Foreign Exchange Rates

DStv Advert_090724

DStv Advert_090724

SBT Tanzania Advert_291123

Thursday, 1 December 2022

WADAU KUWEZESHA WANAWAKE KUJIKWAMUA BAADA YA JANGA LA UVIKO-19

Katika picha, kutoka kushoto ni Aziza Ibrahim mwakilishi kutoka Hekima Consultants, katikati ni Marion Elias - Mkurugenzi katika kampuni ya Ekima Consultants na anayefuatia upande wa kulia ni Ernestina Mwenda - Mkurugenzi wa kampuni ya Active Mama wakati wa mkutano na waandishi wa habari uliofanyika tarehe 30 Novemba 2022 jijini Dar es Salaam kuzungumzia tamasha la Mama’s Day Out linalotarajia kufanyika 9 Disemba 2022 lenye kauli mbiu ya “Anza Upya” likiwa na lengo la kumwezesha mwanamke kujikwamua na changamoto mbali mbali za kiuchumi na kijamii.

30 Novemba 2022, Dar es Salaam - Wakati dunia ikiadhimisha Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia Duniani, kampuni ya Ekima Consultants na wadau wa maendeleo wameandaa tamasha la wanawake lenye lengo la kuwawezesha, na kuwahamasisha wanawake kujikwamua na changamoto baada ya janga la Uviko-19.

Tamasha hilo lenye kauli mbiu ya ‘Anza Upya’ linalotarajiwa kufanyika tarehe 9 Desemba jijini Dar es Salaam lina lengo la kukuza uwezo wao katika kuchangia maendeleo endelevu. Mada zitakazotolewa kwenye tamasha hilo zitaangazia afya ya akili, ustawi, uwezeshaji wa kifedha na kiuchumi, kujijali, na afya ya wanawake; ambazo zitatolewa na wataalamu kutoka sekta ya afya, taasisi za kifedha, mashirika na makampuni binafsi.

Akizungumza katika mkutano na waandishi wa habari, muandaaji wa tamasha hilo, Mkurugenzi wa EKIMA Consultants Marion Elias alisema kuwa tamasha linawalenga wanawake walioajiriwa na waliojiajiri wenye umri kuanzia miaka 25 hadi 65

Kama sehemu yao ya kushiriki kwenye kampeni ya Siku 16 za Kupinga Ukatili wa Kijinsia Duniani, tamasha hili litakuwa na mada zitakazomwezesha mwanamke kutambua viashiria vya ukatili wa kijinsia au kiuchumi na kumwezesha kuchukua hatua ili kujilinda yeye na jamii kwa ujumla.

“Moja ya vikwazo vinavyowakabili wanawake ni ukatili wa kiuchumi na masuala ya usimamizi wa fedha, na tunalenga kutatua baadhi ya changamoto zinazodhoofisha ukuaji wao kiuchumi ikiwemo mipango ya kujiwekea akiba, ukosefu wa huduma za kifedha kama vile huduma za kibenki na mikopo, mipango duni ya uwekezaji, mgawanyo mbaya wa rasilimali, nk.”, alisema Marion.

Akiendelea kuelezea tamasha hilo, Marion alisema kuwa sambamba na mafunzo, washiriki watajengewa uwezo na kuhamasishwa katika mambo mbalimbali ikiwemo kutumia ujuzi, uvumbuzi na ubunifu ili kukuza biashara na taaluma zao na kutimiza malengo waliyojiwekea.

“Tunataka kuona maendeleo ya kudumu, ya kweli na yenye faida; yatakayomwezesha mwanamke kujiendeleza, kujisimamia na kuweza kupiga hatua katika maisha.” alisema Marion.

Naye Ernestina Mwenda, Mwanzilishi na Mkurugenzi wa kampuni ya ‘Active Mama’ inayojihusisha na masuala ya mama na mtoto ameelezea changamoto zinazowakabili wakinamama baada ya uzazi, ikiwemo kushindwa kuendelea na ajira na kuelezea kuwa wanatarajia kuhamasisha wanawake kutafuta mbinu mbadala za kujiendelea kiuchumi baada ya kujifungua.

Marion, alihimiza makampuni na mashirika mbalimbali kutumia tamasha kama fursa ya kuwazawadia wafanyakazi na wateja wao kwa kuwawezesha kushiriki kwenye tamasha hilo linalotarajiwa kukutanisha wanawake zaidi ya 200 kutoka mikoa mbalimbali na limedhaminiwa na kampuni ya Sukari ya Kilombero kupitia chapa yake ya Bwana Sukari, Azam Media, Watu Konekt, Active Mama, The Marz, Renex, Life is Food, na Timeless Ltd.

No comments:

Post a Comment