Na Benny Mwaipaja, Dar es Salaam
Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba amesema kuwa uhusiano kati ya Serikali na Benki ya Dunia unazidi kuimarika na kwamba watanzania watarajie maendeleo makubwa kupitia ushirikiano huo.
Dkt. Nchemba amesema hayo katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam baada ya kumpokea Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Kusini mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa, aliyewasili nchini kwa ziara ya kikazi ya siku mbili kwa mwaliko wa Mhe. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.
Ameishukuru Benki ya Dunia kwa kuisaidia nchi kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo katika nyanja mbalimbali za kijamii na kiuchumi ikiwemo ujenzi wa miundombinu, elimu, afya, mazingira na mingine mingi kupitia mpango wa mikopo nafuu wa dirisha la IDA 19 ambao umemaliza muda wake na pia nchi inatarajia kupata fedha nyingine za kutekeleza miradi ya maendeleo kupitia dirisha jipya la IDA 20.
Kwa upande wake, Makamu wa Rais wa Benki ya Dunia anayesimamia Kanda ya Kusini Mashariki mwa Afrika, Bi. Victoria Kwakwa, amesema kuwa lengo la ziara yake nchini Tanzania ni kujitambulisha na kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na Benki hiyo baada ya kuchukua nafasi ya aliyekuwa Makamu wa Rais wa Benki hiyo Kanda ya Kusini Mashariki mwa Afrika Dkt. Hafez Ghanem, ambaye amestaafu.
Akiwa nchini, Bi. Kwakwa, anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu Jijini Dar es Salaam, baadae ataelekea Visiwani Zanzibar ambapo atakutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Mheshimiwa Dkt. Hussein Ali Mwinyi, na atakutana pia na Waziri wa Fedha na Mipango Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba na viongozi wengine kadhaa wa Serikali.
No comments:
Post a Comment