Dar es Salaam: Novemba 26, 2022 - Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) ambae ni mdhamini Mkuu wa Ligi Kuu ya Soka ya Tanzania Bara, NBC Premiere League jana ilikabidhi zawadi ya pesa na tuzo kwa mchezaji bora wa ligi hiyo wa mwezi Oktoba, Sixtus Sabilo kutoka Mbeya City SC pamoja na kocha bora wa mwezi huo, Nasreddine Nabi kutoka klabu ya Yanga.
Makabidhiano ya zawadi hizo yalifanyika muda mfupi kabla ya kuanza kwa mchezo baina ya Yanga SC dhidi ya Mbeya City FC uliofanyika katika Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam, mchezo ambao ulikamilika kwa timu ya Yanga SC kuibuka na ushindi wa goli 2 kwa sifuri. Magoli ya Yanga yalifungwa na mshambuliaji wa timu hiyo Fiston Mayele.
Katika tukio la makabidhiano ya zawadi hizo, ilishuhudiwa Mkurugenzi wa Biashara wa Benki ya NBC, Elvis Ndunguru akikabidhi mfano wa hundi ya pesa yenye thamani ya Tsh milioni 1 kwa kocha Mkuu wa Yanga Nasreddine Nabi pamoja na tuzo sambamba na king’amuzi cha Azam huku pia mchezaji Sixtus Sabilo kutoka Mbeya City SC akipatiwa mfano wa hundi yenye kiasi kama hicho cha pesa, tuzo na kingamuzi cha Azam.
“Kimsingi ni kwamba sisi kama wadhamini wa ligi hii tunaendelea kujivunia sana kuona ligi yenye ushindani na viwango bora vya kiuchezaji vinavyoendelea kuonekana kwenye ligi hii. Ndio maana utaona kwamba pamoja na ligi kuwa na wachezaji wengi wa kigeni bado wachezaji wazawa wanapambana na kufanya vizuri na wanachukua tuzo hizi. Huu ni uthibitisho kwamba vilabu vyote kwasasa vinaweza kuhudumia vyema wachezaji wake kiasi cha kuweza kutoa ushindani unaotakiwa,’’ alisema.
Kwa mujibu wa Bw Ndunguru, benki hiyo inaendelea na mikakati mbalimbali kuhakikisha timu hizo zinanufaika zaidi na udhamini wa benki hiyo kwenye ligi hiyo ambayo hadi sasa imetoa ajira na kipato kwa watu zaidi ya 12,000.
Aliitaja mikakati mbalimbali ikiwemo mikopo ya mabasi kwa vilabu mbalimbali vinavyoshiriki ligi hiyo ili kurahisha usafiri kwa vilabu hivyo, mpango ambao upo kwenye hatua za mwisho za utekelezwaji.
“Na jitihada zetu hizi haziishii kwenye mchezo wa soka tu bali pia michezo mingine ikiwemo golf na mchezo wa riadha ambapo kupitia NBC Dodoma Marathon inayofanyika kila mwaka jijini Dodoma tumekuwa tukikusanya fedha kwa ajili ya elimu na matibabu ya saratani ya shingo ya kizazi changamoto ambayo inachangia kwa kiasi kikubwa vifo vya kina mama.’’
“Kupitia jitihada hizo hadi sasa zaidi ya Wanawake 9,000 wamefanya vipimo na kati yao 500 wamegundulika kuwa na saratani hiyo na wameshaanza matibabu kwa kushirikiana na Taasisi Ya Saratani Ocean Road(Orci)’’ alisema.
No comments:
Post a Comment