Dar es Salaam - Desemba 11, 2023: Kupitia kampeni inayoendelea ya ‘Sambaza Shangwe, Gusa Maisha’ kampuni ya teknolojia na mawasiliano ya Vodacom Tanzania imekabidhi bima za afya kwa akina mama na watoto 600 wa hospitali za Rufaa za mikoa ya Mwananyamala, Amana na Temeke za jijini Dar es Salaam.
Akizungumza wakati wa tukio la makabidhiano ya bima kwa ajili ya akina mama na watoto katika hospitali ya Rufaa ya Mwananyamala, Mganga Mkuu wa Mkoa, Dkt. Zavery Benela amesema kuwa kampeni hii imekuja muda sahihi ambapo siku mbili zilizopita Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amesaini muswada Bima ya Afya kwa wote kuwa sheria kamili ambapo unalenga kuwezesha upatikanaji wa huduma za afya kwa Watanzania pasipo na kikwazo cha uchumi.
“Nipende kuwapongeza Vodacom kwa kampeni hii ya aina yake inayogusa afya za akina mama na watoto. Kundi hili hukumbwa na maradhi ya hapa na pale katika hatua za awali hivyo kuwa mzigo kwa watu wengi kumudu gharama za matibabu. Kwa msaada huu wa bima kubwa za afya kwa kipindi cha mwaka mmoja, hakika mmewasaidia na kuwapa fursa ya kujipanga kwa siku za usoni. Kwa namna ya kipekee kampeni hii inaendana na mipango ya serikali kwa sasa kuhakikisha kuwa Watanzania wote wanapata huduma za afya bila ya kuangalia kigezo cha uchumi,” alimalizia Dkt. Benela.
Kampeni ya ‘Sambaza Shangwe, Gusa Maisha’ ya Vodacom Tanzania ilizinduliwa mapema mwezi Novemba mwaka huu na inatarajiwa kudumu mpaka Januari 2024. Dhamira yake ni kuwazawadia wateja wake kwa kutumia huduma zao lakini pia kuwapatia zawadi ya upande hata wale ambao sio wateja wao. Jumla ya akina mama na watoto 2000 wanatarajiwa kunufaika nchini kote ambapo mpaka sasa mikoa ya Dodoma, Mbeya, na visiwani Zanzibar wameshanufaika tayari.
Mmojawapo wa akina mama aliyepokea bima ya afya pamoja na mtoto wake, Bi. Sharifa Abdallah ameelezea kuwa, “najisikia furaha na bahati iliyoje kupatiwa bima ya afya ya bure kwa mwaka mzima mimi pamoja na mtoto wangu. Nawashukuru Vodacom na wateja wao kwa kuona umuhimu wa kutukumbuka kwenye kampeni hii hususani kwa upande wa afya. Akina mama na watoto wetu tunakumbana na changamoto ya afya na maradhi ya hapa na pale baada ya kujifungua na kwa watoto wetu wachanga ambao kinga zao bado zinakuwa hazijaimarika. Msaada huu ni ahueni kubwa kwani mmetupunguzua gharama na kutuondelea wasiwasi kwa kipindi chote cha mwaka ujao.”
Akielezea dhamira ya kuwashirikisha zawadi ya upendo Watanzania katika msimu huu wa sikukuku, Kaimu Mkuu wa Kanda ya Dar es Salaam na Pwani wa Vodacom Tanzania PLC, Bw. Caleb Majo amemalizia kwa kusema kuwa, “matibabu ya afya kwa akina mama siku zote yana nafasi muhimu kwa Vodacom na ukizingatia kuwa huu ni msimu wa sikukuu ambao hujumuisha jamii na kujitolea, tumeona ni vema kutumia huduma yetu bunifu ya kidigitali ya bima ijulikanayo kama Vodabima ili kusambaza shangwe na kugusa maisha ya akina mama na watoto wao kwasababu changamoto za kiafya hazichagui mtu”.
“Hii pia inaendana na kujizatiti kwetu katika kuunga mkono serikali kuhakikisha kwamba Watanzania wanapata huduma bora bila ya kuzingatia hali ya yao ya vipato au wanapatikana wapi. Kupitia kampeni hii, hatutarajii kuongeza hamasa juu ya umuhimu wa huduma ya bima ya afya pekee bali pia kuonyesha kwamba bima ya afya ni kwa ajili ya kila mtu na sio kwa wenye vipato vya juu wachache pekee kama watu wengi wanavyoamini,” alimalizia Bw. Majo.
No comments:
Post a Comment