Dodoma – Kampuni ya Vodacom Tanzania imezindua duka kubwa jipya la mfano (flagship store) jijini Dodoma, hatua inayolenga kusogeza huduma bora zaidi kwa wateja wa mkoa huo pamoja na mikoa mingine ya Kanda ya Kati.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa duka hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania, Bw. Philip Besiimire, amesema duka hilo ni mkombozi kwa wakazi wa Dodoma na maeneo jirani kutokana na kuboreshwa kwa huduma mbalimbali, zikiwemo huduma maalumu kwa wateja wenye mahitaji maalumu. Ameeleza kuwa kwa mara ya kwanza, duka hilo limezingatia kikamilifu upatikanaji wa huduma kwa makundi mbalimbali ikiwemo viziwi, watu wenye ulemavu wa miguu, macho na wengineo, huduma ambazo hapo awali hazikuwepo kwa kiwango hicho.
Bw. Besiimire ameongeza kuwa uzinduzi wa duka hilo unaakisi dhamira ya Vodacom Tanzania ya kuendelea kuwekeza katika miundombinu na uzoefu wa wateja, sambamba na mahitaji yanayobadilika ya wateja wake, hususan katika miji inayokua kwa kasi kama Dodoma.
Kwa upande wao, wateja wa Vodacom wameipongeza kampuni hiyo kwa hatua hiyo, wakieleza kuwa duka jipya litawawezesha kupata huduma kwa urahisi na ufanisi zaidi. Wamesema kuwa ukubwa wa duka hilo na mpangilio wake wa kisasa, ukilinganisha na duka la awali, umeongeza faraja na kuboresha kwa kiasi kikubwa uzoefu wao wa kupata huduma.
Uzinduzi wa duka hilo kubwa la mfano Dodoma ni sehemu ya mkakati mpana wa Vodacom Tanzania wa kuimarisha huduma kwa wateja, kuongeza ujumuishi, na kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika maeneo mbalimbali nchini.



.jpeg)


No comments:
Post a Comment