Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Monday 5 August 2024

CRDB MARATHON CONGO YAKUSANYA DOLA 50,000 KUSAIDIA WODI YA WATOTO DRC

Gavana wa Jimbo la Haut-Katanga, Jacques Kyabula (katikati) akimkabaizi mfano wa hundi yenye thamani ya Dola za Marekani 50,000 Waziri wa Afya, Joseph Nsambi Bulanda wa Haut-Katanga (watatu kulia), zilizokusanywa katika CRDB Bank Marathon Congo iliyofanyika Agosti 4 2024 katika jiji la Lubumbashi DRC. Wengine pichani ni Balozi wa Tanzania nchini DRC, Said Mshana (wapili kulia), Mwenyekiti wa Bodi ya Kundi la Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay (watatu kushoto), Mwenyekiti wa Bodi wa CRDB Bank DRC, Dkt. Fred Msemwa (wapili kushoto), Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kundi la Benki ya CRDB, Bruce Mwile (wakwanza kushoto) na Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank DRC, Jessica Nyachiro.

Lubumbashi – CRDB Bank Marathon imefanyika kwa mara ya kwanza nje ya mipaka ya Tanzania katika jiji la Lubumbashi ambapo zaidi ya wakimbiaji 1,000 wameshirikina kufanikisha lengo la kukusanya USD 50,000 kwa ajili ya kusaidia wodi ya watoto katika Hospitali ya Jason Sendwe.

Mgeni rasmi katika mbio hizo ambazo zimeweka historia katika marathon ambazo zimewahi kufanyika katika jiji la Lubumbashi alikuwa ni Gavana wa Jimbo la Haut-Katanga Mhe. Jacques Kyabula ambaye aliambatana na mawaziri 10 wa Jimbo hilo wakiongozwa na Waziri wa Michezo, pamoja na Waziri wa Afya.


Akizungumza baada ya kumalizika kwa mbio hizo za hisani zilizobeba kaulimbiu isemayo ‘Tabasamu Limevuka Mipaka’ Gavana Kyabula ameipongeza Benki ya CRDB kwa kuwaleta pamoja WaCongo pamoja na washiriki kutoka mataifa ya jirani kuja kuchangia kuboresha huduma za afya kwa watoto na kukuza ustawi wa jamii.

"Tunaishukuru CRDB Bank Marathon kwa kusaidia jitihada za Serikali kuboresha huduma za afya kwa wananchi. Serikali yetu inatoa kipaumbele kikubwa katika afya, na tunafurahishwa na jitihada zinazofanywa na Benki ya CRDB katika kusaidia kuboresha afya ya watoto," alisema Gavana Kyabula.


Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini DRC, Balozi Said Mshana aliipongeza Benki ya CRDB kwa juhudi zake za kukuza mahusiano ya kimataifa na kuimarisha umoja na mshikamano katika jamii. Balozi Mshana alisema mbio hizo zilizozaliwa Tanzania zinaonyesha ubunifu ambao taasisi za kitanzania zinaweza kupeleka nje ya nchi katika kusaidia kukuza ustawi wa jamii.

Naye Mwenyekiti wa Bodi ya CRDB Bank DRC, Dkt. Fred Msemwa alieleza kuwa marathon hiyo ni sehemu ya mkakati wa Benki kusaidia juhudi za serikali katika kukuza ustawi wa watu wa Congo. "Marathon hii si tu inahamasisha michezo, bali pia inajenga utamaduni wa kujitolea kwa jamii.

Benki yetu inaamini kwa kuwaleta watu pamoja tunaweza kuyafikia makundi mengi kwa urahisi na hivyo kukuza ustawi wa jamii kupitia programu bunifu kama CRDB Bank Marathon, lakini pia kupitia huduma na bidhaa zetu bunifu tutaweza kusaidia jitihada za kukuza ujumuishi wa kifedha na kiuchumi," alisema.


Akitangaza matokeo ya mbio hizo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Congo, Jessica Nyachiro, aliwashukuru washirika wa mbio hizo Africell, Orange, Ogowe Cleaning, Kin Marche, Policlynique Delta, Shalina, Vinmart Foundation, SUNU Insurance, na Dukan. “Pamoja na kuwa huu ni mwaka wa kwanza kwa mbio hizi lakini mwitikio umekuwa mkubwa sana. Tunawashukuru sana washirika wetu na wakimbiaji wote mlioungana nasi kusambaza tabasamu kwa watoto.”

Marathon iliyofanyika leo Lubumbashi ni ya kwanza kati ya tatu ambazo zimepangwa kufanyika mwaka huu nchini DRC, Burundi, na Tanzania. Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank Foundation ambao ndio waandaji wa mbio hizo, Tully Esther Mwambapa ameeleza furaha yake baada ya mbio hizo zilivyopokelewa vizuri sana nchini DRC.

Tully amewashukuru Watanzania ambao wamejitokeza kwa wingi kushiriki mbio hizo za DRC ikiwamo kuwashukuru washirika wakuu wa mbio hizo Sanlam, CRDB Insurance Company, na Clouds Media. "Nitumie nafasi hii kuwakaribisha watu wote kuendelea kujisajili kwa mbio za Burundi tarehe 11 Agosti na Tanzania tarehe 18 Agosti," aliongezea.

Papy Kayombo, mshindi wa mbio za Kilometa 21 katika CRDB Bank Marathon Congo, ameeleza furaha yake ya kushiriki katika mbio hizo na kusema ushindi wake ni sehemu ya kusambaza tabasamu kwa watoto ambao watapata matibabu katika hospitali ya Jason Sendwe.

Kayombo alisema, "Katika jiji la Lubumbashi utamaduni huu ni mpya na ninaona utasaidia sana kujenga mshikamano katika jamii. Naipongeza sana Benki hii yetu ya CRDB, imeonyesha upendo mkubwa sana kwa watoto wetu na sisi tunaahidi kuiunga mkono."

Viongozi hao pia waliambatana na Balozi wa Tanzania nchini DRC, Balozi Said Mshana, Balozi wa Burundi nchini DRC, pamoja viongozi mbalimbali wa Benki ya CRDB wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay, na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Bruce Mwile.





No comments:

Post a Comment