Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB Bw. Abdulmajid Nsekela akitoa hotuba yake kwa Wafanyabiashara na Wawekezaji walioshiriki katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma.
Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela akizungumza jambo na Mwenyekiti wa Chama cha Wawekezaji katika Sekta ya Hoteli Zanzibar, Paulo Rosso walipokutana katika Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia lililofanyika Jijini Roma.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela wakati wa Jukwaa la Biashara na Uwekezaji kati ya Tanzania na Italia liloandaliwa na Ubalozi wa Tanzania lililofanyika Jijini Roma, nchini Italia.
Nsekela amesema Benki ya CRDB ipo tayari kushirikiana na Serikali ya Awamu ya Sita pamoja na wawekezaji katika kuhakikisha kuwa changamoto zinazoendana na huduma za kibenki zinatatuliwa.
“Nawahakikishia kuwa Benki ya CRDB itawawezesha mikopo ya kuwekeza katika sekta mbalimbali hivyo msiwe na wasiwasi kuhusu mitaji ya kuwekeza ipo karibuni sana tuijenge Tanzania,” amesema Nsekela.
Nsekela ameongezea kuwa Benki ya CRDB inafarijika kuona wawekezaji wengi wameonesha nia ya kuwekeza zaidi Tanzania, huku akimpongeza Balozi wa Tanzania nchini Itali, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo kwa kuandaa Jukwaa hilo ambalo limetoa fursa ya kueleza sekta mbalimbali za uwekezaji zinazopatikana Tanzania.
“Benki ya CRDB pamoja na mambo mengine tutahakikisha kuwa sisi kama benki tunawawezesha wawekezaji wanaowekeza nchini na kuwapa mitaji ya biashara pamoja na biashara za kimataifa kati ya nchi moja na nyingine…,” alisisitiza.
Kwa upande wake Balozi wa Tanzania nchini Italia, Mhe. Mahmoud Thabiti Kombo ameipongeza Benki ya CRDB kwa utayari wake wa kusaidiana Serikali kuboresha mazingira ya uwekezaji nchini kupitia utoaji wa mikopo na mitaji, pamoja na huduma nyengine za kifedha zinazoongeza ufanisi katika uendeshaji wa biashira.
“Benki ya CRDB imeonyesha uzalendo mkubwa kwa kushirikiana na Serikali kuvutia wawekezaji kuja kuwekeza nchini, binafsi sina shaka na uwezo wao kimtaji. Nimefurahi pia wamekwenda mbele zaidi kwa kutoa huduma za ushauri katika uwekezaji, hii inaonyesha ni jinsi gani wamejipanga vizuri,” amesema Balozi Kombo.
Naye, Mwenyekiti wa Chama Wawekezaji katika Hoteli Zanzibar, Bw. Paulo Rosso amewasihi wawekezaji kutoka Italia kuwekeza kwa wingi Tanzania kwa kuwa mazingira ya biashara na uwekezaji ni tulivu na salama.
“Tanzania ni sehemu salama kuwekeza….nawahakikishia mimi nimewekeza Tanzania na ninaona ni sehemu salama ya kuwekeza karibuni sana kuwekeza kwa maendeleo ya Tanzania na Italia,” amesema Bw. Rosso
Jukwa hilo la biashara na uwekezaji kati ya Tanzania na Italia limehudhuriwa na Wafanyabiashara na Wawekezaji takribani 250 kutoka nchi zote mbili. Wafanyabiashara na wawekezaji hao ni wa sekta za utalii, kilimo, madini, na ujenzi.
Pamoja na mambo mengine, jukwaa hilo limewawezesha wafanyabiashara na wawekezaji kujadili fursa, uwezekano wa ubia, changamoto zinazokabili mazingira ya biashara na njia ya kuboresha mahusiano ya kibiashara kati ya nchi hizo mbili.
No comments:
Post a Comment