Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka ameagiza Jiji la Dodoma kuharakisha sheria ndogo ndogo za mazingira ili kuweka hali ya usafi katikati ya Jiji hilo.
Mtaka alitoa agizo hilo Kwa Naibu Meya wa Jiji la Dodoma, Emmanuel Chibago wakati wa kupokea vifaa vya kuhifadhia taka vilivyotolewa na benki ya NMB ili kusaidia utunzaji wa mazingira.
"Siku ile tulipata aibu kubwa, niliamua kuandika kwa mkono wangu kuomba vifaa hivi kwa benki ya NMB na leo wameleta,sasa naagiza vikabidhiwe kwa maandishi ili kila mmoja awe na wajibu wa kutunza na kuvifanyia kazi," alisema Mtaka.
NMB wamekabidhi jumla ya mapipa 100 yenye thamani ya zaidi ya Sh20 milioni wakiahidi kuendeleza ushirikiano na mkoa ili kuweka mji katika hali ya usafi.
Afisa Mkuu wa Fedha wa NMB, Juma Kimori alisema makabidhiano ya vifaa hivyo ni mipango ya benki hiyo katika kurudisha sehemu ya faida kwa wananchi baada ya kodi ambapo mwaka huu wametenga Sh.bilioni 2.9 ikiwa na ongezeko la 41% ukilinganisha na Sh.bilioni 2.05 za mwaka jana.
Kimori alisema walipokea ombi la vifaa vya kutunzia taka (dusty been) 350 kutoka kwa Mkuu wa Mkoa lakini kwa kuanza wametoa 100.
Awali Katibu Tawala wa mkoa Dkt Fatuma Mganga alisema baada ya makabidhiano hayo, sheria za usafi zitaanza kutekelezwa kwa mtu atakayetupa taka hovyo huku Dkt. Mganga akisema, awali ilikuwa ngumu kutekeleza sheria hiyo kwa sababu maeneo mengi hayakuwa na vifaa vya kuhifadhia taka hivyo kila mmoja alitupa kama anavyoona inafaa.
No comments:
Post a Comment