Tanzania imesaini makubaliano ya mkopo wenye masharti nafuu wa thamani ya dola za Marekani milioni 116.34 (takribani shilingi bilioni 268.18) kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) kwa ajili ya ujenzi wa barabara ya kutoka Mnivata-Newala-Masasi mkoani Mtwara yenyeurefu wa kilomita 160 kwa kiwango cha lami.
Mkataba wa msaada huo umesainiwa jijini Dar es Salaam, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Bw. Emmanuel Tutuba, kwa niaba ya Serikali ya Tanzania na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB) Kanda ya Mashariki Dkt. Abdul Kamara.
Bw. Tutuba alisema kuwa kusainiwa kwa mkataba huu utaongeza kiasi cha fedha zilizotengwa kwa ajili ya miradi inayoendelea kutekelezwa na Serikali kupitia ufadhili wa Benki ya Maendeleo ya Afrika kutoka takribani dola za Marekani bilioni 2.27 hadi kufikia dola za Marekani bilioni 2.39.
“Hiki ni kiashiria tosha cha ushirikiano mzuri na wa muda mrefu wa maendeleo tangu mwaka 1971 kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Benki ya Maendeleo ya Afrika”, alisisitiza.
Alieleza kuwa fedha hizo pia zitatumika kujenga daraja la mto Mwiti lenye urefu wa mita 84, ujenzi wa stendi mpya za mabasi katika wilaya tatu (3) za Tandahimba, Newala na Masasi zinazonufaika na mradi, ununuzi wa magari mawili (2) ya kubebea wagonjwa na mashine mbili (2) za X-ray za kupima wagonjwa na utekelezaji wa mikakati ya usalama barabarani pamoja na mafunzo ya ujasiriamali kwa wanawake na vijana.
Bw. Tutuba alisema kuwa gharama za utekelezaji wa mradi ni dola za Marekani milioni 119.65 ambapo Benki ya Maendeleo ya Afrika imetoa dola za Marekani milioni 116.34 na Serikali ya Tanzania itachangia dola za Marekani milioni 3.31.
Aliongeza kuwa utekelezaji wa mradi huo unalenga kuimarisha miundombinu ya usafirishaji katika Ushoroba wa Maendeleo wa Mtwara ili kuchochea kasi ya maendeleo ya kiuchumi na kijamii na kupunguza umaskini kwa wananchi.
Bw. Tutuba, alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo utaunganisha Bandari ya Mtwara na Mikoa ya Kusini mwa Tanzania na kufungua masoko ya kikanda katika nchi za Msumbiji na Malawi.
Aidha, alisema kuwa kukamilika kwa mradi huo kutarahisisha shughuli mbalimbali za uchumi ikiwemo utafiti wa gesi, usafirishaji wa saruji, bidhaa za viwandani, pamoja na mazao ya kilimo likiwemo zao la korosho.
Bw. Tutuba alisema Serikali itaendelea kufanya kazi kwa karibu na Benki ya Maendeleo ya Afrika ili kuimarisha ushirikiano wa kimaendeleo.
Kwa upande wake Naibu Mkurugenzi Mkuu wa Benki ya Maendeleo wa Benki ya Maendeleo (AfDB) Kanda ya Mashariki Dkt. Abdual Kamara, alisema kuwa kukamilika kwa ujenzi wa barabara hiyo kutawezesha kuendeleza maeneo ya vijijini kwenye Ukanda huo wa Maendeleo wa Mtwara na kufanya eneo lote la barabara ya lami kufikia kilometa 816 hivyo kuchochea maendeleo ya maeneo hayo ikiwemo Bandari za Mtwara na Mbamba Bay katika Ziwa Nyasa.
“Mradi huo utarahisisha usafirishaji wa abiria na mizigo katika ukanda wa Afrika na nchi jirani ya Msumbiji, Malawi na Zambia ambazo zitahudumiwa na Bandari ya Mtawara”, alisisitiza Dkt. Kamara.
Dkt. Kamara alisema kuwa mradi huo unatarajiwa kuleta manufaa makubwa katika uchumi wa nchi ambapo inakadiriwa kuwa utachangia uchumi kwa zaidi ya asilimia 20.6 utakapo kamilika.
Kusainiwa kwa mkataba huo utaongeza ufadhili wa benki hiyo hapa nchini, kwenye Sekta ya barabara kwa kiwango cha dola za Marekani bilioni 1.52 ikiwa sawa na asilimia 82 ya fedha zilizowekezwa na benki hiyo hapa nchini unaofikia takribani dola za Marekani bilioni 2.47 ambazo kwa kiwango kikubwa zimeelekezwa kwenye Sekta ya miundombinu ikiwemo usafirishaji , nishati pamoja na maji na usafi wa mazingira.
Dkt. Kamara, ameipongeza Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango kufanikisha upatikanaji wa mkopo huo na kusisitiza umuhimu wa kusimamia kikamilifu utekelezaji wa mradi huo ili ulete manufaa yaliyokusudiwa kwa wakati.
Akizungumzia utekelezaji wa mradi huo, Mtendaji Mkuu wa Wakala ya Barabara Tanzania, Mandisi Rogatus Mativila alisema kuwa wamegawanya katika awamu mbili na kwa kuanzia wataanza na kipande cha Mnivata hadi Mitesa kilomita 100 kupitia Newala na awamu ya pili itakua kipande cha kutoka Mitesa hadi Masasi kilomita 60 ikihusisha ujenzi wa daraja la Mwiti.
Aidha mradi huo utahusisha pia ujenzi wa miradi mbalimbali ya kijamii ikiwemo vyumba vya madarasa, nyumba za walimu na madaktari na mashine za kubangulia korosho na maghala ya kuhifadhia korosho.
Aliahidi pia kusimamia utekelezaji wa mradi huo kwa weledi kwa kuzingatia vigezo vyote vilivyowekwa ili uweze kukamilika kwa wakati kama ilivyokusudiwa.
No comments:
Post a Comment