Dar es Salaam – May 18, 2023 - Taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation na USAID zimesaini mkataba wa makubaliano ili kuunga mkono utekelezaji wa afya ya uzazi na mfumo wa usafiri wa dharura Tanzania kupitia mpango wa serikali wa m-mama.
Hatua hii inakuja baada ya serikali ya Tanzania kupitia Makamu wa Rais, Mheshimiwa Dkt. Philip Mpango kutoa wito wakati wa Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mwaka jana wa kushirikiana ili kupanua mpango wa m-mama nchini kote. USAID iliahidi kuchangia dola za Marekani 5 milioni (takribani TZS 12 bilioni) ambazo zitajumuishwa na fedha ambazo Vodacom iliahidi kutoa awali, kiasi cha dola za Marekani 10 milioni (takribani TZS 23.5 bilioni) kwa serikali.
Kwa upande wa serikali, mbali na kuendesha na kumiliki kikamilifu mfumo mzima, pia imejidhatiti kugharamia gharama zote za usafiri na rasilimali watu kwenye vituo vya mawasiliano tangu kuanza kwa mfumo huu. Jitihada hizi za pamoja zitasaidia upatikanaji wa mfumo wa m-mama nchini kote na hivyo kuwafikia Watanzania zaidi ya milioni 60.
“Tunashukuru ushirikiano wa USAID na Vodacom Tanzania Foundation wa kuimarisha utekelezaji wa m-mama nchini kote. Ushirikiano baina ya sekta za umma na binafsi una umuhimu mkubwa katika kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya huduma ya afya, kwa hakika tunaamini kuunganisha rasilimali na utaalamu wetu, tutaongeza kasi kuelekea ufanikishaji wa Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDG) hususani kwenye afya, tukihakikisha hakuna mama anayeachwa nyuma,” alisema Waziri wa Afya wa Zanzibar, Mh. Nassor Ahmed Mazrui.
Akizungumza wakati wa hafla ya utiaji saini, Kate Somvongsiri, Mkurugenzi wa Ujumbe wa Marekani kutoka USAID amesema, “ushirikiano huu, na mpango wa m-mama unawawezeshawa wanawake kuwa na maisha yenye afya bora, manufaa yake yatakuwa makubwa na kuongezeka zaidi, kama akina mama, wasichana, na Watoto wachanga watanufaika na ufumbuzi wa kipekee kwa changamoto iliyokuwa inawakabili.”
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Vodacom Tanzania Foundation, Bi. Zuweina Farah amesisitiza kwenye umuhimu wa ushirikiano baina ya sekta binafsi na za umma katika kufanikisha Malengo Endelevu ya Maendeleo (SDG) hususani yanayolenga kwenye afya na kubainisha teknolojia na ubunifu kuwa ni chachu ya ufumbuzi wa mabadiliko.
“Mfumo wa m-mama ni ushuhuda wa jukumu letu la kuwaunganisha Watanzania kwa manufaa, tukitumia ubunifu wetu wa kidigitali na kiteknolojia huku tukiainisha changamoto halisi zinazo zikumba jamii za Kitanzania. Afya ya uzazi inabakia kuwa changamoto ya dunia nzima, na ufumbuzi wa kidigitali unahitajika ili kuhakikisha usalama na ufanisi wa usafiri wa dharura kwa wanawake wenye uhitaji. Kupitia ushirikiano wetu na USAID, tunalenga kuacha alama ya kudumu katika huduma ya afya ya uzazi nchini kwa kutumia nguvu ya teknolojia na ubunifu,” alisema.
Tanzania ina kiwango kikubwa cha idadi ya vifo vinavyotokana na uzazi, hususani kwa maeneo ya vijijini ambapo upatikanaji wa huduma ya usafiri wa dharura uwiano wake ni 1 kati ya 10. Ushirikiano baina ya serikali, Vodacom Tanzania Foundation na washirika wengine wa maendeleo kama vile Pathfinder na Touch Foundation kati ya mwaka 2013 na 2021 ulifanikiwa kuanzisha m-mama, mfumo endelevu unaoweza kufanyiwa maboresho ili kupunguza vifo vya uzazi na Watoto wachanga nchini Tanzania. Mfumo huu ulianza kufanyiwa majaribio na kuboreshwa katika wilaya za Sengerema/Buchosa na mkoa wa Shinyanga ambapo kwa wakati ulifanikiwa kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi kwa asilimia 38 katika mkoa wa Shinyanga pekee.
Sasa m-mama inapatikana kupitia namba ya bure (115) inayopatikana katika mitandao yote kwenye mikoa 13 ya Tanzania bara na mitano ya Visiwani Zanzibar. Na mpaka sasa zaidi ya akina mama 21,800 na Watoto wachanga wamesafirishwa kupitia mfumo huu, ambapo takribani Maisha 722 yameokolewa.
Zoezi la leo la utiaji saini linadhihirisha jitihada za pamoja za kuelezea suala muhimu la afya ya uzazi, kusisitiza umuhimu wa ushirikiano baina ya sekta moja na nyingine katika kuleta mabadiliko chanya. Washirika kwa pamoja wamezitaka sekta binafsi, asasi za kiraia na mashirika ya maendeleo kujenga ufumbuzi endelevu miongoni mwao ambao utaacha alama ya matokeo ya muda mrefu kwenye huduma za afya duniani.
Kuhusu Vodacom Tanzania Foundation
Vodacom Tanzania Foundation ni sehemu ya Vodacom Tanzania PLC iliyojikita katika miradi ya kusaidia jamii kwa kutimiza wajibu wake wa kuunufaisha umma hususani makubdi yasiyojiweza hususani wanawake na vijana. Taasisi inajumuisha misaada ya kijamii kwa kutumia teknolojia ya mawasiliano ya simu za mkononi kutoa ufumbuzi kwa changamoto mbalimbali za kijamii.
Kwa kufanya kazi na taasisi za ndani zisizo za kiserikali na washirika, mpaka sasa taasisi ya Vodacom Tanzania Foundation imeunga mkono zaidi ya miradi 120 kwa kuwekeza zaidi ya TZS 15 bilioni kuboresha Maisha ya Watanzania.
No comments:
Post a Comment