Kitomari Banking & Finance Blog is a premier site for banking, finance, business, economic, investment and stock market news as well as selected informative articles from Tanzania, East Africa and the rest of the World. We operate 24 hours a day, 365 days a year with complete context, perspective and precision.
Monday 13 March 2023
VODACOM YAJENGA MINARA 227 YA MTANDAO WA 5G NCHINI
Dar es Salaam – Machi 10, 2023: Katika kufanikisha adhma yake ya kuwaunganisha watanzania na teknolojia ya mawasiliano na kuboresha maisha yao kupitia huduma zenye ubunifu za kidigitali, kampuni ya Vodacom Tanzania Plc imebainisha kuwa mpaka sasa imejenga minara 227 ya mawasiliano ya 5G iliyosambaa katika mikoa mbali mbali nchini.
Taarifa hiyo ilitolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Plc, Philip Besiimire alipozungumza na wateja kwa mara ya kwanza kupitia programu ya ‘VODA CHAT’ iliyofanyika kwa njia ya Twitter Spaces ambapo mada kuu iliyozungumziwa ni kuhusu ufanisi wa mtandao pamoja na huduma mpya ya 5G iliyotambulishwa mwezi Septemba mwaka jana kwa mara ya kwanza kabisa nchini Tanzania.
“Teknolojia inakua, awali tulikuwa tunasambaza huduma za 2G, tukaenda 3G na 4G na mpaka sasa tupo 5G. Lakini pia kuna fununu kuwa kuna sehemu zingine duniani tayari wameshaanza na tafiti za kuhamia 6G – teknolojia itaendelea kubadilika. Kinachofanyika ni kuendelea kuiboresha minara iliyopo ili kuwa na uwezo wa kubeba teknolojia mpya. Pia watengenezaji wa mitambo ya redio kunasa mawimbi ya mawasiliano wanatengeneza vifaa ambavyo vitabeba teknolojia zilizopo kwa pamoja. Kwa ufupi, teknolojia zote zitaendelea kuwepo kwasababu bado tunao Watanzania wengi wanaotumia mtandao wa 2G, wengine wengi pia wanahamia 3G na 4G. Changamoto inayokuja ni gharama za simu janja zinazowezesha kutumia teknolojia mpya kama vile 4G na 5G ambazo bado ni kubwa,” alifafanua Philip
“Hivyo tutaendelea kuwa na wateja wa 5G na 4G vilevile wa 3G na 2G, jukumu letu kubwa kwa sasa ni kuendelea kuwashawishi wateja kuhamia kwenye teknolojia mpya wanufaike na huduma bora zenye faida nyingi zaidi. Pia, kufanya jitihada za kuhakikisha wateja wanapata simu janja kwa bei nafuu na kuendelea kuwekeza zaidi kupanua mtandao wetu. Kama mnavyojua Tanzania ni nchi kubwa yenye idadi ya watu inayoongezeka kila siku ambapo idadi kubwa ni vijana ambao kadri wanavyokuwa watahitaji kutumia huduma zetu na kadri wanavyoongezeka ndivyo itatupasa nasi kuongeza uwekezaji. Bado tuna mambo kadhaa ya kuyafanyia kazi kama vile kuzidi kuboresha miundombinu ili kuhakikisha huduma zetu zinakuwa na ufanisi ipasavyo,” aliendelea Philip
Akifafanua aina ya teknolojia ya 5G ambayo Vodacom Tanzania inaitumia nchini, Mkurugenzi wa Mtandao wa kampuni hiyo, Andrew Lupembe alisema, “Tumezindua huduma ya 5G kwenye wigo wa aina mbili – ya kwanza ni ya 3500 mghz ambayo ni maarufu na inatumiwa sehemu nyingi duniani na hivi karibuni tumepata masafa mengine kutoka TCRA yenye uwezo wa 2300 mghz.”
Kwa kuongezea kwenye wigo wa huduma zake, Mkurugenzi wa Kitengo cha Biashara wa Vodacom Tanzania, Linda Riwa alisema kuwa, “mpaka sasa idadi ya wateja wetu ambao wana simujanja inakaribia 30 - 40%, hii inamaanisha takribani 60% ya wateja wetu hawatumii simujanja - kati ya wateja milioni 17 tulionao. Changamoto kubwa ni gharama kubwa ya simu janja ukilinganisha na vifaa vya 2G. Tunafanya jitihada kadhaa kulitatua hili kama vile kupunguza gharama za simu kama vile tulivyotambulisha simu ya smatikitochi iliyokuwa inauzwa Tsh. 100,000/- lakini sasa inapatikana kwa Tsh. 55,000. Lakini pia kupitia kushirikiana na wauza vifaa hivyo ambapo tunawasaidia kuwaunganisha na vifurushi vya bure vya intaneti kila mwezi kwa mwaka ili kuwapatia unafuu. Mipango ni mingi, mwaka huu tutawekeza zaidi na kujaribu kushusha zaidi bei ili Watanzania wamiliki zaidi simu janja. Moja ya mikakati yetu ni kutambulisha mfumo wa kulipia kidogo kidogo pia.”
Akitoa mtazamo wake kuhusu mustakabali wa Tanzania na fursa zinazopatikana kupitia mazungumzo kwenye mjadala huo, Mkurugenzi Mkuu wa Vodacom Tanzania Plc alimalizia kwa kusema, “kupitia maongezi haya nimejifunza mambo manne ambayo ni shauku ya Watanzania kuunganishwa na mawasiliano nchini kote, kuelewa zaidi namna mtandao wa 5G unavyofanya kazi, upatikanaji wa bidhaa nafuu za kiteknolojia za mawasiliano, pamoja na huduma jumuishi za kijami kama vile fedha, elimu, kilimo, afya, benki, nakdhalika. Niwaahidi kuwa Vodacom itaendelea kuwa wabunifu katika huduma zetu, kuongeza ushirikiano wetu na serikali na wadau wengine lakini pia kukaribisha ushindani zaidi ili Watanzania wanufaike zaidi.”
Kwa kuhitimisha jukwaa hilo la Twitter Spaces, Kaimu Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Vodacom Tanzania Plc, Annette Kanora alisema, “nawashukuru wateja na wasikilizaji kwa kujiunga nasi kutokea maeneo mbalimbali kwenye mjadala huu ambao tumeuendesha kwa mara ya kwanza kupitia mtandao wa kijamii. Kutokana na mafanikio ya tukio letu la leo pamoja na shauku kubwa iliyoonyeshwa, tutaandaa jukwaa lingine likiwa na wazungumzaji mbalimbali kujadili mada tofauti na tutawajulisha lini litafanyika. Vile vile tutaweka utaratibu wa wateja kuchagua mada ambayo wangependa ijadiliwe na kuipigia kura kupitia kurasa zetu tofauti ya mitandao ya kijamii.”
Program hii mpya ambayo inalenga kuwakutanisha watendaji wa kampuni kuzungumza na wateja wao kuhusu masuala mbalimbali yanayowagusa ilifanyika siku ya Jumanne ya Machi 7 kuanzia saa 11 jioni mpaka saa 12 jioni ambapo mpaka sasa mazungumzo hayo yametembelewa na wasikilizaji zaidi ya 2,800.
Kama ulipitwa na mazungumzo hayo unaweza kuyasikiliza tena kupitia hapa:#
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment