Mafuru ametoa pongezi hizo wakati wa uzinduzi wa mafunzo ya utekelezaji wa akaunti hiyo kwa Wakurugenzi Watendaji na Maafisa Wakuu wa Fedha wa makampuni ya bima nchini yaliyofanyika katika Makao Makuu ya Benki ya CRDB jijini Dar es Salaam.
Mafuru amesema uanzishwaji wa Akaunti hiyo ya Dhamana ya Bima ni hatua nzuri ambayo itasaidia kuimarisha usimamizi wa sekta ya bima kuendana na matakwa ya kisheria na udhibiti yaliyowekwa na TIRA.
Amesema kuwa kampuni nyingi za bima zilikuwa zikitumia fedha za amana ya Akiba katika matumizi mengine, pasipo kupata idhini ya TIRA hivyo kupelekea kuingia katika changamoto ya ukwasi, na wakati mwengine kushindwa kulipa fidia kwa wateja kutokana na fedha kuwekezwa katika miradi mingine.
Mafuru alibainisha kuwa uamuzi wa kufungua Akaunti ya Dhamana ya Bima katika benki za biashara ni mwarobaini wa changamoto hiyo, kwani sasa TIRA itaweza kusimamia moja kwa moja fedha hizo za amana za akiba, jambo ambalo si tu litaimarisha usimamizi, bali pia kuboresha maendeleo ya sekta ya fedha.
Aidha, Mafuru alimtaka Kamishina wa TIRA kuhakikisha kampuni zote za bima zinafuata sheria kwa kuweka dhamana ya amana. Alisema kwa kufanya hivyo kutasaidia kuchochea mafanikio ya sekta ndogo ya bima kama ilivyoanishwa katika Mpango wa Taifa wa miaka 10 wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Nchini ‘Financial Sector Development Master Plan’.
Dkt. Saqware amesema mwaka jana Mamlaka kwa kushirikiana Chama cha Watoa Huduma za Bima (ATI), walikubaliana kuandaa Mwongozo wa Uwekazaji wa Usimamizi wa Ukwasi ambao pia ulielekeza uanzishwaji wa Akaunti ya Dhamana ya Akiba kupitia benki za biashara ili kuondokana na tatizo la changamoto ya kimtaji au kushindwa kulipa fidia za madai ya wateja wake.
Akitoa taarifa za utendaji wa sekta ya bima, Dkt. Saqware alimjulisha Naibu Katibu Mkuu kuwa sekta hiyo imeendelea kukua kulinganisha na miaka iliyopita. Amesema mwaka jana mauzo ya bima yaliongezeka kwa asilimia 25 kufikia Shilingi Trilioni 1.146 kulinganisha na mauzo ya 2021. Aidha, alibainisha kuwa malengo ya mwaka huu ni kufikia Shilingi Trilioni 1.5.
Nsekela Akaunti ya Dhamana ya Bima iliyofunguliwa Benki ya CRDB imezingatia kwa asilimia mia moja mapendekezo ya TIRA na wadau wa sekta ya bima, huku akibainisha kuwa akaunti hiyo imeunganishwa na mifumo ya kidijitali itakayosaidia katika usimamizi na utoaji wa taarifa kwa Mamlaka na kampuni za bima.
Nsekela alimuhakikishia Naibu Katibu Mkuu kuwa Benki ya CRDB itaendelea kushirikiana na TIRA na wadau wa sekta ya bima kusaidia Kuboresha sekta hiyo. Nsekela alisema Benki hiyo imekuwa kinara katika utoaji wa huduma za bima kupitia mfumo wa BancAssuarance, huku akibainisha kuwa imekuwa ikitoa huduma hizo katika matawi yake, CRDB Wakala, na kidijitali kupitia SimBanking.
No comments:
Post a Comment