Benki ya Biashara ya DCB imeibuka mshindi kwa kutwaa tuzo ya Benki pendwa Tanzania inayotoa huduma bora kwa wateja katika kinyang’anyiro cha mwaka huu cha tuzo za Consumer Choice Awards Afrika 2021 (CCAA).
Hafla ya kukabidhi tuzo hizo za Consumer Choice Awards Africa 2021 zilifanyika jijini Dar es Salaam, lengo kuu ikiwa ni kuleta ushindani kati ya makamapuni na biashara mbali mbali barani Afrika, kuhamasisha utoaji huduma na bidhaa bora kwa wateja pamoja na kutambua kazi bora za watoa huduma.
Akizungumza jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mtendaji wa DCB, Godfrey Ndalahwa alisema "ushindi wa DCB katika kipengele cha benki inayotoa huduma bora kwa wateja ni faraja kubwa sana kwa benki hiyo kwani ushindi wa tuzo hizi unapatikana kwa kupigiwa kura na wateja, hii imeonyesha imani kubwa walionayo wateja wetu juu ya benki ya DCB".
“Hii ni mara ya kwanza DCB inashiriki katika kinyang’anyiro hiki, Tanzania ina idadi ya benki nyingi tu, kwa benki yetu kupata ushindi huu si kitu kidogo kwetu, ni imani yetu wateja wetu na watanzania kwa ujumla wataendelea kutuunga mkono ili tuweze kufanya vizuri zaidi.
“Sisi kama DCB tunaichukulia tuzo hii kwa mtazamo chanya zaidi tukiahidi kuendelea kutoa huduma bora zaidi na zaidi kwa wateja wetu tukiamini kuwa mteja kwetu sisi ndio mtaji wetu mkubwa kwa maendeleo na mafanikio ya benki yetu.
“Tuzo hii ni ushindi kwa wateja wetu, lakini pia ni ushindi kwa wafanyakazi wetu na menejimenti yetu kwa ujumla kwani bila jitihada na bidii zao DCB isingeweza kufikia kiwango hiki mpaka leo hii tumeweza kushinda tuzo hii”, alisema Bwana Ndalahwa.
Naye Mkuu wa Kitengo cha Masoko na Huduma kwa wateja wa DCB, Bi. Rahma Ngassa alisema DCB ni benki imara na imeendelea kukua na kufanya vizuri mwaka hadi mwaka, siri kubwa ya mafanikio ikijengwa katika kutoa huduma na bidhaa bora kwa wateja wetu.
Alisema ‘’Kama benki tumejiwekea mikakati kabambe ikiwemo huduma bora kwa wateja ni kipaumbele kikubwa. Benki imeweza kuweka njia mbalimbali rafiki za kuwafikia na kuhudumia wateja wetu.
Kwetu DCB mteja ni kila kitu na ndio maana kwa kuwajali wateja wetu tumeendelea kuingiza sokoni bidhaa na huduma zenye ubunifu wa hali ya juu zinazokidhi mahitaji ya soko tunalohudumia”, alisema.
Aidha Bi. Rahma alisema hivi karibuni DCB ilizindua kampeni ya miezi mitatu iitwayo ‘Sinia la DCB' hii ikiwa ni moja ya zawadi waliyowaletea wateja wao ikiwa ni sehemu ya shamrashamra za kuelekea msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka na pia sehemu ya shukurani kwa wateja wao.
“Tunapenda kutoa shukrani za dhati kwa wateja wetu kwa kutuwezesha kuwa Benki pendwa inayotoa huduma bora kwa wateja. Tunatoa wito kwa Watanzania kuendelea kutumia bidhaa na huduma za benki ya DCB ili kuendelea kupata huduma bora za uhakika na haraka.
No comments:
Post a Comment