Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amekutana na kufanya mazungumzo na Mabalozi wawili, Balozi wa Canada na Japan kwa nyakati tofauti ambapo walizungumzia ushirikiano kati ya nchi hizo katika sekta mbalimbali za uzalishaji ikiwemo sekta ya kilimo, mifugo, uvuvi, na sekta binafsi ili kukuza uchumi.
Mazungumzo hayo yamefanya kwenye Ofisi Ndogo za Wizara ya Fedha na Mipango jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na Balozi wa Canada, Mhe. Kyle Nunas, Dkt. Nchemba aliishukuru Serikali ya Canada kwa kutoa fedha kiasi cha dola ya Canada milioni 87.3 kwa ajili ya Mfuko wa Afya na ahadi mpya ya kutoa dola za Canada milioni 75 katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2026, ambazo amesema zitasaidia kuboresha afya ya jamii.
Aidha, Dkt. Nchemba aliipongeza Canada kwa kuahidi kutoa kiasi kingine cha dola za Canada milioni 32 katika mwaka wa fedha 2023/2024 kwa ajili kuendeleza sekta binafsi ambayo ni muhimu katika maendeleo ya nchi na ni injini ya kukuza uchumi.
Alisema kuwa Tanzania imeweka mazingira mazuri ya uwekezaji na kutoa wito kwa wamekezaji kutoka Canada kutumia fursa za masoko ya uhakika yanayopatikana nchini na katika nchi zinazopakana na Tanzania pamoja na uwepo wa idadi kubwa ya wateja ambao watakuwa ni soko la bidhaa zao.
Kwa upande wake Balozi wa Canada hapa nchini, Mhe. Kyle Nunas, aliipongeza Tanzania inayoongozwa na Rais Mhe. Dkt. Samia Suluhu Haasan kwa kusimamia uchumi wa nchi kwa ushupavu mkubwa licha ya kuwepo na changamoto mbalimbali zilizoikumbuka dunia ikiwemo covid – 19 na vita ya Urusi na Ukraine.
Alisema nchi yake iko tayari kuendelea kushirikiana na Serikali kupitia program mbalimbali za maendeleo zinazofanya na nchi hizo mbili ili kuharakisha maendeleo ya nchi na wananchi wake.
Katika hatua nyingine alipokutana na Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yaushi Misawa, Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, alimwomba Balozi huyo kuainisha na kuweka utaratibu namna Tanzania itakavyonufaika na dola za Marekani bilioni 30 ambazo Japan imeahidi kuzisaidia nchi za Afrika kuimarisha uchumi wake.
Aidha, alimweleza Balozi huyo kuwa Tanzania inasubiri kwa hamu majibu ya nchi hiyo katika kufadhili miradi 8 ya kimkakati ambayo Serikali imewasilisha kwa Serikali ya Japan ili miradi iliyokusudiwa ambayo iko katika sekta mbalimbali iweze kuchochea maendeleo ya nchi na kuboresha huduma za jamii.
Dkt. Nchemba alisema kuwa Tanzania imeendelea kuwekeza rasilimali fedha kwenye maeneo yenye kukuza uzalishaji kama kilimo, uvuvi, miundiombinu ya usafirishaji na kuboresha mazingira ya uwekezaji ili kukuza ajira, uzalishaji wa bidhaa za kilimo ili kuweza kulisha nchi za kiafrika na nchi nyingine kwa kuwa Tanzania ni ghala la chakula.
Akijibu hoja zilizwekwa mezani na Serikali, Balozi wa Japan nchini Tanzania Mhe. Yaushi Misawa, aliihakikishia Tanzania kuwa itakuwa ni sehemu ya nchi zitakazonufaika na mpango uliotangazwa na Uongozi wa nchi hiyo wa dola za Marekani bilioni 30 kwa ajili ya kuzisaidia nchi za Afrika kufufua uchumi wao ulioathiriwa zaidi na UVIKO 19, ukame pamoja na vita vinavyoendelea baina ya Urusi na Ukraine.
Balozi Mhe. Misawa, aliwapongeza Rais wa Tanzania Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan na Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, kwa umahili wao wa kusimamia masuala ya uchumi na kuiwezesha nchi kung’ara na kuwa na kiwango cha juu cha ukuaji wa uchumi licha ya majanga yanayoikabili dunia hivi sasa.
Mkutano huo umehudhuriwa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Dkt. Natu El- Maamry Mwamba na Kamishna wa Fedha za Nje wa Wizara hiyo, Bw. Rished Bade.
No comments:
Post a Comment