Kikundi cha ngoma kutoka Makumira Arusha kikitumbuiza wakati wa maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki leo Jijini Arusha. |
Kikundi cha ngoma kutoka Sudan Kusini kikitumbuiza wakati wa maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki Jijini Arusha. |
“Nawapongeza kwa kufanikisha maonesho haya ni imani yangu kuwa kupitia maonesho haya nchi zetu za ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki zimepata fursa ya kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii pamoja na kujadili njia mbalimbali za kukabiliana changamoto zinazoikabili sekta ya Utalii katika ukanda wa Afrika Mashariki,” Amesema Dkt. Mwinyi
“Natoa wito kupitia maonesho haya ambayo yatakuwa yanafanyika kila mwaka kwa mzunguko kwa kila nchi mwanachama……..jitihada zaidi zinahitajika katika kutangaza vivutio vya utalii katika ukanda wetu wa Afrika Mashariki ikiwa ni pamoja na kuboresha sera zetu za utalii,” ameongeza Dkt. Mwinyi
Dkt. Mwinyi pia ameitaka Kamati Maalumu ya Kikanda ya Jumuiya ya Afrika Mashariki kufanya ziara Zanzibar na kujionea fursa mbalimbali zinazopatikana katika sekta ya utalii pamoja na zile za biashara na uwekezaji.
Awali Waziri wa Maliasili na Utalii, Mhe. Dkt. Damas Ndumbaro amesema kupitia maonesho haya ya kwanza katika ukanda wa Afrika Mashariki yamekuwa na mafanikio makubwa ambapo zaidi ya waoneshaji 100 kutoka mataifa mbalimbali duniani wameshiriki, kati yao 41 wakitoka mataifa mbalimbali na nchi 25 zikishiriki ikiwa ni pamoja na sita za Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Nae Waziri wa Uhifadhi wa Wanyamapori na Utalii kutoka Sudan ya Kusini Mhe. Luteni Jenerali Rizik Zakaria Hassan ameipongeza Tanzania kwa kufanikisha maonesho ambayo yemeweza kuvitangaza vivutio mbalimbali vya utalii ndani ya ukanda wa Afrika Mashariki ambayo pia yametoa fursa ya kujadili changamoto zinazoikabili sekta ya utalii.
“Maonesho haya yemekuwa na manufaa makubwa sana kwa kutuweka sekta ya utalii ndani ya jumuiya ya Afrika Mashariki ……….binafsi nawapongeza sana Tanzania kwa kulifanikisha jambo hili muhimu kwetu, naamini kupitia maonesho haya tutazidi kuimarika ziadi kama jumuiya kwa maendeleo yetu sote,” Amesema Luteni Jenerali Hassan.
Kwa upande wake Mkurugenzi wa Forodha na Biashara Jumuiya ya Afrika Mashariki, Bwn. Keneth Bagamuhunda ambaye alimwakilisha Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Mhe. Peter Mathuki, amesema maonesho yalilenga kutoa fursa kwa kila nchi mwanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki kutangaza vivutio mbalimbali vya utalii ili kuifahamisha Afrika na Dunia kuwa ndani ya Afrika Mashariki kuna vivutio vya utalii.
“Tutaendelea na maonesho haya kwa kila mwaka lengo likiwa ni kutangaza utalii na kuhakikisha soko la utalii ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki linakuwa kila mwaka,” Amesema Bwn. Bagamuhanda.
Kwa upande wake, Waziri wa Utalii na Malikale wa Zanzibar, Mhe. Leila Mohamed Mussa (Mb) amesema Afrika kwa sasa inatakiwa fursa za utalii na biashara ili kuweza kuziongezea Serikali zetu mapato.
“Afrika Mashariki inayo mambo mengi ya kutoa katika bara la Afrika na Duniani kwa ujumla hasa katika sekta ya utalii kwa kuwa tumejaliwa vivutio mbalimbali vya utalii,” amesema Bibi Leila Mohamed Mussa.
Oktoba 09, 2021 maonesho ya kwanza ya utalii kwa nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika mashariki yalizinduliwa rasmi na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Dkt. Peter Mathuki jijini Arusha.
Kufanyika kwa maonesho hayo kunatokana na kuzinduliwa hivi karibuni mpango wa pamoja kutangaza utalii katika nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika ya Mashariki uliozinduliwa rasmi na Mawaziri wa Maliasili na Utalii wa Jumuiya ya Afrika Mashariki.
Maonesho hayo yalihudhuriwa na nchi wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ambazo ni Tanzania (Mwenyeji), Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.
No comments:
Post a Comment