Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Nchemba amepokea gawio kubwa zaidi kupata kutolewa na taasisi ya kifedha la shilingi bilioni 45.8 linalotokana na uwekezaji wa Serikali ndani ya Benki ya CRDB kutoka kwa Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Benki ya CRDB, Dkt. Ally Laay.
Makabidhiano hayo ya hundi kifani yalifanyika katika Makao Makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Dkt. Natu El- Maamry Mwamba pamoja na viongozi mbalimbali wa taasisi na mashirika ya umma yenye hisa ndani ya Benki ya CRDB.
“Ongezeko hili la gawio ni kiashiria tosha kwa Serikali kuwa Benki yetu ya CRDB inazidi kuimarika zaidi kutokana na mikakati madhubuti ya kibiashara iliyojiwekea na jambo linalowapa moyo Watanzania na wawekezaji kuwa benki inatoa huduma bora katika jamii”, alisema Dkt. Nchemba.
Dkt. Nchemba alisema fedha zilizopatikana kupitia gawio hilo zitakwenda kusaidia utekelezaji wa miradi ambayo Serikali imeianisha katika vipaumbele vya bajeti ya mwaka 2023/2024. “Kipekee kabisa niipongeze Bodi, Menejimenti na Wafanyakazi wote wa Benki ya CRDB kwa kazi nzuri mnayoifanya,” aliongezea Dkt. Nchemba.
Akielezea namna ambavyo Serikali inaridhishwa na umahiri wa Benki ya CRDB katika kufanya biashara kiushindani, Dkt. Nchemba aliipongeza Benki hiyo kwa kupanua wigo wake kwa kuanzisha kampuni tanzu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kampuni tanzu ya CRDB Insurance Co. Ltd, pamoja na taasisi ya CRDB Bank Foundation ambayo imeonyesha kuwa mstari wa mbele katika kuchochea ujumuishi wa kiuchumi kupitia programu ya IMBEJU.
Aidha, Dkt. Nchemba aliihakikishia Benki ya CRDB na wadau wengine wa maendeleo nchini kuwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan itaendelea kuimarisha na kuweka mazingira rafiki na endelevu ya kufanya biashara katika sekta ya fedha na sekta nyinginezo ili kuwavutia wawekezaji wa ndani na nje.
Dkt. Nchemba alisema Serikali ina mpango wa kuja na programu kabambe ambayo itasaidia kuboresha sekta binafsi na kupunguza mikopo chechefu nchini. Pia alisisitiza juu ya weledi wa wafanyakazi wa mabenki katika utoaji wa mikopo kwa kuhakikisha fedha zinazokopeshwa zinakwenda kwenye miradi au biashara endelevu.
“Katika Mkutano wa Wanahisa uliofanyika katika Kituo cha Kimataifa cha Mikutano Arusha (AICC) mwezi Mei mwaka huu, Wanahisa wa Benki ya CRDB walipitisha kwa pamoja gawio la shilingi 45 kwa hisa ikiwa ni ongezeko la asilimia 25 na hivyo kufanya jumla ya gawio la mwaka huu kufikia shilingi bilioni 117.5,” alisema Dkt. Laay.
Nsekela alisema katika kipindi hicho Benki ya CRDB imepata mafanikio makubwa ya kiutendaji yaliyopelekea benki hiyo kuwa na mchango mkubwa katika kusaidia jitihada za maendeleo nchini. Nsekela alibainisha kuwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita benki hiyo imelipa jumla ya kodi ya Shilingi trilioni 1.1 kwa serikali.
“Katika kipindi cha miaka mitano pia tumeweza kuongeza ajira zaidi ya 600 nchini, tukitumia zaidi ya Shilingi trilioni 1.3 kulipa mishahara na marupurupu, tumefanya kazi na wazabuni zaidi ya 1,000 na kulipa zaidi Shilingi bilioni 625,” alisema Nsekela huku akibainisha benki hiyo imetumia zaidi ya Shilingi bilioni 14 katika miradi ya kijamii kupitia sera yake ya uwekezaji kwa jamii.
Pamoja na kukabidhi gawio kwa Serikali kuu kupitia mfuko wa uwekezaji wa DANIDA, Benki ya CRDB pia imekabidhi gawio kwa taasisi na mashirika mbalimbali ya Serikali ikiwamo PSSSF, NSSF, ZSSF, NHIF, Local Government Loans Board, Chama cha Ushirika cha Wakulima wa Tumbaku Kanda ya Magharibi (WETCU), Umoja Unit Trust Scheme, pamoja na halmashauri Mbinga, Shinyanga, Mufindi, Chunya na Rungwe.
No comments:
Post a Comment