Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiwaongoza viongozi mbalimbali wakiwemo wa kitaifa na viongozi wa taasisi na mashirika mbalimbali walioshiriki kwenye mbio za km 5 za NBC Dodoma Marathon. |
Katika mbio hizo zilizohusisha washiriki kutoka ndani na nje ya nchi, ilishuhudiwa washiriki kutoka Tanzania, Kenya na Uganda wakichuana vikali kwa kuibuka washindi kwenye mbio tofauti hususani zile za km 10, km 21 na km 42. Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaongoza viongozi mbalimbali wakiwemo wa kitaifa na viongozi wa taasisi na mashirika mbalimbali walioshiriki kwenye mbio za km 5.
Akizungumza kwenye hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi na wadau mbalimbali wa mbio hizo, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa pamoja na kuipongeza benki ya NBC kwa mafanikio hayo, alionyesha kuguswa na ongezeko kubwa la washiriki wa mbio hizo kutoka washiriki 1,500 mwaka 2020 hadi kufikia washiriki 8,000 waliojiandikisha rasmi kushiriki mbio hizo mwaka huu. Hatua hiyo alisema inasadifu mwamko mkubwa wa wananchi kushiriki katika michezo hatua ambayo itasaidia katika kukabiliana na magonjwa yasiyoambukiza ikiwemo ugonjwa wa moyo, kisukari na figo.
“Mchango wa Benki ya NBC katika kuinua sekta ya michezo nchini upo wazi sana ambapo wametenga fedha zaidi ya bilioni 36 katika kufanikisha udhamini wa michezo mbalimbali ikiwemo mchezo wa mpira wa miguu. Kupitia mchezo huu wa riadha mbali na kuchochea mwamko wa mchezo husika kwa jamii, kwa mwaka huu pekee wamefanikiwa kukusanya fedha kiasi cha Shilingi milioni 300 zitakazoelekezwa kufanikisha juhudi mbalimbali za kiafya kupitia agenda ya msingi ya kuokoa maisha ya mama na mtoto…hongereni sana NBC,’’ alipongeza.
Alisema hatua ya benki hiyo, inaunga mkono jitihada za serikali kupitia azma ya Rais Samia Suluhu ya kuimarisha sekta ya afya nchini. Aliitoa wito kwa taasisi mbalimbali binafsi na zile za umma kuhakikisha wanabuni matukio mbalimbali ya kimichezo ili wayatumie kujenga afya za wananchi sambamba na kufanikisha agenda mbalimbali za kijamii.
Awali akizungumza kwenye hafla hiyo, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Bw Hamis Mwinjuma pamoja na kuipongeza benki hiyo kwa kuwa mdau mkubwa wa sekta ya michezo hapa nchini kupitia jitihada zake mbalimbali, alisema ukubwa wa mashindano hayo ya NBC Dodoma Marathon unatoa fursa kwa mamlaka zinazosimamia mchezo huo kutumia washindi mbalimbali waliopatikana kwenye mbio hizo kuliwakilisha taifa kwenye mashindani mbalimbali ya kimataifa yakiwemo mashindano ya Olympics na yale ya Jumuiya ya Madola (Commonwealth).
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Bw Theobald Sabi alisema kiasi cha mil 300 kilichokusanywa kupitia mbio kitaelekezwa katika kufanikisha malengo ya mbio hizo ambayo ni ukusanya fedha ili kusaidia mapambano dhidi ya saratani ya shingo ya kizazi kwa kushirikiana na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road pamoja na kutoa ufadhili wa elimu kwa wakunga kupitia Taasisi ya Benjamin Mkapa lengo kuu likiwa ni kuboresha afya ya mama wa mtoto.
“Zaidi pia sehemu ya fedha hii itaelekezwa katika kufanikisha ujenzi wa chumba cha upasuaji wagonjwa kwenye Hospitali ya Taifa ya Muhimbili. Mafanikio haya yanachochewa na dhamira yetu kama benki ya kuwa mstari wa mbele katika kusaidia jamii tunayoihudumia. Pia nawapongeza sana wadau mbalimbali waliojitokeza kufanikisha mbio hizo wakiwemo Kampuni ya Bima ya Sanlam ambao ni wadhamini wakuu wa mbio hizo sambamba na kampuni ya mawasiliano ya Vodacom waliodhamini mbio za km 21 pamoja na wadhamini wengine wote waliotuunga mkono,’’ alisema.
Katika mbio hizo ilishuhudiwa Mwanariadha kutoka Uganda Akanswa Mingichi akiibuka mshindi wa kwanza mbio za km 42 (Full Marathion) kwa upande wa wanaume baada ya kutumia muda wa saa 2 na dakika 13 akifuatiwa na Mwanariadha Eyenali Paul kutoka Kenya alietumia muda wa saa 2 na dakika 14 huku kwa upande wa wanawake mbio hizo ilishuhudiwa Mwanaridha Angelina Yumba akiibuka mshindi wa kwanza baada ya kutumia muda wa saa 2 na dakika 33 akifuatiwa na Chopsiriri Tufena kutoka Kenya alietumia muda wasaa 2 na dakika 34.
Washindi wa kwanza kwenye mbio hizo za km 42 waliondoka na zawadi ya fedha taslimu Tsh milioni 11.5 na vifaa vya michezo kwa jinsia zote huku washindi wa pili wakiondoka na Shilingi Milioni 5 na vifaa vya michezo kwa jinsia zote mbili.
Kwa upande wa mbio za km 21 wanaume ilishuhudiwa Mwanariadha kutoka Kenya Peter Mwangi akiibuka mshindi wa kwanza baada ya kutumia muda wa saa 1:02:23 akifuatiwa na Mwanariadha Joseph Panga kutoka Tanzania alietumia muda wa saa 1:02:35 huku kwa upande wa wanawake mbio hizo ilishuhudiwa Mwanaridha Sarah Makera akiibuka mshindi wa kwanza baada ya kutumia muda wa saa 2 na dakika 10 akifuatiwa na Suzana Chembui kutoka Kenya alietumia muda wa saa 1 na dakika 11.
Washindi wa kwanza kwenye mbio hizo za km 21 waliondoka na zawadi ya fedha taslimu Shilingi milioni 5.5 na vifaa vya michezo kwa jinsia zote huku washindi wa pili wakiondoka na shilingi 2.5 na vifaa vya michezo kwa jinsia zote mbili.
No comments:
Post a Comment