Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania PLC, Hilda Bujiku akizungumza kwenye mkutano na Wanahabari (hawapo pichani). |
Kampuni iliripoti mapato ya huduma ya Shilingi bilioni 956.5, ambayo yameshuka kwa asilimia 1.0 ikilinganishwa na mapato ya mwaka uliopita. Hii kwa kiasi kikubwa imeathiriwa na upotevu wa mapato ya Shilingi bilioni 103.8 yaliyotokana na tozo kwenye miamala ya simu kuanzia Julai 2021. Viashiria vingine vilivyoripotiwa ni mapato ya M-Pesa ya Shilingi bilioni 329.5, yakiwa yamepungua kwa asilimia 7.6 ikilinganishwa na Shilingi bilioni 356.8 iliyorekodiwa katika mwaka wa fedha uliopita. Hata hivyo jambo la kutia moyo ni mapato ya data ya simu, yaliongezeka kwa asilimia 18.9% na kufikia Shilingi bilioni 204.0.
Akizungumza na wanahisa, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya Vodacom Tanzania Plc, Jaji Mstaafu Thomas Mihayo, aligusia mazingira ya uendeshaji wa mwaka uliopita na uimara wa kampuni akibainisha kuwa Vodacom imeweza kudumisha nafasi yake ya uongozi katika soko nchini (market share) na maoni ya kuridhika kwa wateja, kwa kutumia kipimo kwa zana (Net Promoter Score – NPS).
“Ninaamini kuwa Kampuni ilikua na utendajikazi wa kuridhisha pamoja na mazingira ya biashara yaliyokuwa na changamoto. Utendaji huu unaonyesha uthabiti wa muundo wetu wa biashara, uimara wa menejimenti, na ubora wa utekelezaji wetu sambamba na jitihada zetu za kukuza ujumuishwaji wa kidijitali na kifedha,” alisema Jaji Mstaafu Mihayo.
Mwaka wa fedha wa 2021/22 ulikuja na uanzishwaji wa tozo kwenye miamala ya simu ambayo athari yake ilionekana mara moja huku wananchi wakitaka mapitio ya viwango hivyo. Ripoti ya kila mwaka ya Vodacom inaonyesha kuwa mapato ya M-Pesa yalipungua kwa asilimia 7.6. Mapato yatokanayo na huduma zisizo asilia za M-Pesa yalithibitisha kustahimili athari za tozo, huku ukuaji mkubwa wa mapato wa asilimia 26.1 yalitokana na huduma za mikopo kama vile ‘Songesha’ na M-Pawa. Huduma hizi zimekuwa muhimu katika kuwezesha wateja na mawakala kushughulikia mahitaji yao ya kifedha ya muda mfupi.
“Wakati athari za tozo kwenye mapato ya jumla ni vigumu kuzifuta, tunatiwa moyo na mtazamo wa wazi kutoka kwa serikali, kuhusiana na suala hili. Mnamo Septemba 2021, tozo zilipunguzwa kwa asilimia 30 na baadae zikapunguzwa tena kwa asilimia 43 kuanzia Julai 1, 2022, hivyo kupelekea jumla ya punguzo la asilimia 60 tangu kuanzishwa kwa tozo. Tunaendelea kutegemea ushirikiano endelevu ili kuboresha mazingira ya biashara,” alisema Mwenyekiti huyo wa Bodi.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji, Hilda Bujiku alisema pamoja na kuwepo kwa shinikizo katika mapato, mafanikio ya utekelezaji wa mkakati wa kampuni hiyo yameendelea kuleta matokeo chanya katika maeneo mengine muhimu, hivyo kuisaidia kampuni hiyo kusogea karibu zaidi na kufikia maono yake ya kuiongoza Tanzania katika ulimwengu wa kidijitali na kubadilisha maisha kupitia teknolojia.
“Mapato yetu ya data ya simu yaliongezeka kwa asilimia 18.9 ambayo kwa kiasi kikubwa inachangiwa na kuongezeka kwa mahitaji ya huduma za data. Matumizi ya data kwa kila mteja yaliongezeka kwa asilimia 22.3 kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya simu janja pamoja na uwekezaji endelevu katika mtandao wetu. Watumiaji wa simu janja waliongezeka kwa asilimia 12.1 hadi kufikia watumiaji milioni 4.1, wakiwakilisha ongezeko la asilimia 54.2 ya wateja wetu wa data,” aliongeza Bujiku.
Huduma za data zimebaki kuwa kigezo kikuu cha ukuaji kadri mahitaji ya data nchini yanavyoongezeka. Katika mwaka huu, kampuni iliwekeza Shilingi bilioni 174.0 katika matumizi ya mtaji, yaliyolenga kuboresha ubora wa mtandao kwa kuharakisha usambazaji na uboreshaji wa mfumo wa 4G na kuimarisha miundombinu ya TEHAMA. Hii ilikamilishwa na mpango wa kuunganishwa vijijini ambao tayari unahusisha minara 1,680, ikiwemo minara 283 iliyojengwa kwa ushirikiano na serikali kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF), ili kupanua mawasiliano kwa jamii za vijijini.
“Tunaendelea kutumia mtandao wetu mpana na mfumo wa ikolojia kwenye matumizi ya kidijitali kubadilisha maisha ya Watanzania zaidi kutumia muunganisho wetu huku tukitazama zaidi sekta za elimu, afya, mazingira na kilimo. Mwaka huu tumeboresha programu yetu ya M-Mama ambayo inalenga kupunguza vifo vya wajawazito, kupitia utoaji wa huduma za usafiri wa dharura kwa wajawazito na watoto wachanga hadi kwenye vituo vya kutolea huduma za afya katika maeneo ya vijijini nchini Tanzania” alisema Hilda.
Kwa upande wa thamani kwa wanahisa wake, kampuni ilitangaza kuwa hakutakuwa na malipo ya gawio mwaka huu kwani kampuni ilipata hasara katika mwaka uliochangiwa na shinikizo la mapato. “Uongozi unachukua hatua zote muhimu ili kuifanya kampuni kupata faida katika siku za usoni” alisema Hilda. Tangu ilipoorodheshwa kwenye soko la hisa zaidi ya miaka mitano iliyopita, Vodacom Tanzania imetoa jumla ya Shilingi bilioni 549.3 kama gawio kwa wanahisa wake ikijumuisha Shilingi bilioni 400 zilizolipwa kama gawio maalum.
Wakati wa Mkutano huu Mkuu, wanahisa pia waliwachagua kwa mara nyingine Wakurugenzi tofauti Wasio Watendaji kwenye Bodi ya kampuni hiyo huku aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa Vodacom Tanzania Plc Sitholizwe Mdlalose akijiunga na Kampuni kama Mkurugenzi Asiyekuwa Mtendaji, (Non-Executive Director).
No comments:
Post a Comment