DRC wakiwa ni 3,000 kila nchi.

Mbio hizi zilizofanyika Dar es Salaam ni za tatu baada ya zile zilizofanyika nchini DRC, na Burundi. Nchini DRC mbio hizo zilifanyika tarehe 4 Agosti ambapo Dola za Marekani 50,000 zilikusanywa kusaidia kuboresha huduma za afya kwa watoto hospitali ya Jason Sendwe jijini Lubumbashi. Kwa upande wa nchini Burundi, mbio hizo zilifanyika tarehe 11 Agosti ambapo Faranga za Burundi Milioni 120 zilikusanywa kusaidia wahanga wa mafuriko mkoa wa Gatumba jijini Bujumbura.



Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo ya mbio hizo Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation, Tully Esther Mwambapa amewapongeza washindi wa mbio hizo, na kuwashukuru washirika wa mbio hizo wakiwemo kampuni za bima Sanlam na Alliance Life ambao ni washirika wakuu wa mbio hizo. “Tunawashukuru sana washirika wetu na wakimbiaji wote kwa kuungana nasi katika juhudi za kusambaza tabasamu kwa watoto walioathirika,” amesema Mwambapa.

Washindi wa mbio hizo Kilometa 42 upande wa wanawake ni Joyloyce Kemuma kutoka Kenya, upande wa wanaume mshindi ni Moses Nengichi kutoka Kenya. Kilometa 21 upande wa wanawake ni Sara Makera kutoka Tanzania, na upande wa wanaume ni Joseph Panga kutoka Tanzania. Kilometa 10 upande wa wanawake ni Hamida Nasor kutoka Tanzania, na upande wa wanaume ni Mao Hindo Ako kutoka Tanzania.


Sara Makera mshindi wa mbio za Kilometa 21 upande wa wanawake ameeleza furaha yake kushiriki katika mbio hizo na kusema kuwa ushindi wake ni sehemu ya kusaida matibabu ya watoto wenye matatizo ya moyo na  matibabu ya wakinamama wenye ujauzito hatarishi hospitali ya CCBRT.

“Mimi kama mwanamke ninajisikia faraja kubwa kushiriki kusambaza tabasamu kwa watoto na wakinamama. Watu wanapaswa kufahamu kuwa afya bora ni haki ya kila mtoro na wakinamama pia hawastahili kupoteza maisha wakati wa kujifungua. Tunawashukuru CRDB Bank Foundation kwa kutuunganisha pamoja katika juhudi hizi,” amesema.








No comments:

Post a Comment