Morogoro, Agosti 11, 2024: Benki ya Taifa ya Biashara imesisitiza dhamira yake ya kufadhili masomo ya wakunga 500 hadi kufikia mwaka 2028 ikiwa ni sehemu ya mkakati wa benki hiyo katika kuboresha sekta ya afya kupitia uzazi salama na kupunguza vifo vya watoto na kina mama katika sehemu mbalimbali nchini hususani zile zenye uhaba mkubwa wa wataalamu hao.
Dhamira hiyo ya NBC imewekwa wazi na Meneja wa benki hiyo tawi la Morogoro, Bw Deusdedit Mashalla wakati akizungumza kwenye Mahafali ya tano ya Stashahada ya Uuguzi, Ukunga na Teknolojia ya Maabara katika Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Morogoro (MCOHAS), yaliyofanyika chuoni hapo mwishoni mwa wiki. Benki ya NBC kwa kushirikiana na Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation ilifadhili masomo ya wakunga 50 kati ya wahitimu 151 waliohitimu kwenye mahafali hayo.
Kwa mujibu wa Bw Mashalla, kupitia makubaliano ya benki hiyo na Taasisi ya Benjamin Mkapa inayoratibu mpango huo, wakunga wanaotarajiwa kupatikana kupitia mpango huo ni wale ambao tayari wapo kwenye ajira na watajengewa uwezo zaidi ili wakahudumu katika maeneo yenye uhitaji mkubwa wa wataalamu hao hapa nchini.
“Lengo haswa ni kuhakikisha ifikapo mwaka 2028 jumla ya wanufaika wa ufadhili huu inafika 500 ili waende kuokoa maisha ya kina mama na watoto huko kwenye maeneo ya pembezoni kwa kuwa kwasasa ndio yanakabliwa na uhaba mkubwa wa wataalamu hawa. Leo wamehitimu 49 mmoja alipata changamoto hivyo hajafanikiwa kuhitimu na wengine 50 wanatarajiwa kunufaika na mpango huu huko Mwanza hivi karibuni kwa kushirikiana na wenzetu wa Taasisi ya Benjamin Mkapa,’’ alisema.
Kwa mujibu wa Bw Mashalla mpango huo unawezeshwa kupitia mbio za NBC Dodoma Marathon zinazofanyika kila mwaka jijini Dodoma ambapo mbali na kufadhili masomo hayo, mbio hizo pia zimekuwa zikibeba jukumu la kusaidia mapambano dhidi saratani ya shingo ya kizazi kwa wanawake kupitia utoaji elimu kwa umma na uchunguzi.
“Zaidi ya wanawake 40,900 wamefanyiwa uchunguzi kupitia mbio hizo ambapo wanawake 1,600 miongoni mwao waligundulika kuwa na vimelea vya saratani hiyo hatari zaidi na kupatiwa matibabu mapema,’’ aliongeza.
Katika hatua nyingine Bw Mashalla alilisitiza umuhimu wa elimu ya fedha kwa wahitimu hao pamoja na watumishi mbalimbali nchini ili kuwajengea uwezo utakaowawezesha kutumia vema fedha wanazozipata kwa manufaa yao kiuchumi, hatua aliyosema itawasaidia kuwaondolea msongo wa mawazo pindi wanapotimiza wajibu.
Kauli hiyo ya Bw Mashalla ililenga kuunga mkono ushauri ulitolewa na Mganga Mfawadhi wa Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro Dkt. Daniel Nkungu kwa wahitimu hao ambapo aliwasisitiza kuhakikisha wanatambua lengo kuu hasa la wao kuhudumu kwenye taaluma hiyo sambamba na kuwa na uelewa wa kutosha kuhusu masuala mazima ya fedha.
“Pamoja na kuwasisitiza sana kuhusu umuhimu wa nyinyi kufahamu lengo hasa la kuhudumu kwenye taaluma hii ndivyo pia, nawasisitiza sana kuhusu matumizi sahihi ya fedha zenu. Kuna uhusiano mkubwa sana wa hali ya uchumi wa watumishi wakiwemo wa afya na ubora wa huduma wanazozitoa kwa wananchi.’’
“Mtumishi ambae anakuja kwenye majukumu yake akiwa na msongo wa mawazo kutokana na madeni na hali mbaya kiuchumi anaweza kuingiza hasira hizo kwa wale anaowahudumia au hata wafanyakazi wenzie na hivyo kuathiri ubora wa huduma anayoitoa…nawaomba sana msiingie kwenye mtego huo,’’ alisisitiza.
Awali akizungumza kwenye mahafali hayo Mkuu wa Chuo hicho, Evarist Urassa alitoa wito kwa wahitimu hao pamoja na watumishi wengine wa afya wanaohudumu kwenye maeneo mbalimbali nchini kuhakikisha wanajiendeleza kielimu mara kwa mara ili kuendana na mabadiliko makubwa ya kitaaluma yanayoendelea kushuhudiwa kwenye sekta hiyo yakichochewa na maendeleo ya kiteknolojia yanayoendelea kushuhudiwa duniani.
“Leo hii nyie mnahitimu masomo ya stashahada na mnaenda kuhudumia jamii, lakini mjue bado safari ya kimasomo inaendelea. Rai yangu kwenu na wengine ambao wapo kwenye majukumu yao tayari wakumbuke kujiendeleza kwa kuwa taaluma hii inapokea teknolojia mpya kila siku na hata mbinu za kimatibabu pia zinabadilika kulingana na sababu mbalimbali zikiwemo ujio wa vimelea na magonjwa mapya kila siku,’’ alisema.
Aidha Mkuu huyo aliwaomba wadau mbalimbali kushirikiana na serikali kuboresha miundombinu ya chuo hicho kikongwe kilichoanzishwa mwaka 1975 ambapo tayari kinakabiliwa na uchakavu wa majengo na uhaba wa vifaa vya kujifunzia zikiwemo ‘computer’ na samani zake zikiwemo meza na viti.
Kwa upande wake Meneja Uhusiano wa Taasisi ya Benjamin Mkapa Foundation, Mariam Ndabagenga pamoja na kuwapongeza wahitimu, aliishukuru benki ya NBC kwa ufadhili wa masomo ya wakunga hao huku akiwasihi wahitimu hususani wanufaika wa program hiyo kuhakikisha wanaonyesha tofauti ya kiutendaji kwa kuwa bora zaidi pindi wanaporudi kwenye majukumu yao.
“Kama hamtaonyesha tofauti tuliyoitarajia pindi mtakaporejea kwenye majukumu yenu mtakuwa mmetuangusha sana sisi kama waratibu na wadau wetu waliofadhili mpango huu. Mafanikio yenu ndio yatakuwa chachu ya kuwashawishi wadau wengine zaidi wajitokeze kufadhili wataalamu wengine kwenye maeneo mengine ikiwemo suala zima la lishe ambalo tunalitazama kama mpango mpya’’ alitaja.
No comments:
Post a Comment