Dar es Salaam, 20 April 2024: Katika juhudi za kuboresha teknolojia za kidijitali katika sekta ya elimu, Benki ya Exim imezindua huduma ya 'Exim Smart Shule' maarufu kama 'Shule Kidijitali', suluhisho la malipo linalorahisisha malipo ya ada za shule moja kwa moja na wazazi, walezi, au wanafunzi wenyewe. Kupitia namba maalum inayotolewa na mfumo, malipo yanaweza kufanyika kwa urahisi kupitia matawi ya Exim Bank, Exim Wakala, na mitandao ya simu za mkononi. Mpango huu unalenga kurahisisha michakato ya malipo ya ada, kukuza ufanisi na upatikanaji wa huduma za malipo ya ada za shule.
Ramadhan Mbaga, Mkuu wa Kitengo cha Bidhaa za Kidijitali wa Exim Bank, anasema, “Kupitia Exim Smart Shule, wazazi na wanafunzi wanaweza kufanya malipo kwa urahisi kwa kutumia njia mbalimbali kama vile matawi yetu ya Benki ya Exim, Exim Wakala, na mitandao ya simu.”
Kutumia huduma hili pia kunaleta ufanisi kwa sababu kila namba ni ya kipekee kwa kila mwanafunzi kwendana na muamala wa malipo. Hii husaidia kuhakikisha kuwa malipo yanawekwa kwa usahihi katika akaunti ya mwanafunzi husika, kupunguza uwezekano wa kukosea namna ya kufanya malipo bila kuchanganya hesabu.
Matumizi ya Exim Smart Shule yanaweka uwazi katika mchakato wa malipo ya ada. Wazazi hupokea taarifa ya miamala ya malipo yao na kuthibitisha kuwa yamekamilishwa kwa mafanikio.
'Exim Smart Shule' inarahisisha malipo ya ada kwa wazazi, walezi, au wanafunzi kwa njia mbalimbali ikiwemo mtandao mkubwa wa matawi ya benki hiyo, mitandao ya simu za mkononi, na vituo vyake vya mawakala maarufu kama ‘Exim Wakala’ vilivyosambaa kote nchini. Urahisi huu unamuwezesha mhusika kufanya malipo kwa urahisi akiwa popote bila kuhitaji kufika kwenye shule.
Kifedha, mfumo huu ni salama na wa uhakika katika kufanya malipo ya ada kwa kutoa utambulisho maalum kwa kila muamala uliofanywa. Hii husaidia kupunguza uwezekano wa mtu kuingia kwenye akaunti ya mzazi bila idhini na uwezekano wa wizi.
Kupitia Smart Shule, wazazi na walezi watakuwa na uwezo wa kupata ripoti kuhusu watoto wao, kalenda ya mwaka ya shule, na mfumo wa kufuatilia usafiri wa wanafunzi. Aidha, wanafunzi watafaidika na maktaba iliyojaa vitabu vya kusoma ili kuwasaidia kufanya vizuri katika masomo yao.
“Kupitia huduma hili, Benki ya Exim inasaidia shule zilizojiunga na mfumo huu kutumia namba maalum kwa kila shule kwa ajili ya kufanya malipo. Hii inapunguza mzigo kwa utawala wa shule na kuhakikisha rekodi za shule ziko sawa,” anasema Elizabeth Mayengoh, Meneja wa Kanda kutoka Exim Bank.
'Exim Smart Shule' ni hatua muhimu katika kuelekea katika ufanyaji wa malipo ya ada za shule kidijitali, ikitoa urahisi, ufanisi, na usalama kwa wazazi, walezi, wanafunzi, na taasisi za elimu. Huduma hili bunifu inaonesha namna ambavyo Exim Bank inaamini katika ujumuishwaji wa kifedha kidijitali na mchango wake katika sekta ya elimu nchini. Ni Ushahidi mwingine wa kaulimbiu ya Exim Bank kuwa ‘Ubunifu ni maisha’.
No comments:
Post a Comment